HATUPIMI BANDO

22 September 2016

MTOTO WA KITANGA AMENIVUNJA MGUU


Mikasa mingine huwa ukisimuliwa unacheka badala ya kumuonea huruma aliyekumbwa na mkasa huo. Jamaa yangu mmoja huko Tanga juzi alivunjika mguu akakimbizwa hospitali na wasamaria wema. Akapokelewa vizuri, daktaria akamuuliza jamaa yangu kimetokea nini mpaka akavunjika mguu. Kwa mshangao wa daktari jamaa akaanza, ‘Dokta mkasa huu ulianza miaka kumi iliyopita’ Dokta akashangaa, akamwambia  jamaa yangu sitaki kujua yaliyopita nataka kujua imekuwaje ukavunjika mguu?’ Jamaa yangu akasisitiza ‘ Dokta nisikilize kwanza nikuhadithie mkasa mzima sasa. Miaka kumi iliyopita nilikuwa nafanya kazi ya upishi kwa bosi moja kule Ngamiani. Yule mzee alikuwa na watoto watatu mmoja msichana. Huyu binti alikuwa mzuri sana, vijana wote mtaani walikuwa wakijaribu kupata nafasi katika roho yake lakini haikuwa rahisi kwa kuwa alikuwa akichungwa sana na baba yake na kaka zake. Mimi sikuwa na tatizo lolote maana tulikuwa tukishinda nae pale nyumbani masaa mengi, akinisaidia katika shughuli mbalimbali za mapishi jikoni. Kila mara jioni alikuwa anakuja chumbani kwangu tunaongea mengi, na kila mara kabla hajatoka chumbani kwangu alikuwa akiniuliza kama nahitaji kitu chochote, nilikuwa namjibu sikuwa nahitaji kitu. Na kila baada ya jibu hili, alikuwa akicheka sana na kuondoka zake. Kwa kweli nilikuwa nina uhuru wa mkubwa ndani ya nyumba ile, na mshahara wangu ulikuwa mzuri sana, hivyo sikuona kama kuna kitu zaidi nilikuwa nahitaji. Na hili liliendelea miezi mingi. Nikiri kwa kweli nilikuwa na mimi nampenda sana binti huyu wa Kitanga, lakini nilikuwa naogopa kumtamkia hili, tuliendelea kuishi hivi mpaka siku baba yake alipompeleka nje ya nchi kusoma, roho iliuma sana kumkosa. Sasa dokta leo nilikuwa nimekwea mnazi nikiwa juu si ndio kumbukumbu ikanijia kuhusu yule binti, na lile swali alilokuwa akiniuliza kila alipomaliza mazungumzo  ndipo akili iliponijia kuwa lile swali kumbe mimi nilikuwa mjinga sikuwa nimemuelewa binti yule miaka ile, alichokuwa anataka kunipa kumbe ndicho nilikuwa nakiota siku zote, kwa bahati mbaya nikajisahau na kuachia mikono na kuanguka na kuvunjika mguu’.

No comments: