HATUPIMI BANDO

29 November 2016

JAMANI WACHAWI WAPO MTAANI KWETU


Wachawi bado wapo bize sana kama hujui. Halafu wachawi bwana watu wana roho mbaya sana, ishu zao huwashughulikia watu wao wa karibu tu. Ukiwa mnatoka kijiji kimoja, au mtaa mmoja au nyumba moja, au nduguyo au rafiki yako, kati ya hao ndo atatoka atakae kuloga. Kama hakujui mchawi hana shida na wewe. Unajua wachawi wana mbinu mbaya sana kwa mfano umepiga dili limetiki una tumilioni kadhaa, au umepokea fedha zako za mafao ya kustaafu, au singo yako imehit, unapitapita kwa nduguzo au marafiki kuulizia ufanye mradi gani, basi mmoja wapo kama mchawi atakupa wazo, kwa mdomo au kimawazo, ohh fungua genge au fungua kigrosari, nunua gari au kalime. Basi utaona bonge la wazo, mihela yako yote unaingiza kwenye mradi. Kama genge ndio utaona watu wanalikwepa tu, mpaka mtaji unakuishia hivihivi laiv, kama ulifungua kigrosary utajikuta au wewe mwenyewe unageuka mlevi unajikopesha hizo pombe na kununulia wateja wako mpaka kamradi kana buma, kama umenunua kagari, siku mbili tu kamepigwa mzinga, ukijidai kulima basi mwaka huo ndio bei ya ulicholima kinashuka bei ghafla unaambulia patupu, hapo ujue kuna mkono wa mtu. Jana na mimi yamenikuta nimelogwa hivihivi najiona. Niliamka nikiwa na alfu tu, njaa inauma, nikangia kwa mama ntilie nipate japo kikombe cha chai cha mia, maandazi mawili ya mia na bakuli la maharage la mia tatu. Hapo nikajua nabakiwa na mia tano, itatosha nauli ya daladala kwenda kariakoo nikabahatishe chochote.  Mama ntilie akaniletea oda yangu nikaanza kula taratibu, hee kutizama chini hivi si nikaona mtu kadondosha noti ya alfu, basi kwa ustadi mkubwa nikaivuta kwa mguu bila mtu yoyote kunishtukia kisha nikaikanyaga vizuri. Roho yangu ikawa sasa na amani, nilipomaliza raundi ya kwanza nikaagiza tena chai nyingine, maandazi na maharage. Wakati wa kulipa nikainama na kuchukua ile alfu na kumpa mama ntilie tukaagana kwa furaha tumbo limejaa safii. Nikakimbilia daladala la Kariakoo nikakaa tena kwenye dirisha nipate upepo. Mchezo ukanigeukia konda alipotaka nauli, nilijisachi mwili mzima siioni alfu yangu, machozi yalinilengalenga nilijua konda hatanielewa. Na hapo ndipo akili ikanijia kuwa ile alfu nilidhani kadondosha mtu mwingine nilikuwa nimedondosha mimi mwenyewe. Nikagundua mara moja lazima kuna mchawi kaniroga, na nina shaka na kale kazee mtaani kwetu nilikokaambia siji kukaamkia dahh kweli uchawi upo

23 November 2016

NYIE WANA IJI YA KENYA KISWAHILI YENU APANA MUSURI

SASA kama mvua iko naendelea kunya, wana inchi kwanini wakue macho, si wazibe pua harufu itatoka ile kali? Nataka toa advice mukuje Tanzania mpaka iache kunya.

KUMBE MTEJA NI HUYU?


Aise yaani huwezi amini ni kizungumkuti. Lakini swali kubwa ni hela kashika nani? Maana kila mtu anasema hana hela sasa zimekwenda wapi? Juu ya hapo unasikia na benki nazo zinalalamika kuwa biashara mbaya, sasa hela ziko wapi? Au wenye hela  wamezificha uvunguni mwa vitanda badala ya kuzipeleka benki?  Yaani sielewi. Juzi baba mwenye nyumba kanifwata asubuhi kabla hata hakujakucha akanambia hataki maneno mengi anataka kodi yake. Akili  ikawa inanizunguka, mfukoni senti tano sina. Nilikuwa na kativi kangu chogo nikaona nikaona bora nitafute mteja nikauze ili nipate japo hela ya kumpunguza makali ya baba mwenye nyumba.  Katika kutafuta wateja fundi tivi mtaani kwangu akanambia kuna mteja alikuja kuulizia tivii ya bei rahisi hivyo kama ninayo yeye anaweza kuiuza chapchap. Nikabeba mgongoni mali na kuipeleka kwa fundi, kisha nikaelekea kuendelea na shughuli zangu. Kila dakika kumi nilikuwa nambip fundi kujua nini kinaendelea. Hatimaye fundi akanambia biashara inaonekana imetiki, mteja kaipenda mali yangu, kaahidi kuja kuichukua. Nilijisikia mzigo mzito ukishuka kutoka mabegani kwangu, maana ningemlipa baba mwenye nyumba japo kidogo, ningepata nafuu ya miezi kama mitatu hivi nijipange upya. Niliporudi nyumbani nikamkuta baba mwenye nyumba ananisubiri, kakunja uso akionyesha hataki utani. Bila kupoteza muda akanambia anataka hela yake leo leo. Nikatumia kila lugha kumtarifu kuwa kuwa dili nafanya na kesho yake ningelipwa. Baada ya matusi ya kutosha akaondoka na kunambia kesho yake anarudi acute pesa. Nikampigia fundi kuulizia kuhusu mteja, fundi akanambia mteja akasema kuna mahala atalipwa hivyo atachukua mzigo kesho yake. Mapema asubuhi nikatumiwa mesej na baba mwenye nyumba, kuwa nitimize ahadi au patawaka moto. Nami nikamtumia fundi ujumbe ajaribu kumkumbusha mteja ili alipe mapema. Kufikia mchana ngoma ikawa palepale, mali yangu haijalipiwa na mteja aalikuwa kasema anasubiri pesa. Wakati nawaza ntafanyaje mteja asipolipa, fundi akanipigia simu niende kwake nikutane na mteja uso kwa uso tukubaliane. Nikaenda haraka kwa fundi huku nasali kimoyomoyo kuwa mteja alipe japo kitu cha kumuonyesha baba mwenye nyumba. Nilipofika kwa fundi si nikamkuta baba mwenye nyumba kumbe ndie mteja wa tivi yangu. Nilijisikia miguu ikiishiwa nguvu  

HIZI FIKSI ZA WANAIJERIA ZINAFIKIA PABAYASASA WAANZISHA CHUO CHA UNABII


16 November 2016

TILAMBU HOYEEEE


Haya tena kumekucha wengine wanasherehekea, wengine wanalia Trump ndio kishakuwa Rais wa Marekani. Huwezi kuamini kule kijijini kwetu kuna sherehe kubwa sana. Wanakijiji wanasherehekea Trump kuwa Rais. Najua utashangaa, hata mimi mwanzo nilishangaa, lakini ngoja nikupe mkasa mzima ujue sababu ya watu kucheza ngoma kusherehekea ushindi wa Trump. Nilikuwa nimeshachoshwa na kelele za mjini nikaona nirudi kijijini kama wiki hivi nikapumzishe akili. Kijiji chetu kiko kama kilomita 15 toka barabara ya lami hivyo ukishuka kwenye basi unaweza aidha kukanyaga kwa miguu au kupanda bodaboda. Nikachukua bodaboda, japo hunikuti nikipanda hiyo kitu hapa mjini, bodaboda za mjini zinatisha bwana, hawa jamaa udereva wao una uchizi ndani yake. Basi ile kukaribia kijijini tu nikaanza kusikia ngoma, baadae nikaanza kuona nyumba zimepambwa, niliposhuka kwetu namuona mjomba wangu mmoja yuko tilatila akanikaribisha, ‘Wamjini kalibu ufulahie maisha’.  Nikamsalimu na ndugu zangu wengine wote walionekana kuwa na furaha kubwa. Ndipo nikauliza kulikoni furaha zote au walikuwa wanajua nitakuja? Shangazi yangu moja akajitokeza na kupiga kigelegele cha nguvu na kusherehekea, ‘Tlambu Tlambu Tlambu hoyee’ Sasa wakanichanganya, Trump na kijiji chetu wapi na wapi? Waswahili dunia nzima wanahofu na ujio wa Trump hapa kwetu watu wanasherehekea, kuna nini?. ‘Shangazi Trump kafanya nini?’ shangazi akaniambia kikwetu ‘Hujasikia? Tlambu kashinda uchaguzi’. Nikamwambia nimesikia ila sijui kwanini wanafurahia. Shangazi akanikaribisha kwenye kiti akanambia,’Unamkumbuka yule binamu yako aliendaga Ulaya zamani?’ Nikamwambia ndio, kwani nani pale kijijini hamkumbuki yule mjinga, aliondoka zamani, kuna siku alirudi ila alifanya vituko vya mwaka, kwanza alijidai kasahau kikwetu , hata Kiswahili alikuwa anapata shida kuongea, pili alikashifu sana kijiji, na wanakijiji kuwa wachafu hawana maendeleo, na aligoma hata kuingia kwao akisema anaweza kupata maambukizi. Alipoondoka aliaacha simulizi ya muda mrefu kijijini. Nikamuuliza shangazi ‘Sasa kafanyaje yule kichaa?’ Shangazi akanambia, ‘Si unajua Tlambu kasema anawafukuza wageni wote Marekani? Basi binamu yako kanipigia simu juzi, anataka kurudi anaomba nimkatie kasehemu ka shamba tena kaongea kilugha vizuri. Sasa hapa tunamsubiri tuone ataingilia mlango gani hapa nyumbani Tlambu oyeee’,

15 November 2016

SWAGA ZILIKUWA ZAMANI BWANA. SIKU HIZI MHHHHHH


Mandeleo yameua swaga nakwambia. Watu siku hizi wanajidaiii eti wana swaaga, aa wapi!! swaga zilikuwa zamani bwana. Enzi hizo za redio moja, mtu ukitoka kijijini na kuweza kuja kukaa mjini hata wiki moja tu, ukirudi unajikuta wewe ndie mjanja wa kijijini, na kama ulibahatika kuja jiji la Dar es Salaam, basi watu wote wanakusikiliza wewe unavyowahadithia jinsi ulivyopanda basi la ghorofa, au hata ulivyoibiwa mara baada ya kushuka kituo cha basi, na kila anaetaka kusafiri anakutafuta kukuomba ushauri jinsi ya kujilinda na wezi Dar es salaam.
Swaga zilikuwa enzi hizo ambapo mtu unakuwa ndie mwanafunzi pekee aliyevaa viatu shule nzima, walimu wenyewe wanakuogopa maana lazima wazazi wako wana uwezo mkubwa. Hizo ndio zilikuwa swaga bwana. Kila asubuhi kulikuwa na ukaguzi wa wanafunzi, mwalimu anakagua kucha, meno na lazima kila mtu aonyeshe mswaki wake, swaga ni pale wanafunzi watatu tu shule nzima ndio mna miswaki ya plastiki wengine wote wana miswaki ya miti, hapo utakuta mwalimu mkuu anawatoa mbele na kuonyesha miswaki yenu kwa wengine kama mfano na kuwambia shule nzima, “What is this? This is a toothbrush, haya semeni wote toothbrush” , acha bwana.
Enzi ya Mwalimu hali ilikuwa ngumu , mtu ukiwa na ndugu yako yuko nje, tulikuita Mamtoni, akakuletea suruali ya jeans basi wewe unaweza kuoa chaguo lako, na mji wote wanakutambua kuwa una jeans, enzi hizo kinaitwa ‘kigozi’. Ukiwa na raba zilizoitwa ‘rabamtoni’, au baadae ‘za kuchumpa’ mtaa mzima wanazijua hizo raba sio siku hizi kila nyumba watu wana raba, hakuna swaga bwana siku hizi swaga zamani ndugu yangu.
Watu wengine hawajui kulikuwa na wakati kuwa na TV ilikuwa uhujumu uchumi, hivyo kuwa na TV ilikuwa boooonge ya swaga, japo kulikuwa hakuna kituo cha TV cha kurusha matangazo, TV ilikuwa inaenda na video kaseti, basi kwenu mkiwa na TV, washamba washamba wote wa mtaa unawakaribisha washangae wakati unatafuta mita, TV za siku hizo zilikuwa hazina rimoti, hivyo kuna kigudumu unazungusha hicho hata nusu saa ndipo unaanza kupata picha au sauti , lazima uzungushe mpaka sauti na picha zitokee pamoja, washamba lazima wabaki wanakodoa macho kukuangalia unapofanya maufundi hayo, na baadae kwenda kuhadithiana kwao..
Swaga ilikuwa pale kwenu tu ndio kuna simu mtaa mzima, watu wanakuja kubembeleza simu zao zifikie kwenu na wanalipa wakitaka kupiga kwa ndugu zao, watu walikuwa wakipiga magoti wakati wanaongea na wakubwa zao kwenye simu, na watu wote wanajua mna simu maana waya ya simu ilikuwa ikionekana inaingia kwenu.
Swaga zamani bwana, baba yako akinunua VW hata kama mko watoto wanane na mama yenu na hauzgelo juu mnajazana kwenye kivokswagen kwa starehe kabisa na mzee anazunguka mitaa yote mjini washamba wanawaangalia.
Hizo ndo swaga bwana.
Nakumbuka swaga za mwalimu wangu wa hesabu aliyekuwa anavaa kaptura nyeupe shati jeupe, saspenda nyeusi zimeshikilia kaptura, soksi ndefu zimefika chini ya magoti, viatu vya ngozi vyekundu. Kwenye soksi alikuwa anachomeka kiko na peni aina ya BIC mbili . Kwenye mfuko wa shati peni tatu, mkono wa kushoto ana leso nyeupe, mkono wa kulia ameshika kiboko.
Swaga zilikuwa zamani bwana

USHAURI WA BURE USIVUTE BANGI SIKU YA HARUSI YAKO PART 1


14 November 2016

MTANI WACH HAYO MAMB MTANI

Mtani wangu sasa ndo umefanya nini? Mtani wangu babake nanilii yule modo maarufu, kafungua akaunti benki akaweka hela zake bila shida,  ile kutoka nje kakuta watu wamepanga foleni wanatoa hela kwenye ATM, nae akapanga mstari zamu yake ilipofika akatoa mkwanja wake wote kisha akarudi beki na kuomba wamuwekee vizuri maana kakuta watu nje wanatoa hela bila mpango wasije wakatoa na zake

JIRANI YANGU SIO MTU WA MCHEZOMCHEZO


Mdada mmoja jirani yangu , alikuwa kila siku ananilalamikia kuwa kuna rafiki yake hataki kulipa deni la nguo na viatu alivyochukua siku nyingi, jambo ambalo limeua mtaji wa biashara yake, mbali zaidi amekuwa hata simu zake hapokei. Kwa siku anampigia hata mara kumi lakini hapokei na kila akienda kwake hamkuti. Kwa kweli nilikuwa namuonea huruma na pia nilikuwa naumia mimi maana yake alikuwa anakuja geto kila asubuhi mara aombe sukari, mara chumvi mara nauli, vocha ndio usiseme. Leo asubuhi kanigongea, nikaamka nikijua napigwa mzinga mwingine asubuhisubuhi, badala ya masikitiko akanipa bahasha ndani nikakuta alfu hamsini, wakati nashangaa  akasema ‘Zako hizo na pole kwa kukusumbua kwa muda mrefu’. Nikamuuliza za nini? Akanijibu aliyekuwa anamdai kamlipa, hivyo ameona ni haki nipate japo kidogo. Nikashukuru, na ndio nikamuuliza kwani kimetokea nini mpaka akalipwa? Hapo ndipo aliponipa stori nzima. Baada ya kuona simu hazipokelewi basi akamtumia mdeni wake ujumbe wa maneno ufuatao. ‘ Shosti  sikupigii kwa ajili na kukudai nilikuwa nakwambia tu kuwa kuna mabinti wawili walikuwa wanamgombea mumeo, wametandikana sana, mumeo alikuwa pembeni anaangalia tu. Mmoja akapigwa akakimbia basi mumeo akaondoka na yule mshindi kamkumbatia kiunoni’. Haikuchukua hata dakika tano mdeni wake akampigia, hakupokea. Katika nusu saa zilipigwa  missed call kama 30. Baadae mdeni akaanza kutuma meseji, ‘Ugomvi ulikuwa wapi?’ ‘Walielekea wapi na mume wangu?’, ‘Mwanamke mwenyewe unamjua?” , ‘Shosti tafadhali nambie kumbuka urafiki wetu shosti’. Baada ya hapo zikaanza missed call tena, ambazo hazikupokelewa. Ndipo ikaja mesej  tamu,’Hela zako ninazo tukutane wapi nikupe unielezee mkasa mzima?’ Hapo ndipo jirani akajibu. ‘Shosti nitumie kusudi nipatie na usafiri nije nikupeleke walipoenda, kiukweli alichofanya shemeji ni cha aibu, twende tukamkomeshe’. Hazikupita sekunde chache deni likalipwa na hela za usafiri juu. Hapo ndipo jirani yangu akaenda kwa wakala akatoa fedha zake kisha akazima simu na kuendelea na shughuli zake kwa raha zake. Jirani yangu si mtu wa mchezo mchezo

