HATUPIMI BANDO

26 August 2017

MJINI KUMEJAA MACHIZI

YAANI hapa mjini ukipaangalia kwa makini unaweza ukajikuta unacheka peke yako barabarani watu wakadhani we chizi kumbe unakumbuka uchizi wa wakazi wa mjini. Yaani kuna vitu watu wanafanya havieleweki, wanajitengenezea mazingira ya kupata matatizo makubwa. Hebu we fikiria, jamaa anakuwa na mabinti 15 kila mmoja anamwambia anampenda kuliko kitu chochote duniani. Wote hao wanamuangalia yeye kwa matumizi yao ya kila siku ili waonekane wa maana mjini, na wote wamemuomba awanunulie simu, wengine Samsung model mpya, wengine iPhone6 na wote amekubali maombi yao, baada ya hapo anaanza kuhangaika kuuza hata mali zake na za kazini kwake ili afurahishe timu yake ya wapenzi. Sasa kwanini nisicheke peke yangu? Wakati huo fala huyu anatakiwa kulipa kodi ya nyumba yake ale vizuri apeleke matumizi kwa wazazi wake, yaani kama sio uchizi huo ni nini? Halafu kuna hawa jamaa ambao wako kibao hapa mjini, utawakuta kila siku baa. Hawa wanaanza siku na kilo mbili za mishkaki na ndizi tatu, kachumbari pembeni, baada ya hapo chupa zinaanza kuteremeshwa na ofa kutolewa kwa marafiki na mashabiki. Na wakati huo zoeezi la kuagiza nyama na supu ya pweza linaendelea tena na tena, kimsingi mpaka jamaa anaamua kuelekea nyumbani kwa mke na watoto wake wane amekwisha tumia kitu kama laki mbili kwa masaa manne. Sasa kwake sasa, watoto wamekula ugali kwa mchicha, tena unga wenyewe ulikuwa hautoshi wamelala na njaa, watoto wamelalia kigodoro cha nchi moja wakishindana kuvutana shuka moja, yeye mwenyewe anapokuja kulala ni juu ya godoro limechoka kabisa anajifunika kanga ya mkewe. Mke alimuachia shilingi alfu tatu asubuhi. Sasa kama sio uchizi huu ni nini sasa? Asubuhi anaamka ana shilingi alfu tano anajifanya mtu mzuri anamwambia mkewe, ‘Tugawane hii we chukua alfu tatu mi nipe alfu mbili hali ngumu mke wangu’. Pambafu.
Halafu machizi wengine ni hawa wazazi ambao mzee mfanya kazi mshahara wake laki nne kwa mwezi, mkewe mama ntilie anauza maandazi, kila saa kumi alfajiri anakuwa tayari yuko mtaani anajaribu kukusanya shilingi alfu mbili tatu, wazazi hawa wakikusanya kipato chao kwa mwezi hakifiki laki saba. Wana binti yao yuko kidato cha pili, ana simu kali mbili, kila moja bei yake si chini ya laki nane. Wazazi wanaona poa tu, hawajui wapi kapata simu, wapi anapata vocha. Tena mara nyingine wanamuomba awapigie simu ndugu na jamaa, kama sio uchizi ni nini? Wacha nicheke barabarani peke yangu mie.

No comments: