HATUPIMI BANDO

6 July 2016

NINAFIKIRIA KURUDI SHAMBA


Hahahahaha yaani kila siku Bongo kuna kichekesho kipya, mi nashangaa unamkuta mtu kanuna siku nzima anapata mastresi na pengine kupata vidonda vya tumbo na presha wakati mambo ya kuondoa presha yamejaa kila kona. Hebu angalia kwa mfano jinsi Wabongo walivyo mabingwa wa visingizio, kila jambo likikwama kuna bonge ya kisingizio. Kwa mfano ukishamlipa mganga wako wa kienyeji mihela kibao ili akuunge na Frimason ili wakupe dawa ya utajiri, unajikuta siku zinapita hakuna cha utajiri wala nini, ukienda kwa mganga wako kumuuliza ndipo atakapoanza visingizo, kwanza anaanza kukuuliza, ‘Ulifwata masharti yote niliyokwambia?, Uliweza kutoa sadaka ya siafu kumi wa kiume?’ Ukisita tu kujibu, ndipo ataanza, ‘Unaona hilo ndio tatizo lenu nyie wateja, sisi tunaongea na mizimu inatoa masharti nyie hamfuati halafu mnalalamika’ Hapo hata ujitetee kuwa hakukwambia hilo atang’ang’ania kuwa alikutaarifu wakati anakupa ile dawa ya kinga ya kuzuia wabaya wasikuone utakapotajirika. Juzi niliingia kwenye ofisi za kampuni moja ya simu kulalamika kwanini kila nikinunua bando ya siku inaisha kabla siku haijaisha, nikinunua bando ya wiki inaisha baada ya siku tatu. Dahh kabinti flani emeizing kalikokuwa kanaongea Kiswahili cha mahauzgelo wa wazungu, kakaniuliza jina, umri, kazi ninayofanya, idadi ya watoto, kisha kuomba kuona aina ya simu ninayotumia. Halafu ndo kakaanza kuleta kisingizio. “Mzee umeshasoma masharti yetu kuhusu bando?” Nikakaambia sijawahi kuyaona kwani yako wapi? ‘Sasa mzee we unatumia bando zetu bila kujua masharti yake? Wewe kama mteja unatakiwa ujue masharti yetu. Sisi kama kampuni tunakata vati kwenye hela yako ya bando, pia tunakadiria masaa ambayo yako katika mzunguko wa eataim yetu na kulinganisha na thamani ya dola ya siku hiyo, ndio tunajua  siku hiyo ina masaa mangapi nadhani umeelewa ?” Sikuwa nimeelewa nikaondoka taratibu bila kuaga. Ila kali zaidi ni ya huyu jamaa yangu aliyetembelewa na mkewe  ghafla ofisini kwake, akakutwa kampakata sekretari wake wananyweshana chai, mama wa watu alipowaona moyo ukataka kumtoka, akili ikasimama kufanya kazi, muda uliotosha kabisa kwa sekretari kutimua mbio na kumpita yule mama akiwa kasimama mlangoni kama sanamu. Bosi akaanza kumkaribisha mkewe kama vile hakuna cha ajabu kimetokea. ‘Aise wife karibu sikujua unakuja, yaani hapa kwa kweli tunafanya kazi kwa stress sana, yaani serikali imebana matumizi mpaka inakera, hebu ona wafanyakazi wawili tunalazimika kutumia kiti kimoja na kikombe kimoja cha chai, hii haikubaliki kabisa yaani mi naona heri niache kazi nirudi kwetu nikalime”

No comments: