HATUPIMI BANDO

20 July 2016

KOSA LAKO MWENYEWE BABA, HUKUMTAARIFU KUWA UNARUDI


Kuoa si mchezo nawambieni ohoo. Najua kuna watu wataanza kunibisha. Unajua Bongo kuna watu wabishi huwezi kuamini, yaani mtu anaweza kubishana mpaka na redio. Kuna kabila naogopa kulitaja wabishi hao, kuna mwaka mmoja timu ya mkoa wao ilicheza soka na timu ya mkoa mwingine, ukapigwa mpira wa kona na kuingia golini bila kuguswa, jamaa wakabisha kuwa sio goli. Kwa hiyo siwezi kushangaa wakibisha kuwa kuoa si mchezo. Yuko rafiki yangu mmoja aliamua kuoa, wote tulikuwa na wasiwasi maana huyo mchumba wake alikuwa hajatulia kabisa. Lakini si unajua mtu ukipenda unavyokuwa mbishi. Tukaanza ishu za michango, tena siku hizi rahisi, sana ukiona unakaribia kuoa unaanzisha magrupu ya watsap kusudi uwakamue michango. Mambo yakaenda poa hatimae siku ya siku ikafika watu tukala tukanywa mwenzetu akawa ameoa. Shem bwana alikuwa utadhani hajaolewa, ratiba zake zilikuwa zilezile na watu walewale, kwa kuwa tulikwisha jua kabla hatukushtuka, na jamaa yetu nae alionekana yuko poa tu, maisha yakaendelea. Sasa kuna siku jamaa yetu akapata kasafari ka kikazi kwenda Kenya. Akaa huko kama mwezi akarudi bila taarifa. Jamaa kaingia mjini muda wa saa tano usiku moja kwa moja kafika kwake na kugonga dirisha la chumba chake cha kulala ili mkewe amfungulie mlango, si ndio aliposikia sauti ya mwanaume ikiuliza bila wasiwasi, ‘Nani wewe?’. Jamaa yetu akashtuka na kujibu, ‘Unaniuliza mimi nani toka chumbani kwangu?’ Kulikuwa na kimya cha muda mfupi na ghafla kukawa na vurugu za mtu akitimka na nusu dakika baadae kuna jamaa alichomoka kupitia mlango wa mbele na kupotelea gizani. Jamaa yetu aliingia ndani kachanganyikiwa. Shem akaenda kujificha chumba cha mpangaji mwingine maana alijua anaweza kupata kipigo cha mbwa mwizi. Jamaa alilala asubuhi akadamkia kwa mama mkwe wake na kumueleza jinsi alivyodhalilika kwa kukuta mwanaume chumbani kwake. Mama mkwe alionekana kusikitika sana kwa hili, lakini alianza kuongea mambo ya ajabu sana, akaanza kusema, ‘Unajua baba kwa kweli hata mimi nimesikitika sana, hivi huyu binti yangu kwanini kafanya ujinga kama huu, baba naomba nimpigie simu niongee nae maana hili jambo la ajabu sana’. Mama  mkwe akatoka nje na kumpigia simu binti yake. Baada ya dakika tatu akarudi. ‘Baba kama nilivyokwambia hata mimi nimeshangaa sana kitendo cha binti yangu, lakini sasa nimepata jibu ilikuwaje’. Jamaa akamuangalia mama mkwe wake kama hamuelewi hivi kisha akamuuliza, ‘Mama sikuelewi kwani kakwambia nini?’ Mama mkwe akamjibu jamaa kwa upole sana, ‘Baba kosa ni lako. Kumbe ulirudi ghafla bila ya kumtaarifu mwenzio? Angekuwa na taarifa wala haya yote yasingetokea baba”

13 July 2016

DAI RISITI OHOO


Sasa  inalazimika kudai risiti kwa kila huduma, maana mambo yamekuwa ndivyo sivyo kabisaaa. Yaani mambo yaliyokuwa bure zamani siku hizi watu wanadai malipo tena kwa kutangaza kabisa hadharani. Juzi tu nimesoma mdada mmoja msupasta katangaza kuwa anaetaka kuwa mpenzi wake ajipange, hataki mapenzi na mtu ambaye akimuomba hela ya matumizi amwambie eti hana. Haya mapenzi ya kidot kom mbona kizungumkuti? Mapenzi gani ya kupangiana masharti? Sasa kama ukiwa fala unakubali masharti namna hiyo, kwanza ujue kabisa kuwa  wewe kweli fala mzoefu. Yaani asubuhi unaamka tu unasikia ‘Bebi leo nataka kula soseji na mayai ya kukaanga yenye mbogamboga ndani na kipande cha samaki, maziwa fresh na juis, naomba alfu ishirini nimtume dada akanunue’. Unatoa. Nusu saa baadae ‘Bebi naona losheni yangu imeisha huwa natumia ile inaitwa D’Or naomba alfu stini nikanunue’ Unatoa. ‘Bebi nataka kwenda Mbagala kumsalimia dada naomba alfu hamsini za teksi na hela kidogo ya kumpa dada anaumwa, laki na ishirini zitasaidia’ Unatoa. Wakati yuko kwa dada anakupigia simu, ‘Bebi huku nimemkuta dada moja anauza madira mazuri nimechukua matatu shilingi alfu stini naomba unitumie kwenye simu’ Unatoa. ‘Bebi nataka kurudi ile hela ya teksi haitoshi’ Unatoa. ‘Bebi napita hapa saluni kuosha nywele, usinitumie pesa ntamkopa tumlipe kesho bebi, shilingi elfu hamsini tu’ Unajibu ‘Sawa’. Akifika home anakwambia kachoka analala ila, ‘Bebi leo nitoe out nasikia kuna klabu mpya wenzangu wote wameshaenda kasoro mimi tu. Halafu sina hata nguo ya kuvaa tukienda huko ntakimbia hapo kwa Da Tunu ameleta nguo nzuri toka China japo anikopeshe tumlipe wiki ijayo au siyo bebi?’ Unakubali.
Jioni mnatoka, kwa masharti kuwa teksi iwafuate tena ambayo ataagiza yeye, anakwambia ‘Bebi tupitie kwa Anko Kitime kwanza tule mishkaki anamishkaki mizuri sana’ Mnapitia mnanunua mishkaki kama thelathini hivi na chips. Kisha ndipo mnaelekea klabu. Kufikia saa saba, laki tatu imefutika kwa vinywaji  vyenu na vya rafiki zake, wewe mwenyewe umekunywa maji chupa ndogo mbili. Siku ya kwanza imeisha mnarudi kulala. Mkiamuka mzunguko unaanza,  aise dai risiti kwa kila kitu hapo, maana katika kila risiti kuna pasenteji inayobaki kwa serikali na katika hela ile ndio tunapeleka huduma kwa wananchi………

