HATUPIMI BANDO

11 September 2017

HOTUBA YA BABA MKWE ILIKUWA YA MWAKA


Yaani baba mkwe katoa mpya juzi, mpaka sasa bado sijajua nicheke au nisikitike, maana nasema tena baba mkwe katoa mpya. Juzi Jumamosi tulifanikisha sherehe ya harusi ya mtoto wa kiume wa rafiki yetu. Sisi ndio tulikuwa wanakamati hivyo kwanza nijisifu tuliwezesha bonge ya harusi, japo huwa nawaza tu ule mkwanja tuliokusanya wangepewa hawa maharusi hakika wangemaliza umasikini na kuanza maisha ya kifahari, lakini ndio hivyo tena tulipanga kutumia mamilioni yote yale kwa ajili ya kula na kunywa kwa masaa machache tu.

Turudi kwa baba mkwe, sherehe ilianza vizuri kabisa, MC alikuwa mmoja wa wale ma MC ambao wanapenda kusikia sauti zao wenyewe basi anaongea huyo, kila jambo analirefusha mpaka inachosha. Hatimae ikafika wakati MC akatutangazia kuwa baba mkwe anataka kuja kutoa wosia. Binafsi kipengele hiki huwa kinanichekesha sana, kama mtoto hakupewa malezi mazuri, haka kahotuba ka dakika za mwisho ndio kweli katarekibisha tabia zao kweli? Tuache hayo, baba mkwe akakamata maik, akasalimu ‘Mambo?’. Hapohapo nikashtuka, nikaona baba mkwe huyu wa kileo sana, baada ya kumcheki vizuri nikagundua kuwa kinywaji alichokuwa amekunywa vimemchangamsha kidogo. Baba mkwe baada ya kujibiwa salamu zake akaanza hotuba ambayo sitaisahau mapema. ‘Kijana upo? Naona umeamua kumuoa binti yangu, mimi kama baba yake nasema wazi inaonekana humfahamu binti yangu vizuri, mtu anaemfahamu binti yangu hawezi kufanya uwenda wazimu wa kutaka kumuoa huyu mtoto’. Dahh ukumbi mzima ugeuka kimyaa, bibi harusi alikuwa kajiinamia. ‘Huyu binti yangu ni mkorofi katusumbua sana mimi na mama yake, toka alipofikisha umri wa miaka kumi na sita. Kafukuzwa shule tatu, kila shule ikilalamika kuwa anawaharibu wanafunzi wenzie. Hatimae shule ikamshinda, kifupi sijui haswa baada ya hapo alikuwa anaishi wapi. Japo mara chache alikuwa analala nyumbani. Huyu binti yangu hebu fikiria hata instagram walifungia ukurasa wake kutokana na picha alizokuwa akiziweka humo. Nadhani kijana ulimuona picha zake kwenye magazeti ukaona umepata malaika, hafai kabisa huyo hafai. Nimeona nikueleze ukweli usije baadae kunilalamikia mashetani yake yakimpanda. Mimi na mama yake sasa tunaondoka, tulikuja kuwaonya tu ili msije kutusumbua baadae, pole kijana wangu’ Baba mkwe, mama mkwe, mashangazi, wajomba, makaka haooo wakasepa.

No comments: