HATUPIMI BANDO

28 April 2016

NATAKA KUOA MDOSI


KATIKA kipindi kirefu sasa nimekuwa naangalia uwezekanao wa kuoa. Hii ishu ya kula ugali mbichi niliousonga mwenyewe kiukweli inaniudhi. Nikiwacheki jamaa zangu tuliocheza pamoja utotoni wote wana wake zao na watoto kadhaa, tena wengine wana zaidi ya mke mmoja na tukikutana mtaani utakuta wanaelekea kwenye michepuko yao, kimsingi wako bizi sana. Mimi nimekuwa napanga na ma mimi niwe na mke. Jambo moja ambalo nimeamua ni kuwa sioi Bongo hata iweje, toka hizi instagram na whatsap zimeingia mjini, wadada wa hapa wamekuwa na timu zao, hebu fikiria ukioa mke mwenye timu ya nguvu si ndio utatukanwa instagram kila asubuhi. Lazima nioe kitu toka nje ya nchi, hii kwanza itasaidia hata kuleta mabadiliko katika ukoo wangu, na Taifa letu kwa ujumla. Pili italeta  sifa, japokuwa mtu mmoja kwenye ukoo wetu kaoa mgeni toka nje ya nchi, tatu itapunguza umbeya, maana ntaleta mke hajui Kiswahili, hivyo wifi zake wakianza mafumbo, ye haelewi anacheka tu. Halafu na yeye mwenyewe atakuwa hana cha kuongea hata akienda saluni, mambo yetu yatabaki kuwa siri. Nimeshaanza utafiti, nimekuwa natumia muvi mbalimbali kujifunza Taifa gani linafaa kuoa. Kwanza nimeshajua kuwa siji kuoa Mnaijeria, we angalia muvi zao, wadada wa Kinaijeria wagomvi hao, hawaoni tabu kulianzisha saa yoyote, halafu hawaoni tabu kukuendea kwa mganga. Wanaijeria siwataki kabisaaa. Baada ya kuona muvi za akina Kim Kadeshian na vituko vya baba yao, sitaki kuoa Mmarekani kabisa, hebu fikiria baba mkwe kabadilisha jinsia kawa mdada, sasa unamwita baba mkwe au unamwita mama mkwe? Wamrekani tupa kule. Ila mpaka sasa roho yangu imewaangukia Wahindi, nimepanga kumuoa Mdosi. Yaani sauti za mabinti wa Kihindi wakiimba utapenda, sura zao wote nzuriiii, halafu sio wagomvi wapole yaani kwa kweli hapo ndio chaguo langu. Ila kuna changamoto kubwa sana kumpata mdada wa Kidosi hapa kwetu. Kwenye muvi hawa wadada utakuwakuta kwenye bustani kama ya Mnazi Mmoja wanaimba na kufukuzana na wapenzi wao, sasa mbona hapa kwetu sijawahi kuwaona wapenzi wa namna hiyo wakifukuzana na kuparamia miti wakiimba kwa mapenzi. Mimi nimeshajifua naweza kuimba na kucheza wimbo wote wa Kuch kuch kotaye. Mkimuona binti wa Kihindi wa umri wa kuolewa nielekezeni ili nikamuimbie niweze kupata mke. Hapa Kazi moja tu, kuoa Mhindi mwaka huu.