HATUPIMI BANDO

26 January 2017

KUNA MADEREVA WANA ROHO MBAYA SANA


Duniani kuna watu wana roho mbaya sana jamani dah. Yaani mtu anakufanyia kitu kibaya unaumia yeye ndio kwanza ananunua soda anakunywa anakuangalia jinsi unavyoteseka. Halafu binadamu tuna kamsemo fulani eti mtu mkatili namna hii ana roho ya kinyama, yaani tunawaonea kabisa wanyama, huwa hawana roho mbaya. Ila binadamu khaaa. Leo niongelee dereva wa basi moja ambae alinifanyia mtima nyongo sitasahau, niliapa sipandi tena mabasi ya kampuni yake. Siku hiyo nimeamka mapema nikawahi basi naelekea mkoani kwenye dili zangu. Safari ikaanza vizuri kama kawaida video za muziki wa Bongofleva zikaanza kuonyeshwa, kausingizi kadogo kakaninipitia. Niliposhtuka tulikuwa tumeenda mbali kidogo kwa mbali nikasikia kama vile nataka kwenda jisaidia, nikaona poa ntasubiri basi litakaposimama nijinafasi. Baada ya masaa mawili hali yangu ikawa sasa ngumu kidogo, nikasimama na kwenda kwa dreva na kumtaarifu hali yangu. Akanijibu kistaarabu, ‘Subiri tunasimama hapo mbele baada ya dakika chache’. Nikarudi kwenye kiti, dakika arobaini na tano baadae hakukuwa na dalili yoyote ya basi kusimama, hali yangu ilikuwa tete sikuwa hata na nguvu za kusimama kumwendea dreva maana nilijua nikisimama tu nitaachia. Nikampigia kelele konda, akanijibu, ‘Jamani si umeambiwa tutasimama muda si mrefu? We mzee vipi?’  Jamani jasho likaanza kunitoka, ningekuwa mtoto mdogo ningeshaachia , nilikuwa nahangaika kwenye kiti vibaya sana, video naiona naisikia lakini hata sijui ilikuwa inaimba wimbo gani. Kila sekunde kwangu ilikuwa mwaka, na gari likijirusha ilikuwa kama vile sasa ndio najiachia. Nikaona heri nitambae mpaka kwa dreva. Nikafika mbele na kumuomba, ‘Baba chonde naumbuka mwenzio’. Alichofanya ni kubadili gia na kunambia subiri kidogo mzee, kuna kituo cha mzani hapo mbele huwa tunasimama, utamaliza mambo yako huko. Nikaona isiwe tabu kama kuumbuka nishaumbuka, nikajiachia palepale mbele ya dreva. Yaani uzito wote ukanitoka nilikuwa kama nimeshusha mzigo wa tani kumi. Konda na dreva wakaanza matusi yao wala sikuwasikiliza, nikawa natabasamu kwa raha, nikarudi kwenye kiti changu suruwali imelowa, abiria nao wengine wanatukana wengine wananihurumia, potelea mbali mradi nimerudi kuwa binadamu huru tena. 

18 January 2017

WANAMUZIKI NA WANASIASA KUMBE NDUGU KABISANilikuwa nimekaa kwenye kijiwe kimoja wanapouza pombe za kikwetu, nashushia plastiki moja baada ya jingine, siku hizi hata hivi vijiwe vyetu hivi vimeboreshwa kuna luninga. Hata sisi sasa tunaona laiv hotuba za wanasiasa na kupata burudani ya kusindikizwa na Bongofleva wakati wa kushushia hii kitu. Ujue ukiwa unakunywa hivi vitu akili inachangamka, unaweza ukaanza kinywaji hujui kiingereza baada ya plastiki tatu kiingereza kinakuwa rahisi kabisa. Au unaanza hujui kabisa kucheza lakini baada ya plastiki kadhaa unakuwa na uwezo wa kucheza show kwenye kundi la Wasafi Classic, hizi ni baadhi ya faida chache za pombe za huku kwetu ambazo Taifa halijazitumia. Sasa hapa akili imechangamka nimegundua kumbe wanamuziki na wanasiasa ndugu kabisaa, tena inawezekana hawa ni pacha. Kwanza kabisa wote wanaishi mjini kwa kutunga mistari. Ila huyu ndugu mmoja huwa anaweka biti kwenye mashahiri yake hivyo anayosema yanautamu unajikuta unacheza wakati unamsikiliza. Ukianza na babu za hawa Bongofleva, utakumbuka wimbo kama Dada Asha wa Tabora Jazz ambapo mwimbaji aliahidi kumnunulia Asha ndege. Wale urafiki Jazz wakawa na wimbo wao eti maisha mjini hayafai wanaenda kijiji cha Ujamaa kulima. Watu wakakubali na kucheza sana mistari hiyo, wakati wanamuziki hao wanapoahidi kumnunulia Asha ndege, hata baiskeli hawana, dah, hawa na walipokuwa wakihimiza watu kwenda kijijini kulima hata jembe walikuwa hawajui linashikwaje. Hao ndio wanamuziki bwana na mpaka leo hawajabadilika ila wameboresha uwongo wao siku hizi unasindikizwa na video, wote wana mabinti wakali, magari ya kifahari nguo za bei mbaya na nyumba za ghorofa, vyote hivyo hawana hahahahaha. Sasa ndugu zao wanasiasa nao wana mistari mikali lakini bila muziki, hawa bwana wanaweza kukwambia nipe kura zako ntakuletea barabara, utaishi maisha kama Ulaya, kila mtu utakuwa na hela mfukoni, magonjwa yatakwisha. Mwenyewe utajikuta unapiga makofi. Na wao siku hizi wameboresha mistari yao, inaonekana mpaka kwenye luninga, ukiingia mkenge uwachague ndio huwaoni tena mpaka baada ya miaka mitano wanapokuja kukupa mistari mingine iliyoboreshwa zaidi. Ngoja niongeze plastiki jingine, nami nijione nina ngumi kama Tyson, nikawashushie kipigo wale vibaka mtaani kwetu.  

14 January 2017

UNAKUMBUKA MAMBO ENZI ZA MITIHANI

Unakumbuka mambo yalivyokuwa siku za mtihani?

1. Katikati ya mtihani unasikia mwanafunzi anaekujaga wa kwanza kila siku anamwambia mwalimu, 'Samahani mwalimu swali la 4 limekosewa' , wakati huo wewe lile swali umeshalijibu lote bila tatizo....

2. Pale unaposikia wanafunzi wenzio wanaomba karatasi za graph, wakati wewe umeshamaliza maswali yote na hukuona popote panahitaji karatasi ya graph........
3. Pale ambapo msimamizi wa mtihani anatangaza. 'Rukeni swali la sita tutalirekibisha', wakati swali hilo wewe ndio uliona rahisi kuliko yote.....
4. Pale unapoona wenzio wote wanatumia rula na wewe huoni mahala popote panapotakiwa rula.....
5. Mkisha maliza mtihani wa hesabu mko nje mnapumzika kungojea kuingia kufanya mtihani wa Jiografia, wenye akili wanabishana, 'Jibu pale lilikuwa asilimia 38 mwingine anasema hapana ni asilimia 38.5, wakati wewe jibu ulipata 4500.....

