HATUPIMI BANDO

27 April 2017

BINGWA WA NDOTO MUBASHARA


KILA  binadamu ana mambo yake mengine ya ajabu sana ukihadithiwa huwezi kuamini. Kuna mshikaji wangu mmoja wanamuziki maarufu sana, ila ana ishu yake moja watu wangejua stori yake ndio ingekuwa kichwa cha habari cha kila gazeti. Mshikaji wangu huyu mtu mmoja smati sana kabla hajatoka nje ya nyumba yake lazima ajicheki kama yuko vizuri ndio anatoka nje. Nyumbani kwake ana vioo vikubwa vitatu vyote vya kujiangalia kabla hajatoka, akiwa na unauhakika na anavyoonekana ndio anatoka. Ukijidai kumuwahi asubuhi ukimgongea kama hajajitayarisha hafungui mlango. Kuna watu walisha mzushia aeti anafuga majini, na majini yake hayataki uchafu, si unajua wabongo umbeya uko kwenye damu. Basi mshikaji huyu jina simtaji hapa maana siku hizi ukimtaja mtu jina, mabingwa wa umbeya wanamfuata mtu kwenye instagramu, wataanza kumpaka humo utadhani walikuwa nae jana kumbe hata sura wanaijulia kwenye gazeti. Unajua siku hizi umbea umegeuka dili, kuna watu wanapata umaarufu siku hizi kwa mtaji wa kuwapaka watu kwenye instagramu. Basi hapa hampati mtaji huo.   Sasa mshikaji wangu huyo tatizo lake ni staili yake ya kuota. Jamaa akipata usingizi akianza kuota tu basi huanza kufanya shughuli anazoota mubashara kabisa. Yaani akiota yuko dansini basi ataamka atashika gitaa lake na kuanza kupiga, ukimkuta utadhani yuko macho kumbe mwenzio yuko usingizini anaota hivyo. Sio mara moja anatoka chumbani kwake na kwenda mpaka mtaa wa pili na kurudi kuendelea kulala, asubuhi ndipo huwa anaamka anajikuta na matope miguuni, kutokana na kukanyaga madimbwi kwenye safari zake. Juzi juzi sasa katoa kali, mshikaji aliota kakaribishwa kwenye pati ikulu. Alivyonihadithia mwenyewe alisema alikaribishwa mlangoni na mheshimiwa Rais mwenyewe, kufika ndani akakutana Mawaziri wakasalimiana sana, akaomba sigara wakampa akavuta kisha wakaenda kula. Msosi ulikuwa wa nguvu sana, kila alichotaka alikula, mwenyewe anasema Rais alikuwa anamhamasisha ale vizuri, basi hatimae akashiba akaomba kuondoka. Kabla hajaondoka akajisikia anahitaji kujisaidia ndipo akaonyeshwa mahala pa kujisaidia, akaingia na kushusha mzigo vizuri tu. Aliposhtuka akajikuta yuko chumbani kwake kitandani, lakini chumba kinanuka harufu mbaya sana, halafu nusu ya mto mmoja aliokuwa amelalaia umetafunwa, akili ikamrudia akakumbuka ndoto aliyoota, ikawa kazi moja tu kuanza kufua mashuka na kupiga pafyumu chumba harufu ipungue, alipomaliza akaenda hospitali kumueleza dokta mkasa wake wa kutafuta mto wa sponji.

21 April 2017

NAJUA TU WENYE ROHO MBAYA WAMENIROGA


 Yaani mi naona nina kamakosi fulani, toka nizaliwe sijawahi kupata mrembo wa nguvu. Yaani kila mara inatokea ishu ya kuniwekea kipingamizi cha kupata mrembo ambae ana mvuto wa pekee. Yaani naona wazi kuna mkono wa mtu. Kuna watu sijui roho zao zikoje, wao wanapenda kuona mtu anateseka hata kama wao hawapati kitu, yaani ni  roho mbaya tu imamfanya mtu ana kuwekea kagundu fulani basi warembo unapishana nao, wanakupita hivi hivi mubashara hawakuoni kabisa hata uwe umevaa nini. Kwa upande wangu na hili gundu limeanza miaka mingi sana kwanza nilikuwa sijalistukia, lakini sasa nimesha jua mambo sio sawa, kuna haja ya kutafuta mtaalamu, nisafishe nyota. Nyenzo moja muhimu sana ukitaka kupata warembo wa ukweli ni kuwa na simu inayoenda na wakati. Nimegundua kuna mtu kachafua nyota yangu ya kupata simu kali. Unaweza kucheka lakini hilo ndilo gundu nililo logelezwa, nyota ya kupata simu za kisasa imefukiwa kaburini. Warembo wa ukweli wanamaindi sana aina ya simu uliyonayo, sasa mimi nimefanyiwa kitu kila mara nakuwa sina simu inayoenda na wakati. Enzi zile wakati simu za twanga pepeta zinatamba, mi nilikuwa sina simu kabisa, warembo wote wa ukweli walinikataa sababu hiyo. Nikahangaika nikaja kupata kasimu kangu ka twanga pepeta, kumbe warembo wamehama wanataka watu wenye blek beri, kila ninae jaribu kumuingia akishagundua nina twanga pepeta ananitolea nje tena kwa kashfa. Nikajinyima nikaja kupata blek beri yangu, nikawa nairingishia hata kujaribu kuwaonyesha, warembo kila nilipowakuta, baada ya muda  nikagundua wananicheka kumbe wajanja walishahamia simu nyingine, watu wakawa wanakutana whatsapp sijui insta, mie nikawa siko huko, basi nikachakalika nikapata na mie simu yenye whatsapp, ile naanza kujisifu nakuta wameanza kutumia simu za kupangusa, nimestrago nimepata ya kupangusa hawaniangalii mpaka nipate iphone, jamani nina mkosi gani? Sasa kununua iphone ni mtihani, nikijinyima sana naweza nikawa na iphone  mwisho wa mwaka , lakini najua tu staili nyingine ya simu itakuwa imeanza , siku nikimjua aliyeniroga namtoa kongosho

17 April 2017

UTAJUAJE KAMA UMEROGWA? SOMA HAPA


Je, umerogwa? Kuna  watu wengi wanatembea bila kujijua kama wamerogwa. Blog yako hii sasa imeamua kusaidia wananchi kama hawa ili wajijue kama maisha yao yameingiliwa na mkono wa mtu. Kutokana na roho nzuri sana ya mkuu wa blog hii , mtaalamu kutoka mkoa mmoja ambao hautatajwa hapa kuepusha wabaya, ameajiriwa na blog na analipwa kwa fedha za kigeni ili kusaidia  kutoa ushauri hata tiba kwa wale ambao wamejikuta wamelogwa. Kitu cha kwanza ni kujua kama umelogwa au la, zifuatazo ni dalili za wazi kuwa maisha yako yako chini ya mkono wa mtu. Tutakuwa tunaongeza ishara hizi kila zitakapokuwa zinatokea, naomba nimuachie mtaalamu aeleze dalili za kujua umelogwa
Kimsingi ukiwa na moja kati ya yafuatayo tuandikie chini kwenye comment tujue namna ya kukushauri;
1.   Ikiwa umefanya kazi katika kampuni shirika au kwa mtu binafsi miaka kumi bila kupandishwa cheo au kuongezwa mshahara.
2.   Kama ulifeli Kiswahili na hesabu kwenye mitihani yako
3.   Kama kila ukimuona mwanajeshi unapata hisia za kumzaba kibao
4.   Kama una gari linalokuwa muda mwingi zaidi gereji kuliko barabarani
5.   Kama wewe ni mpenzi damu wa Arsenal
6.   Kama kila ukipigwa picha unatoka hujapendeza
7.   Kama mwanao wa pekee anabwia unga
8.   Panya wamekula jina lako tu kwenye vyeti vyako vya elimu.
9.   Ukijikuta unachelewa ndege
10.              Ukijikuta unanyang’anywa pointi za ligi.
11.              Unapokosea na kutumia super glue badala ya matone ya dawa ya macho.
12.              Ukijikuta unaota unatekwa.
Kwa leo mtaalamu ametuacha hapa tukutane tena baada ya siku chache kuongezewa dalili za kurogwa. Tafadhali tuandikie kama unaona kuna kitu kinakuhusu

12 April 2017

HUWA SIINGILII MAMBO YA FAMILIA ZA WATU


Waalimu wa hesabu enzi za shule ya msingi walikuwa na maswali mengine ya ajabu ajabu, hebu fikiria swali kama hili unalikuta kwenye mtihani;
John ana miaka 10 pungufu ya baba yake. Mama yake ana miaka 40, miaka 20 zaidi ya John. Tafuta umri wa
a)  John
b)  Baba
c)   Mama
Swali kama hili nilikuwa naruka. Mimi sio mbeya wa kufwatilia familia za watu wengine.

6 April 2017

HATA MBWA HUWA WANAFUKUZIA MAGARI

BABU: Mke wangu huwa unaona wivu ninavyofukuzia vibinti vidogovidogo?
BIBI: Wala, mbona hata mbwa huwa wanafukuzia magari japo kuwa hawawezi kuya endesha?