10 November 2016

KWA WALE WATAKAOFUKUZWA NA TRUMP KARIBUNI NYUMBANIChungu ndio hicho kiko jikoni mambo yamekaribia kuiva, Trump ndo keshakuwa Rais wa marekani. Nimeona nitoe wosia kwa ndugu zangu Wabongo-Wamarekani, nadhani kipindi hiki wanahitaji ushauri nasaha. Kwanza hongereni kwa uchaguzi safi wa kidemokrezia, Kibongobongo lazima kupeana hongera kwa kila kitu hata ukimaliza msiba utaambiwa ‘Hongera kwa kumaliza msiba salama’. Hili muanze kulizoea maana najua muda si mrefu mtalazimika kurudi nyumbani. Nyumbani ni nyumbani. Kutokana na maelezo ya Rais wenu shughuli ya kurudi itaanza karibuni nimeona nichukue nafasi hii kuwatayarisha na hali ya huku. Kwanza huku umeme sehemu nyingine unazingua, tafadhali njoo na power bank, usitegemee kununua za huku, utakasirika maana powerbank za huku majanga matupu unaweza kununua ikafanya kazi au ikafa baada ya siku mbili, au ukauziwa ‘kanyaboya’ kabisaa. Neno kanyaboya maana yake utauziwa ndichosicho. Kifupi njoo na pawabenki yako. Pia nashauri chaji kabisa simu huko halafu uje huku maana inawezekana ukalazimika kufikia kijijini kwenu ambako umeme hauko kabisaa, wanakijiji wanategemea kuchaji kijiji jirani kwenye duka lenye jenereta.  Weka pesa pembeni ya kununua ‘airtime’ huku hakuna WIFI za bure, ukifika kuna kampuni kibao za line za simu zinatoa huduma ya intanet lakini kuna nyingine bomu kishenzi, watakuambia lipa elfu utapata internet siku nzima kumbe wao siku yao ni masaa matatu tu. Uliza kwanza wenyeji wakuambie. Usafiri wa haraka na gharama ndogo huku ni bodaboda, kutokana na ubahili mliojifunza huko, huo ndio usafiri mtakao ona unawafaa lakini tegemeeni kuvunjika miguu sana mapema kama mtang’ang’ania usafiri huo. Kwa watoto ambao mtalazimika kurudi huku na wazazi wenu, eleweni kuwa  huku mzazi wako akikupiga hakuna kesi, labda akuuwe, hivyo mkija huku hakikisheni mna adabu, ukimjibu hovyo mzazi wako ruksa jirani kuingilia kesi na kukupa mkong’oto na umma utamuunga mkono. Hakuna kazi huku, hata kama una digrii na kiingereza cha kimarekani haisadii men, tena afadhali zamani babako kama anamjua mtu anaemjua mwanasiasa mjumbe wa bodi fulani ungepata kazi, siku hizi huku yuko mtu anaitwa JPM mchezo huo hakuna. Kwa mayanki mnaojifanya mahendsam, Mademu wa hapa huwa hawachangii kulipa ukimtoa out, hapo ujue bili zote zako hata kama ana hela kuliko wewe, hivyo ukija kichwakichwa aukijua demu atajitegemea wakati wewe ndio umemwambia muende mkale chakula cha jioni au muende klabu, utalia, tena wana kamtindo kakusema 'anakuja na mwenzie kusudi awe na kamapani'. Wadada mkija huku sio unavaa kila nguo kila mahala, ukienda sokoni na kimini usishangae wakati ukaanza kushangiliwa kama supasta,utafanyiwa mambo mazito hadharani, ukienda polisi kushtaki kuwa unanyanyaswa utafunguliwa mashtaka kwa kutembea utupu shauri yako usiseme sikukuambia. Ishu za kukumbatiana hadharani kuonyesha mnapendana acheni hukohuko, mtapigwa mawe huku.
Na kama ulikuwa huwasiliani na nduguzo ishu yako itakuwa ngumu kidogo, maana watu wataabaki wanakuangalia tu unapoharibikiwa wakucheke. 
Karibuni sana

2 November 2016

PITIA KURASA HIZI UFURAHI ZAIDI

PITIA KURASA HIZI
www.johnkitime.co.tz
www.theiringa.blogspot.com .......hasa kama uliwahi kuishi Iringa au unaishi Iringa
https://laughtz.blogspot.com/  ....blog ya vichekesho na habari katika lugha ya Kiingereza

1 November 2016

BABA SAMAHANI ILE HELA YA ADA NIMETUMIA KUBETI


Dogo kampigia simu baba yake;

DOGO: Baba katika zile shilingi laki mbili ulizonipa nikalipe ada nimetumia shilingi alfu 30 kubeti

BABA: Unasema nini we mpumbavu mshenzi mkubwa? Nimekukanya mara ngapi kuhusu kubeti?

DOGO: Lakini baba

BABA: Lakini baba nini ngoja urudi utaona ntakachofanya.

DOGO: Nilitaka kukwambia kuwa nimeshinda shilingi milioni 3

BABA: Ndio hayo ninayosema wewe mpumbavu sana kwanini hukutumia laki nzima kubeti? Si ungepata pesa nyingi zaidi? Ngoja urudi niwataarifu ndugu zako kuhusu uulivyo na akili za kuamua haraka mwanangu mpenzi...

pitia www.johnkitime.co.tz