12 January 2017

WASHKAJI MNABOA JIREKBISHENI 2017


Oya washkaji naona sasa niongee lugha mtakayonielewa, mwaka huu lazima tubadilike au vipi? Kuna watu wanaboa mpaka basi  sasa nimeona niwaibukie humu mnielewe. Nianze na washkaji wa Ubungo kituo cha mabasi yaendayo mikoani, aise hivi nani aliwaambia mradi mtu anapita karibu na hicho kituo basi lazima anataelekea Moshi Arusha Mwanza Iringa au  Njombe? Yaani kila siku napita hapo naelekea home Ubungo hamchoki kunisumbua eti niende kwenye miji hiyo nasema nimechoka mnaboa, anaesafiri si ataingia ndani kuafuta tiketi?  Kwanza kuingia kiyuoni nako ni shida tupu, mmeweka milango ya chuma ya kuzunguka, mtu ukija na tenga lako kubwa hamruhusu apite geti kubwa eti lazima apite kwenye kamalango hako kakuzunguka ambako hakatoshi kupitisha tenga, mnataka afanye miujiza, au yote hii kusudi watu wakodi vitorori  vyenu ambavyo mnaviruhusu kupita kwenye geti kubwa mnaboa sana mjue. Mtu achukue mzigo wangu halafu apite geti ambalo mi siruhusiwi kupita tukipotezana si ndio mzigo wangu umekwenda na maji? Mnajua mnaboa  aise. Halafu mtindo wa kuuza tiketi yuzd pale mlangoni wakati wa kuingia acheni mwaka huu, ntakuja lianzisha pale tutaishia kugawana majengo ya serikali mmoja magereza mwingine hospitali ohoo. Halafu kamtindo kanyie makonda kuruhusu watu kuja kuhubiri bidhaa zao kwenye mabasi acheni mwaka huu, mtu umeamka kwenye saa tisa usiku uwahi basi la saa kumi na mbili asubuhi ile unajinyoosha kupunguza usingizi unasikia, “Samahani ndugu abilia Je, unachunusi au unanuka kikwapa? Je, soksi zinanuka? Usikonde tunakuletea dawa ya kunywa ya Anko K inasaidia sana, hata mimi nilikuwa nanuka kikwapa siku hizi sinuki kabisa kwa ajili ya bidhaa hizi” Aise mnaboa sana mjue.
Halafu hivi nyie machinga wa Kibaha mabasi yamewakosea nini? Basi likiingia kituoni Kibaha lazima kila machinga aligonge kwa ngumi, yaani sijui ndio masharti ya waganga wenu kuwa mkitaka kuuza basi basi likiingia kituoni pigeni ngumi, yaani kama ndio umetoka Dar na umeshaanza kupata kausingizi, unaweza kukurupuka ukadhani labda basi linapata ajali.
Mjue mnaboa sana  kwa kweli

7 January 2017

2017 SITAKI TENA SIMU ZA KUPANGUSA


Haya tumshukuru Mungu 2017 ndiyo hiyo tumevuka. Tunanza na mikakati ya kuishi vema 2017. Mimi nina mipango mikakati kibao, ngoja niwamegeeni michache labda itawasaidia. Mkakati wa kwanza nikubadilisha taratibu zangu za mawasiliano. Wakuu natangaza kuwa hamtaniona tena whatsapp, wala insta wala facebook. Ile simu yangu ya kufuta nauza tena nauza bei rahisii. Nimegundua ile simu ina jinni la kumaliza pesa, jinni la kumaliza muda, na wote hao wakishirikiana na jinni mahaba. Yaani kuna jini mle linakulazimisha uwe na vocha muda wote masaa 24, yaani linakufanya hata ukiumwa badala ya kwenda kununua dawa we unaenda kununua vocha ili tu uposti kwenye whatsapp na facebook kuwa unaumwa, sasa akili gani hiyo. Yaani ukiamka bila credit kwenye simu unakuwa kama mgonjwa, unahangaika kutafuta pesa hata ikiwezekana ujidhalilishe uombe watu wengine wakuunganishe. Jini baya sana lile. Hili jini la kumaliza muda linahakikisha akili yako yote imekaa inangojea meseji za whatsapp, usiku na mchana, kabla hujalala lazima ucheki nani katuma ujumbe, na kama ukikuta grup lina stori unaweza ukajikuta uko macho saa tisa za usiku unajibishana na mtu yuko Marekani ambako mwenzio kule mchana jua linawaka. Hata kama unaendesha gari hili jinni linakulazimisha uwe unachat, yaani badala ya kuwaza mambo ya kutafuta pesa unahangaika shingo umekunja, unachat na watu kumi kwa mpigo. Huku insta lazima ucheki kama kuna mtu kamtukana supasta wako ili timu yenu mmchangie kumpasha, sasa jambo la ujinga ni kuwa supasta mnaemtetea wala hawajui wala hana taimu na nyinyi sasa si bangi hizi? Halafu kuna hili jinni mahaba, hili linakurahisishia kupata wapenzi wengi kwenye simu halafu wote kazi yao ni kukuomba uwaunganishe muda wa maongezi, hebu fikiria mtu una wapenzi kumi kila mmoja anaomba muda wa maongezi, si kutiana umasikini huku? Unamuandikia mmoja  I miss you halafu una kopi na kupesti kuwatumia wote tisa kila nusu unakazi hiyo, hapana imetosha nauza hii simu ya kupangusa, naanza 2017 na ka nokia tochi hata kama yuzdi tu, mradi niwe huru na hawa majini.