HATUPIMI BANDO

23 February 2017

BANGI MBAYA USIONJE OHOO


Kutumia dawa za kulevya sio ujanja kabisaaa. Ni mtego ambao ukiingia kutoka sio rahisi. Dawa za kulevya zina haribu kabisa taratibu za maisha, vijana wengi hawataweza tena kufikia kiwango chao cha mafanikio katika maisha kutokana na kuingia katika janga hili, kwani malengo ya maisha hubadilika kukawa na lengo moja tu, nalo ni kupata pesa tu ya kununua dawa nyingine ili kulewa tena na tena. Usikubali kuingia katika mtego wa dawa za kulevya.

Ila vituko vya watumiaji wa dawa za kulevya ni vingi mno. Wakati niko sekondari kuna mwenzetu mmoja alifanya maajabu makubwa. Ilikuwa ni wakati wa mapumziko ya saa nne asubuhi, akawakuta rafiki zake wako chooni wanavuta bangi nae siku hiyo akaona aonje huo moshi. Mwanzo hakuona tofauti yoyote mpaka pale alipoingia darasani. Akiwa kimya anafuatilia masomo mara akahisi kuwa kuna siafu wameingia ndani ya shati lake, akapiga ukelele na kuanza kuvua shati huku akilalamika ‘Siafu siafu’. Darasa zima tukashtuka na kuanza kumuangalia, alipomaliza kuvua shati akilalamika kuhusu siafu ambao sie wengine tulikuwa hatuwaoni ghafla akadai wamehamia kwenye suruali na kuivua suruali, ilichukua muda mfupi wenzie aliovuta nao bangi wakatambua kuwa kuwa ni matokeo ya bangi, si ndipo minong’ono ya bangi ikaanza kuzunguka darasani watu wakaanza kucheka badala ya kumhurumia. Ndugu yetu akatimka nje ya darasa kukimbia siafu aliokuwa akiwaona yeye peke yake. Suruali na shati akiwa kaviacha darasani. Wanafunzi waliokuweko nje wakaanza kumfukuza na hatimae kumkamata, wakati huo akawa kabadili maneno, akawa analalamika kuwa mawingu yanashuka. Akawa na anaangalia juu na kulalamika kuwa mawingu yanashuka yatamgandamiza. Shule nzima ilikuwa imepata habari kuwa mwenzetu kavuta bangi sasa inamletea aluweluwe. Akapelekwa kwa mwalimu mkuu huko akabadilika, akaanza kumkumbatia mwalimu mkuu aliyekuwa mama mtu mzima na kudai ni valentine wake wa siku nyingi. Ilikuwa kazi mwalimu kujaribu kujinasua kwa kijana ambaye alikuwa kavaa bukta tu  aking’ang’ania kuwa anamkumbatia valentie wake. Hatimae akafungwa kamba mikono nyuma japo aliendelea kucheka na kudai mambo mbalimbali mara akijitetea kuwa yeye ni Rambo na ataweza kujifungua mara alalamike kuwa yeye mfungwa wa kisiasa. Ila jambo moja ni kuwa kuanzia siku ile aliapa hataonja tena dawa za kulevya za aina yoyote maishani mwake.

No comments: