PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

KOSA LAKO MWENYEWE BABA, HUKUMTAARIFU KUWA UNARUDI


Kuoa si mchezo nawambieni ohoo. Najua kuna watu wataanza kunibisha. Unajua Bongo kuna watu wabishi huwezi kuamini, yaani mtu anaweza kubishana mpaka na redio. Kuna kabila naogopa kulitaja wabishi hao, kuna mwaka mmoja timu ya mkoa wao ilicheza soka na timu ya mkoa mwingine, ukapigwa mpira wa kona na kuingia golini bila kuguswa, jamaa wakabisha kuwa sio goli. Kwa hiyo siwezi kushangaa wakibisha kuwa kuoa si mchezo. Yuko rafiki yangu mmoja aliamua kuoa, wote tulikuwa na wasiwasi maana huyo mchumba wake alikuwa hajatulia kabisa. Lakini si unajua mtu ukipenda unavyokuwa mbishi. Tukaanza ishu za michango, tena siku hizi rahisi, sana ukiona unakaribia kuoa unaanzisha magrupu ya watsap kusudi uwakamue michango. Mambo yakaenda poa hatimae siku ya siku ikafika watu tukala tukanywa mwenzetu akawa ameoa. Shem bwana alikuwa utadhani hajaolewa, ratiba zake zilikuwa zilezile na watu walewale, kwa kuwa tulikwisha jua kabla hatukushtuka, na jamaa yetu nae alionekana yuko poa tu, maisha yakaendelea. Sasa kuna siku jamaa yetu akapata kasafari ka kikazi kwenda Kenya. Akaa huko kama mwezi akarudi bila taarifa. Jamaa kaingia mjini muda wa saa tano usiku moja kwa moja kafika kwake na kugonga dirisha la chumba chake cha kulala ili mkewe amfungulie mlango, si ndio aliposikia sauti ya mwanaume ikiuliza bila wasiwasi, ‘Nani wewe?’. Jamaa yetu akashtuka na kujibu, ‘Unaniuliza mimi nani toka chumbani kwangu?’ Kulikuwa na kimya cha muda mfupi na ghafla kukawa na vurugu za mtu akitimka na nusu dakika baadae kuna jamaa alichomoka kupitia mlango wa mbele na kupotelea gizani. Jamaa yetu aliingia ndani kachanganyikiwa. Shem akaenda kujificha chumba cha mpangaji mwingine maana alijua anaweza kupata kipigo cha mbwa mwizi. Jamaa alilala asubuhi akadamkia kwa mama mkwe wake na kumueleza jinsi alivyodhalilika kwa kukuta mwanaume chumbani kwake. Mama mkwe alionekana kusikitika sana kwa hili, lakini alianza kuongea mambo ya ajabu sana, akaanza kusema, ‘Unajua baba kwa kweli hata mimi nimesikitika sana, hivi huyu binti yangu kwanini kafanya ujinga kama huu, baba naomba nimpigie simu niongee nae maana hili jambo la ajabu sana’. Mama  mkwe akatoka nje na kumpigia simu binti yake. Baada ya dakika tatu akarudi. ‘Baba kama nilivyokwambia hata mimi nimeshangaa sana kitendo cha binti yangu, lakini sasa nimepata jibu ilikuwaje’. Jamaa akamuangalia mama mkwe wake kama hamuelewi hivi kisha akamuuliza, ‘Mama sikuelewi kwani kakwambia nini?’ Mama mkwe akamjibu jamaa kwa upole sana, ‘Baba kosa ni lako. Kumbe ulirudi ghafla bila ya kumtaarifu mwenzio? Angekuwa na taarifa wala haya yote yasingetokea baba”

Comments