NDEGE MPYA NDIO ZISHAFIKA


HAYA tena ndege mpya hizo, hatimae tutaweza kusafiri kwenda makwetu kwa kutumia ndege, makofi tafadhali. Mambo si ndiyo haya, siku ya uzinduzi na mimi nilikwenda eapot, nizione zile ndege zetu kwa macho yangu, ujue nimechangia kununua zile ndege, si unajua zimenunuliwa na kodi za wananchi na mimi ni mwananchi. Kimsingi ilitakiwa jina langu nalo liandikwe kwenye kadi ya ndege, ya kuonyesha mwenye mali lakini nimeikabidhi serikali kodi yangu hivyo nimeiruhusu serikali iandike jina lake kwa kipindi cha mpito.  Siku Mkuu wa Kaya anazindua ndege, nilikuwa mmoja wapo wa wananchi ambao tulipanga foleni kuingia ndani ya ndege na kukagua kama kodi yetu imenunua kitu sahihi, nashukuru kila kitu kipya, viti vyake raha full kunesa. Kwa sasa nangojea ratiba itoke nijue ndege zitakuwa zinaenda wapi, hapo ndipo ntatafuta safari. Lazima nipande ndege mwaka huu. Nina rafiki zangu Mwanza, Njombe, Singida, Ntwara, Thame, Arusha Chini, kote lazima niende na ndege. Ila kuna kitu muhimu niwataarifu, ndege sio kama mabasi haya ya kwenda mikoani, ndege kitu kingine bwana , ndege kitu cha heshima, wakati unapanda ndege mtu lazima ujitayarishe kisaikolojia na pia kuwataarifu ndugu na jamaa na mtaani wajue ishu hiyo. Ngoja nikupe mfano, ukiwa unapanda daladala za kwenda kule kwa wale jamaa ambao huwa wanaingilia madirishani, utakuta kuanzia konda kavaa hovyo, dereva kavaa hovyo, basi halijaoshwa mwezi wa pili sasa, viti vibovu, hivyo msafiri na wewe ukiwa hovyohovyo poa tu. Halafu kuna mabasi siku hizi unanunua tiketi mapema, ukiingia kuna konda wa kike msafi, dereva kavaa tai, basi safi hivyo na wewe unajipanga usije kuchafua basi la watu. Sasa ndege ni kitu kingine, kila kitu kisafi mara kumi, wahudumu warembo, mapailoti mahendsam, unaweza ukapata bahati ya kuoa au kuolewa kutokana na safari moja tu ya ndege, sio mchezo. Hivyo basi siku chache kabla ya kupanda ndege lazima kuanza matayarisho. Unafanya shopping ya ukweli viatu vipya, pafyumu kali, sanduku jipya la magurudumu, kimsingi kila kitu kipya cha kupandia ndege mpya. Suti kali kwa wanaume, akina mama saluni ni muhimu, unaingia kwenye ndege unapendeza, ila onyo tafadhali madera sio fresh kwenye ndege mpya. 

No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.