PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

WAMENIUZIA MCHICHAAAA

Baada ya kuhangaika muda mreeefu kutafuta njia ya kuingia studio kurekodi nyimbo zake , hatimae jamaa yangu jina nalihifadhi, akakutana na  jamaa wakamwambia kuwa wao wanamfahamu mtu mwenye studio. Ndugu yangu akasindikizana na rafiki zake wapya mpaka jengo moja akaambiwa hapo ni studio, akakuta vijana wenzie nje ya lile jingo, wengine akawafahamu, wasanii maarufu ambao aliwahi kuwaona tu kwenye TV na magazeti , hapo akajua lazima nae sasa atakuwa mmoja wa wasanii maarufu Bongo hii.  Baada ya hapo kila siku akawa anafika pale studio akibembeleza nae kuingia kurekodi wimbo wake, kitu alichokigundua mapema ni kuwa wengi wa wasanii walikuwa wakivuta sigara, lakini kichwani akajua hii si sigara halali maana harufu ya sigara hiyo ulikuwa tofauti, na uvutaji wake uikuwa wa kisirisiri. Baada ya hapo ilionekana  waliovuta walikuwa wakichangamka  na kuchekacheka bila mpango huku mistari ikianza kuwatoka mfululizo. Ikaonekana kila mtu anajisifia alivyovuta sigara hiyo mara ya mwisho mara ya mwisho kwa stori za kufurahisha, jamaa yangu peke yake akawa hana stori ya kueleza, polepole akaanza kuwaza namna ya kuaanza kuvuta  sigara wanayovuta wale masupasta. Hilo lilikuwa kosa la kwanza. Swali likawa atapata wapi, na hakutaka aulize maana wenzie wangejua kuwa yeye mshamba na  kuwa hajawahi kuvuta ile sigara wala hajui inapatikana wapi. Hatimae akagundua kuwa kuna jamaa alikuwa akija pale studio ndio aliyekuwa akileta zile sigara zenye harufu tofauti. Siku hiyo akamfwatilia na kumsimamisha. Kwa wasiwasi akaanza, ‘Mambo bro”. Jamaa akajibu, “Poa nikusaidie nini?” ‘ Nilikuwa nataka ile kitu”. “Kitu gani kuwa muwazi” Hapo akasita maana hakujua sigara zile zinanunuliwa kwa pakiti au moja moja. “Naomba zile sigara” Muuzaji akamuangalia machoni,”We mgeni ehh? Haya unataka kiasi gani, aina gani?”, “Nichagulie wewe ile unayoona nzuri“,  Muuzaji akachekaa sana  “Haya leta alfu mbili nikupe kitu cha Makambako chenye mix” ,pamoja na kuwa alikuwa haelewi maana ya maelezo hayo akajikakamua na kujibu, “Yah hiyo sio mbaya”. Jamaa yangu akatoa pesa akapewa kitu kimefungwa kwenye karatasi, kwa spidi akaondoka na kurudi studio.  Kufika studio akazunguka nyuma ya jingo ambako ndiko wavutaji walikuwa wakijificha na kuvuta. Akafungua na kukuta majani haraka kwa kuangalia wengine akasokota sigara yake  na kuomba kibiriti na kuanza kuvuta. Kosa la pili alivuta moshi mwingi mno, akaanza kukohoa bila kupumzika, huku wenzie jirani wakimcheka bila kumsaidia. Akajikaza na kuendelea kuvuta hadi sigara ikaisha, kilichomsikitisha ni kutokusikia mabadiliko yoyote, na hivyo kujua kuwa katapeliwa kauziwa mchicha. Haraka akaanza kulalamika kwa wote waliokuwepo pale, “Unajua jamaa kaniuzia mchicha? Unajua nimeuziwa mchicha?” Kila mtu akaanza kumuangalia kwa makini na kumshangaa kuhusu mada hiyo mpaya ambayio aliianza ghafla. Jamaa yangu akaingia studio na kukuta kazi ya kurekodi inaendelea, bila wasi wasi akamtaarifu producer tatizo lake. “Producer subiri kwanza unajua jamaa kaniuzia mchicha shilingi alfu mbili” Producer akabaki anashangaa na kumshauri jamaa atoke nje ya studio. Jamaa yangu huku akishangaa kwanini watu hawamuelewi kuwa alitegemea kauziwa kitu cha kumpa stimu badala yake kauziwa mchicha.  Rafiki zake waliomkaribisha studio wakamfuata na kujaribu kuelewa nini kinaendelea. Ndipo akawapa mkasa mzima na kuwaeleza jinsi alivyotapeliwa kwa kuuziwa mchicha kidogo kwa shilingi alfu mbili. Hapo ndipo wenzie wote wakajua kuwa mwenzao akili si yake. Wakamshauri apumzike kwenye kochi aondoe uchovu..  Jamaa yangu akawa anasikia sauti kichwani mwake ikimwambia vua nguo  kabla hujalala kwenye kochi maana kuna joto. Hapo akaomba ushauri kwa wenzie avue au asivue. Zogo kubwa likaanza studio, jamaa yangu akisisitiza kuwa lazima avue nguo ili aweze kulala kwa amani kwenye kochi. Hapo kazi ikawa kuwaza namna ya kumsaidia jamaa akili imrudie, wengine wakasema apewe maziwa wengine amwagiwe maji, wengine wakidai awekwe chini ya feni, mwenye aking’ang’ania kuvua nguo.  Ghafla akaanza kudai moyo unataka kutoka, akawa ajiziba mdomo akidai moyo unataka kutokea mdomoni, na akaatimua mbio masupastaa kadhaa wakimfukuza. Jamaa akaaingia hoteli ya jirani na kuomba maji maana moyo unataka kumtoka. Hatimae alikamatwa na wenzie kumrudisha kwao ambako alikimbilia kwa baba yake na kushtaki kuwa kauziwa machicha  wa shilingi alfu mbili na tapeli.

Comments