PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

KUMBE MTEJA NI HUYU?


Aise yaani huwezi amini ni kizungumkuti. Lakini swali kubwa ni hela kashika nani? Maana kila mtu anasema hana hela sasa zimekwenda wapi? Juu ya hapo unasikia na benki nazo zinalalamika kuwa biashara mbaya, sasa hela ziko wapi? Au wenye hela  wamezificha uvunguni mwa vitanda badala ya kuzipeleka benki?  Yaani sielewi. Juzi baba mwenye nyumba kanifwata asubuhi kabla hata hakujakucha akanambia hataki maneno mengi anataka kodi yake. Akili  ikawa inanizunguka, mfukoni senti tano sina. Nilikuwa na kativi kangu chogo nikaona nikaona bora nitafute mteja nikauze ili nipate japo hela ya kumpunguza makali ya baba mwenye nyumba.  Katika kutafuta wateja fundi tivi mtaani kwangu akanambia kuna mteja alikuja kuulizia tivii ya bei rahisi hivyo kama ninayo yeye anaweza kuiuza chapchap. Nikabeba mgongoni mali na kuipeleka kwa fundi, kisha nikaelekea kuendelea na shughuli zangu. Kila dakika kumi nilikuwa nambip fundi kujua nini kinaendelea. Hatimaye fundi akanambia biashara inaonekana imetiki, mteja kaipenda mali yangu, kaahidi kuja kuichukua. Nilijisikia mzigo mzito ukishuka kutoka mabegani kwangu, maana ningemlipa baba mwenye nyumba japo kidogo, ningepata nafuu ya miezi kama mitatu hivi nijipange upya. Niliporudi nyumbani nikamkuta baba mwenye nyumba ananisubiri, kakunja uso akionyesha hataki utani. Bila kupoteza muda akanambia anataka hela yake leo leo. Nikatumia kila lugha kumtarifu kuwa kuwa dili nafanya na kesho yake ningelipwa. Baada ya matusi ya kutosha akaondoka na kunambia kesho yake anarudi acute pesa. Nikampigia fundi kuulizia kuhusu mteja, fundi akanambia mteja akasema kuna mahala atalipwa hivyo atachukua mzigo kesho yake. Mapema asubuhi nikatumiwa mesej na baba mwenye nyumba, kuwa nitimize ahadi au patawaka moto. Nami nikamtumia fundi ujumbe ajaribu kumkumbusha mteja ili alipe mapema. Kufikia mchana ngoma ikawa palepale, mali yangu haijalipiwa na mteja aalikuwa kasema anasubiri pesa. Wakati nawaza ntafanyaje mteja asipolipa, fundi akanipigia simu niende kwake nikutane na mteja uso kwa uso tukubaliane. Nikaenda haraka kwa fundi huku nasali kimoyomoyo kuwa mteja alipe japo kitu cha kumuonyesha baba mwenye nyumba. Nilipofika kwa fundi si nikamkuta baba mwenye nyumba kumbe ndie mteja wa tivi yangu. Nilijisikia miguu ikiishiwa nguvu  

Comments