PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

BARA SIRUDI TENA YAKHEEEE

Rafiki yangu Mwinchumu, mkazi wa Dole, hukooo Zanzibar alinikaribisha nikamtembelee Zanzibar, mwenyewe alinipa sifa hizi za Zanzibar, 'Njoo yakhe ubabadili upepo, ule urojo, usikilize taarab asili'.  Nami hili nililipokea kwa furaha kubwa, we fikiria mtu kutoka Iringa kuvuka bahari mpaka Zanzibar, mbona ningerudi Iringa wangenikoma. Nikingia kilabuni watu wangekuwa wananong’onezana, ‘Aise huyo jamaa aliwahi kwenda Zanzibar, hebu mpeni kisado cha ulanzi atuhadithie kukoje huko’, nina uhakika ile ningerudi tu ningepata hata mke. Si mchezo waif angekuwa anajisifu kisimani.’Mume wangu aliwahi kwendaga Zanzibar”. Kijijini kwetu hawana dogo wangetunga hata wimbo. Maana kuna jamaa kijiji cha jirani aliwahi kuwa na ndugu yake aliyepanda ndege basi akatungungiwa wimbo, 'Wagendye mwindege salama', yaani ulisafiri na ndege ukarudi salama,
Hatimae siku ilifika nikawa nimeshafika bandarini tiketi mkononi nikaingia kwenye meli, sijui kwanini rafiki yangu Mwinchumu alikuwa anaiita hii meli ‘chombo’, kwetu chombo ni bakuli na sahani. Basi nikaingia kwenye chombo. Kulikuwa na viti vingi, maTV kila upande yanaonyesha masinema, nikatafuta kiti nikakaa, pembeni nikaona kagrosari nikaenda na kununua juis ya mapera na sambusa kumi. Unajua kwetu mapera ni kitu unaanza kula toka una umri wa miaka miwili, hivyo juis yake inanikumbusha mbali sana, halafu nilikuwa na hamu sana na sambusa. Nikarudi kwenye kiti changu na kuanza kula na kunywa kwa furaha. Chombo kikaanza safari, nikaanza kuiona Darisalama hiyooo inapotea taratibu. Mara akapita mhudumu akatugawia mifuko ya rambo, sikutaka kuonekana mshamba na mimi nikapokea na kuuhifadhi nikajua lazima hawa jamaa wakati wa safari watagawa korosho au karanga au pengine hata sambusa, hivyo wanagawa mifuko kwanza.
Kausingizi lazima kalinichukua, maana ghafla nikashtuka, yaani fujo, tulikuwa tunarushwa mara tunashushwa, kuagalia nje, mawimbi makubwa yalikuwa yanakiyumbisha chombo. Nikajua ndio tunazama, macho yakanitoka, nikajizuia kupiga kelele. Nikaanza kujisikia hovyovyo, yaani tumbo likawa kama linapigwa ngumi. Nikawa naona kizunguzungu cha ajabu, nikawa naanza kusikia kichefuchefu, boti inarukaruka huko na kule, nikawa nimejishikilia kwenye kiti kwa nguvu. Nilifunga macho tabu, nilifungua macho shida, cha ajabu niliona mama mmoja anamnywesha juis mwanae, nao hawana wasiwasi kabisaaa, nini kilikuwa kikinitokea mimi? Pembeni kule nikaona mtu mmoja anatapikia kwenye mfuko ya Rambo, hapo ndipo nikagundua kazi ya ile mifuko niliogawiwa. Kwa kweli nilikuwa najua sasa nafia baharini, yaani Mnyalu nafia kwenye maji? Halafu hata kuoa sijaoa.  Chombo kilivyokuwa kinarushwa kama karatasi, na nilivyokuwa najisikia nilianza kukumbuka sala zote na matambiko yote ya kikwetu. Nilichukua mfuko wangu wa Rambo, nikatapika juis ya mapera na sambusa zote kumi na chai niliyokunywa asubuhi hata ugali wa jana nao ulitoka, ukawa utumbo nao unataka kutoka. Sikumbuki mengi ila nakumbuka kwa mbali nasikia watu wanasema tumefika Zanzibar, muhudumu mmoja akaninyanua na kuanza kunitoa nje, miguu ilikuwa inakataa kusimama, wakanitoa nje, nikakutana na Mwinchumu, nae kuniona eti kaanza kucheka,’ Yakhe vipi tena hahahaha? Mbona umelegea karibu Unguja yakhe’ Kwa kweli sikumjibu nilikuwa tayari naanza kufikiria kwa woga safari ya kurudi Iringa. Na kama mambo yenyewe yanakuwa kurudia yaliyonikuta leo, nikajikuta narudia tena na tena, ’Mwinchumu, Mwinchumuee mi Bara sirudi tena”

Comments