PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

HIZI NDOA HIZI WE UZIONE HIVIHIVI


Hahahahaha kazi kwelikweli, juzijuzi kazini kwetu kulitangazwa semina ya siku moja ya wanaume waliooa. Kuna taasisi inayohusika na jinsi ya kuendeleza familia zenye Amani, ilifika kazini kwetu na kututangazia kuwa wanaume wote walio katika ndoa wahudhurie semina  bila kukosa, bosi wetu akajitolea kulipia chai na chakula cha mchana. Hii ishu sikutaka inipite, kwanza nilikuwa na maswali mengi sana nilitaka kujua jinsi ya kurudisha penzi la awali na mke wangu, nilitaka mambo yarudie enzi zile ambapo kila niliporudi nyumbani nilikuta katandika kitanda vizuri na juu yake kaweka maua. Nilikuwa nakuta chakula kimefunikwa kawa lenye maneno matamu ya mahaba. Nikitoka kidogo hata kama nilienda mtaa wa pili kucheza bao, nikirudi namkuta waif kabadili nguo ananikaribisha utadhani nilisafiri wiki. Nilikuwa natamani enzi zile zirudi tena

Basi semina ilianza  kwa maelezo mengi na mifano mingi sana. Mchana baada ya kula, kila mtu aliambiwa amtumie mkewe meseji kwenye simu. Meseji rahisi tu, aandike neno NAKUPENDA na kulituma kwa mkewe. Basi kila mtu akaandika na kutuma, baada ya hapo tukaambiwa kila mtu ampe jirani yake simu yake. Haikuchukua muda mrefu milio ya mesej za majibu zikaanza kusikika , watu wote tulikuwa kimya. Kisha muwezeshaji wa semina ile akaomba walioshika simu waanze kusoma majibu yaliyorudi kwenye simu. Ngoma ilianza hapo. Simu ya kwanza ilisomwa jibu lilikuwa, ‘Vipi baba Jeni, kuna nini?’. Iliyofuata,’Labda enzi hizo siyo sasa’, nyingine ikajibu, ‘Sikukopeshi tena huwa hurudishi hela zangu’, nyingine ikarudi imeaandikwa, ‘Umefanya nini tena? Safari hii sikusamehe?’ Tulianza kucheka sasa, ikasomwa meseji nyingine mke akajibu,’Sijakuelewa’. Nyingine ikajibu,’Ni wimbo mpya wa Diamond?’, mke wangu nae akajibu, ‘Usiponambia meseji hii ilikuwa inaenda kwa nani, usirudi’. Mwenzangu mmoja akapata swali,’Nani mwenzangu?’ Bosi wetu nae alipata jibu toka kwa mkewe, lilikuwa onyo, ‘Sinilikwambia uache kulewa mchana mume wangu’. Ila kulikuwa na meseji moja ya jamaa yetu wa uhasibu ambaye mnoko sana wakati wa kutulipa mafao yetu, ila tulimuonea huruma alipoanza kutoa machozi kutokana na jibu la mkewe ambaye inaonekana alijichanganya na kujibu,’We vipi nilikwambia usiwe unanitumia meseji za hivi mume wangu akiziona itakuwa shida’  Na simu ya afisa utumishi ilikuwa na  swali, ‘Vipi umemjaza mimba mtumishi mwingine?’. Tumetoka kwenye semina tumechanginyikiwa kuliko tulivyoingia.

Comments