SWALI NIMRUDISHIE MCHUNGAJI HELA YAKE?

NILIKUWA nimeishiwa sana njaa inaniuma kwa bahati nikakutana na mchungaji wangu mtaani. Nikamueleza tatizo langu na kumuomba japo alfu mbili nikanunue chips mayai. Kwa masikitiko makubwa mchungaji akanambia hana hata senti au lazima angenisaidia mimi mwanakondoo wake, lakini akaniwekea mikono kichwani na kuniombea Mungu afanye muujiza nipate pesa ya kula. Alipomaliza kuniombea wakati anaondoka akatoa kitambaa mfukoni ajifute jasho, na pale pale noti ya shilingi alfu kumi ikadondoka Mchungaji hakuiona akaendelea na safari. Swali Je, nimshtue Mchungaji au ndio muujiza alioniombea umetokea?

6 July 2016

NINAFIKIRIA KURUDI SHAMBA


Hahahahaha yaani kila siku Bongo kuna kichekesho kipya, mi nashangaa unamkuta mtu kanuna siku nzima anapata mastresi na pengine kupata vidonda vya tumbo na presha wakati mambo ya kuondoa presha yamejaa kila kona. Hebu angalia kwa mfano jinsi Wabongo walivyo mabingwa wa visingizio, kila jambo likikwama kuna bonge ya kisingizio. Kwa mfano ukishamlipa mganga wako wa kienyeji mihela kibao ili akuunge na Frimason ili wakupe dawa ya utajiri, unajikuta siku zinapita hakuna cha utajiri wala nini, ukienda kwa mganga wako kumuuliza ndipo atakapoanza visingizo, kwanza anaanza kukuuliza, ‘Ulifwata masharti yote niliyokwambia?, Uliweza kutoa sadaka ya siafu kumi wa kiume?’ Ukisita tu kujibu, ndipo ataanza, ‘Unaona hilo ndio tatizo lenu nyie wateja, sisi tunaongea na mizimu inatoa masharti nyie hamfuati halafu mnalalamika’ Hapo hata ujitetee kuwa hakukwambia hilo atang’ang’ania kuwa alikutaarifu wakati anakupa ile dawa ya kinga ya kuzuia wabaya wasikuone utakapotajirika. Juzi niliingia kwenye ofisi za kampuni moja ya simu kulalamika kwanini kila nikinunua bando ya siku inaisha kabla siku haijaisha, nikinunua bando ya wiki inaisha baada ya siku tatu. Dahh kabinti flani emeizing kalikokuwa kanaongea Kiswahili cha mahauzgelo wa wazungu, kakaniuliza jina, umri, kazi ninayofanya, idadi ya watoto, kisha kuomba kuona aina ya simu ninayotumia. Halafu ndo kakaanza kuleta kisingizio. “Mzee umeshasoma masharti yetu kuhusu bando?” Nikakaambia sijawahi kuyaona kwani yako wapi? ‘Sasa mzee we unatumia bando zetu bila kujua masharti yake? Wewe kama mteja unatakiwa ujue masharti yetu. Sisi kama kampuni tunakata vati kwenye hela yako ya bando, pia tunakadiria masaa ambayo yako katika mzunguko wa eataim yetu na kulinganisha na thamani ya dola ya siku hiyo, ndio tunajua  siku hiyo ina masaa mangapi nadhani umeelewa ?” Sikuwa nimeelewa nikaondoka taratibu bila kuaga. Ila kali zaidi ni ya huyu jamaa yangu aliyetembelewa na mkewe  ghafla ofisini kwake, akakutwa kampakata sekretari wake wananyweshana chai, mama wa watu alipowaona moyo ukataka kumtoka, akili ikasimama kufanya kazi, muda uliotosha kabisa kwa sekretari kutimua mbio na kumpita yule mama akiwa kasimama mlangoni kama sanamu. Bosi akaanza kumkaribisha mkewe kama vile hakuna cha ajabu kimetokea. ‘Aise wife karibu sikujua unakuja, yaani hapa kwa kweli tunafanya kazi kwa stress sana, yaani serikali imebana matumizi mpaka inakera, hebu ona wafanyakazi wawili tunalazimika kutumia kiti kimoja na kikombe kimoja cha chai, hii haikubaliki kabisa yaani mi naona heri niache kazi nirudi kwetu nikalime”