HATUPIMI BANDO

31 March 2017

WAKUJA ADAI FEDHA ZAKE ALIZONUNULIA DAWA YA AMAPENZI FEKI


Jana nimepita nacheka kwenye mitaa ya kwetu, watu wengine wakawa wananiangalia kwa jicho la kujiuliza, najua walikuwa wakidhani nimevuta moshi wa kitu kilichopigwa marufuku, najua wengine watakuwa walikuwa wananionea huruma wakijua kuwa akili yangu imepata msukosuko kidogo. Mi sikujali niliendelea kujipa raha mwenyewe na kucheka zaidi. Mkasa niliokuwa nimeuona hata wewe ungekuweko ungecheka wiki nzima. Nilikuwa nimekatisha  kwenye uchochoro mmoja ili niwahi kufika nyumbani, si unajua sie Wabongo kwa vichochoro ndio wenyewe, mambo ya kufuata barabara kama magari sie hatuwezi kabisa. Basi nikakatisha kichochoro kimoja, huko nikakuta kuna kelele ugomvi mkubwa unaendelea, watu walishaanza kukusanyika, kama kawaida ya Mbongo yoyote, lazima kujionea mweyewe kila tukio mubashara, nikajipenyeza kuona kulikoni. Lohh hapo ndipo nilipoanzia kucheka, jamaa mmoja alikuwa kamkunja mwenzie ambae kavaa mavazi maarufu kuvaliwa na Wamasai, sasa kwa vile kakunjwa shuka na kwa vile hakua na vazi jingine, nusu ya mwili ulikuwa hadharani. Huyu mkunjaji kwa lafudhi lazima alikuwa ametokea maeneo ya Kanda ya Ziwa, alikuwa anadai hela yake. Inaonekana kuna siku hawa wawili walikutana sehemu, Mmasai akiwa anauza dawa mbalimbali za kiasili, jamaa yangu kutoka Kanda ya Ziwa akaulizia kama Masai ana dawa ya mapenzi akaambia ipo na inasemekana bei ilikuwa shilingi arobaini elfu. Jamaa wa poti akazitoa na kurudi na dawa nyumbani kwa furaha kubwa akijua kuwa yule kimwana wa Kizaramo aliyekuwa akimtamani siku nyingi dawa yake imeshapatikana. Tatizo kubwa lilitokea siku alipofuata masharti yote na kisha kuelekea kwa kimwana ambae alikuwa chaguo la moyo wake. Alipofika akaanza kufuata masharti ya mwisho ambayo yalihusu kuzunguka nyumba ya kimwana na kisha kuchota mchanga kidogo na kuweka mfukoni na hapo ni kumfuata kimwana na kumgonga bega, mambo yote mazuri yangeanzia hapo, eti kimwana angemkumbatia  na kuanzia hapo kuwa mali za Wapoti. Tatizo ni kuwa baada ya kufuata masharti yote ya Masai, Poti akaishia kutandikwa makofi na kumwagiwa maji ya ukoko wa ugali wa ulezi na yule kimwana na pia kutishiwa kupelekwa polisi.  Kuanzia siku hiyo wa Poti alikuwa akimtafuta Mmasai ili kurudishiwa pesa yake, sasa jana wamekutana.  Palikuwa patamu hapo …..instagram@johnkitime

22 March 2017

KUMBE SISI MABOSI FEKIMarekani wamempata Rais, hata siku mia haja timiza, lakini hakika dunia nzima tunamsikia kwa mambo yake, mwenyewe anapenda mtandao wa twita huyo, haoni tabu kumkandia mtu kwenye twita. Sio mara moja anaviita vyombo vya habari, kuwa mabingwa wa taarifa feki.  Watu wote tulikuwa tunaamini kila kinachotangazwa na vyombo vya Marekani sasa tumezinduliwa, Rais wao mwenyewe anaviita feki. Nimekaa hapa nikawa nawaza nikaona na sisi huku kwetu kuna vitu kama vina harufu ya ufekifeki hivi. Yaani nimekaa nawaza hawa watu wanaoitwa na mara nyingine wao wenyewe wanajiita , watumishi wa umma. Unajua ukiwa mtumishi ina maana unamtumikia bosi wako, kwa hiyo mtumishi wa umma , bosi wake ni umma si ndio? Ina maana mimi na wewe ni mabosi wa hawa watumishi wa umma si ndio? Sasa mbona mambo yako kinyume? Wao mbona wanaekti kibosi na kutufanya sisi umma ndio vidampa, au ndio kusema sisi mabosi feki? Au sio?. Juzi nimeenda ofisi moja ya umma, nikawa naenda kwa mikogo nikijua mi ndio bosi nikataka kumuona mtumishi wa umma mmoja. Kufika pale nikaambiwa nimsubiri anahudumia wengine, poa nikakaa nje ya ofisi ya umma ambako kuna kaukuta kamejengwa kama benchi hivi, watu wengine watatu wakaniunga mkono. Akaja mtumishi wa umma moja ambaye ni mlinzi wa pale, akaanza, ‘Kwanini mnakaa hapo? Hebu tokeni hapo” Tukamuuliza “Sasa tukakae wapi?” Tukijua jamaa anajua sisi ndio mabosi wake. Akatujibu “Mie sijui ila tokeni mkakae hata kule barabarani”, nikajiona mi bosi feki kweli, huyu mtumishi wa umma anatufukuza umma, yaani anafukuza  mabosi wake?
Halafu hawa watumishi wetu  wanajua kuna watu wengi huwa wanakuja kutaka huduma na wanahitaji mahala pa kukaa, hawatengenezi mahala pa kukaa sisi mabosi wanaishia kutufukuza. Tena usije ukakosea ukakaa karibu na kituo cha polisi,  utatimuliwa ushangae mwenyewe, ole wako uulize, “Afande sasa nikakae wapi? Utaishia nyuma ya kaunta, na sio ya baa.

20 March 2017

TUJITAHIDI KUCHEKA, HATA SYRIA IMETUZIDI KWA FURAHA


Haya tena taarifa ya Umoja wa Mataifa ndio imetoka na Norway ndio nchi yenye furaha nyingi kuliko zote duniani. Kwa miaka miwili iliyopita Norway ilikuwa ya nne na Denmark ilikuwa ya kwanza, mwaka huu Norway imekuwa ya kwanza. Mwaka huu nchi ya pili imekuwa Denmark, ikifuatiwa na Iceland, Switzerland, Finland, Netherlands, Canada, New Zealand. Nchi za Australia na  Sweden kwa pamoja zimekuwa za tisa. Kwa mwaka huu Marekani ya 14, Ujerumani ya 16, Uingereza ikichukua nafasi ya 19. Urusi ni ya 49, Japan ya 51 wakati China ni ya 79. Nchi ya Rwanda ni ya 151, Syria ya 152, Tanzania ya 153, Burundi ya 154, nay a mwisho ni Central Afrika Republic. Kati ya mambo yaliyopimwa yalikuwa ni afya, kuwa na mtu wa kumtegemea, uhuru wa kuamua cha kufanya maishani, uhuru wa kutoka na janga la rushwa

HE JAMANI MBONA MFALME HAJAVAA KITU?


Leo sijui kwanini nimekumbuka hadithi moja ya Abunuwasi. Hapo zamani za kale Abunuwasi alimuendea mfalme akamwambia anaweza kumshonea suti ya thamani sana ambayo wenye dhambi watakuwa hawaioni na wasio na dhambi tu ndio watakuwa wanaiona. Mfalme akampa kazi Abunuwas ya kutengeneza suti ya aina hiyo kwa ajili yake. Kwa siku kadhaa Abunuwasi alijifungia katika chumba akawa bizi anashona suti ya mfalme. Baada ya siku tatu, mfalme akamtuma msaidizi wake akaangalie kazi inavyoendelea, yule msaidizi akaingia chumba alichokuwa akishonea Abunuwasi lakini hakuona kitu japo alimuona Abunuwasi akifanya vitendo kama vile yuko bizi anashona nguo. Msaidizi akamwambia Abunuwasi, ‘Nimetumwa na mfalme niulizie umefikia wapi?” Abunuwasi akamjibu, “Kwani we huoni jinsi suti ilivyoanza kupendeza, ila bado namalizia nguo nyingine nataka kuanzia nguo za ndani ziwe ni hizi za kitambaa ambacho hakionekani kwa wenye dhambi”. Hakika yule msaidizi alikuwa haoni kitu lakini ili aonekane hana dhambi akaanza kusifu jinsi nguo zilivyoshonwa kwa ufundi. Akatoka na kurudi kumueleza mfalme kuwa Abunuwasi kamshonea nguo nzuri sana si za dunia hii kwa jinsi zilivyo nzuri. Mfalme alifurahi sana, kesho yake akamtuma msaidizi mwingine, nae kama yule wa jana akarudi kwa mfalme na ripoti nzuri sana ya maendeleo ya koti, pia akaleta taarifa nzuri kuwa kesho yake Abunuwasi angemaliza kazi na angeleta nguo ili mfalme azivae. Kesho yake mapema Abunuwasi akaingia katika kasri la mfalme akiwa kama kashika lundo la nguo, ambazo mwenyewe alisema wasio na dhambi tu ndio wataziona. Wasaidizi wa mfalme wote hawakuwa wanaona kitu lakini walianza kupiga makofi wakisifu jinsi nguo zilivyokuwa nzuri, hamna aliyekuwa anataka kuonekana ana dhambi. Hatimae Abunuwasi akamkabidhi mfalme nguo, mfalme nae hakuwa anaona kitu lakini ili asiambiwe ana dhambi akajidai eti nae anaziona akaanza kumsifu Abunuwasi kwa umahiri wake wa kuchagua rangi na hata ufundi wake mkubwa wa kushona. Abunuwasi akamuomba mfalme azivae zile nguo, wakaingia faragha mfalme akavua nguo zake na akaanza kuvaa nguo asizoziona kwa msaada wa Abunuwasi. Kwa vile alivua nguo zote na kuvalishwa mpya zisizoonekana, rohoni mwake alikuwa anajiona yuko uchi lakini akaona akitangaza haoni kitu wananchi wangemshangaa kuwa mfalme ana dhambi, hivyo akaendelea kusifia na kujiangalia kwenye kioo akisifu nguo zilivyompendeza. Kisha akalazimika kutoka nje ili wananchi waone nguo mpya za mfalme. Wote walikuwa wanamwona mfalme yuko uchi lakini wakawa wanaogopa kuonekana wana dhambi hivyo kila mtu akawa anashangilia na kusifu uzuri wa nguo za mfalme. Lakini ghafla mtoto moja mdogo kwa sauti kubwa akamuuliza baba yake, “Baba mbona mfalme yuko uchi?”. Minong’ono ikaanza mwishowe watu wakaanza kumuunga mkono mtoto, mfalme nae sasa aibu ikamshika kwani alijua sasa watu wote wanamuona yuko uchi, akatimka na kujificha kwenye kasri lake na hadithi yangu imeisha hapo.

15 March 2017

BABA RUDI NYUMBANI UPESI

WhatsApp-logo 
DOGO: (Kampigia simu baba yake) Baba rudi nyumbani upesi  
BABA: Dogo niko bizi nina mkutano na JPM baada ya robo saa  
DOGO: Haya shauri yako mama anasoma mesej zako za whatsapp kwenye simu yako

3 March 2017

MJINI NI SHIDAAA MAMBO SHAGHALA BAGHALA


Juzi niliamua kuzunguka mjini kuangalia vituko vya maendeleo. Yaani we acha tu, ushishangae kuona fenesi zimefungwa kwenye glasi za juis, wala usishangae kuona chandarua kimegeuzwa neti ya kuvulia samaki, mambo yako shaghala baghala. Lakini vituko vikubwa nilivikuta nilipoingia supa maketi. Baada ya kuchunguza kwa makini nikagundua kuna kitu cha ajabu sana kinaendelea, kumbe sio kila anaeingia supamaketi anaingia kununua kitu, watu wana sababu mbalimbali. Aina ya kwanza ya wateja ni wale wanaoingia kujipiga picha, wenyewe wanaziita selfie, yaana hawa wako kibao kila kona unakuta mtu anajipiga picha aonekane alikuwa supamaketi na haraka kuposti watsap na insta. Katika hili wadada ndio wengi zaidi ingawaje na kwa upande wa wakaka, wako wale wanaovalia suruali nusu mlingoti ndio idadi kubwa zaidi. Sasa hawa wakimaliza kujiselfisha mara nyingi hawanunui chochote ila wakijitahidi sana hununua bigi ji au maji madogo.

Halafu hapohapo wako madenti ambao wanapendana, basi hupanga kukutana supamaketi, hawa utawaona wanazunguka tu humo ndani hawatoki, wanajipiga selfi kibao ingawaje hawazipost insta, halafu mwisho hawanunui kitu. Mapenzi ya shule ni sheeeda. Kuna kundi la wateja ambao huingia supamaketi na kununua vitu ambavyo hata kwenye genge mtaani kwao vipo, lakini kwa kuwa supamaketi unapewa  mfuko una jina la supamaketi, hii ni swaga kubwa  mtaani, kila mtu anajua uliingia supamaket. Hawa huishia kununua mkate, au chumvi, wakijitahidi wataongeza na blubendi. Halafu kuna kundi la wamama washua, hawa huingia supamaketi na kikaratasi kimeandikwa kila kitu wanachotaka kununua, bahili hao, utakuta wanatembea na kalkuleta, wanaenda hesabu sambamba na mhudumu, mara nyingi hawa huja na watoto wao wakorofi, wanakimbia kimbia hovyo supamaketi, na ni wazi wanasoma intanesho, maana utasikia wamama hao kila dakika wakiita ‘ Junia, junia kam hia, Juni no stop that’ Wazungu weusi flani hivi. Halafu kuna wale wachunguza bei. Hawa huwa hawanunui chochote kazi yao kuzunguka tu supamaketi wanaangalia bei ya vitu, wanashika shika tu. Mara yuko kwenye sabuni, kahamia kwenye chakula mara aangalie sahani arudi kwenye sabwufa, akitoka hapo anaenda kwenye friza hawachoki hawa anaweza ingia supamaketi tatu kwa siku halafu hanunui kitu. Nitafute instagram @johnkitime nikuhadithie kitu