HATUPIMI BANDO

31 March 2016

ENZI ZETU MWENYE MPIRA NDIE ANACHAGUA TIMU


Enzi hizo wakati bado ningali mtoto, kila mtaa ulikuwa na kiwanja cha kuchezea, tena kikubwa maana unaweza ukakuta michezo mitatu ya soka na michezo miwili ya netiboli inaendelea kwa wakati mmoja, achana na wale waliokuwa wakicheza mdako, kiboleni, gololi na hata kufukuzana tu. Kwenye soka enzi zile, tulikuwa na sheria zetu za kuongoza mchezo huo. Sheria zetu hazikuwa zinafwata za FIFA, kwanza wakati huo hata hilo neno FIFA tulikuwa hatulijui. Wenyewe tulijitengenezea amri ambazo hazikuandikwa popote lakini kila mtu alikuwa anazijua kimoyomoyo. Tulikuwa na amri zetu kama kumi hivi. Kwanza wakati huo mipira yenyewe ilikuwa tabu kupatikana hivyo wengi tulikuwa tunatengeneza wenyewe kwa kufunga makaratasi na kuanza mechi ambazo kupumzika ni uamuzi tu, inawezekana mtu kishafungwa 20 kwa kumi na mbili, basi mnaamua kupumzika. Lakini ilikuwa ikitokea mwenzenu mmoja wazazi wake wako vizuri wakamnunulia mpira wa kweli, hapo basi kidogo kulikuwa na taratibu mpya katika kuchezea mpira ule. Tulijitengenezea amri kama kumi hivi. Amri ya kwanza ilikuwa mwenye mpira ndie anaeamua nani atacheza, hivyo kama uliwahi kumnyima kashata au andazi ni wazi huchezi. Amri ya pili ilikuwa mtoto bonge ndie golikipa, hilo lilikuwa halina ubishi. Tatu ni kuwa wachezaji wazuri ndio wanaochaguliwa kwanza na mwenye mpira kuwa watakuwa timu yake. Amri ya nne ilikuwa kukiwa na penati ruksa kubadilisha kipa kama kipa wenu hamumuamini. Amri ya tano ya mpira enzi zetu ni kuwa ukipiga mpira kwa nguvu au kwa mandochi yaani kwa vidole, kumbuka tulikuwa hatuvai viatu, basi mwenye mpira ana ruksa ya kukuonya au kukukataza usicheze. Amri ya sita ya mpira enzi zetu ni kuwa usipochagia hela ya kujaza upepo mpira utapigwa marufuku kucheza. Amri ya saba ilikuwa hakuna marefa wala washika vibendera, na mpira unachezwa mpaka kuzunguka goli, ila mwenye mpira anaweza akageuka refa wakati wowote na atakachosema lazima kiwe. Kati ya amri muhimu ilikuwa ni ile ya nane, si ruhusa kabisa kumkaba mwenye mpira, hiyo ni faulo. Ya tisa ni kuwa ukitoboa mpira unalipa. Mwisho ni kuwa mwenye mpira akikasirika au akiumia au akiitwa na mama yake ndio mwisho wa mechi.

24 March 2016

CHEZEA MUOSHA MAGARI WEWE


Yaani kuna mdada kanitumia barua juzi anataka ushauri nimebaki nimeduwaa sina la kusema kabisa. Ninachoweza kusema ni kuwa sasa nina uhakika wa ule msemo wa wahenga kuwa Kupenda Upofu. Hebu  na nyinyi hebu someni wenyewe mi nakaa pembeni.
Anko Shikamoo,
Vipi mzima? Anko mie huwa napenda sana kusoma makala zako, na zinanifurahisha sana, na nikisoma naona kuwa wewe una busara sana, sasa nimepata tatizo naomba unipe ushauri babu yangu. Naomba unisaidie pliz. Anko huu ni mwezi wa nne toka nimeolewa, yaani tayari najilaumu sana kuhusu ndoa hii. Kiukweli najuta sana. Kabla ya kunioa mume wangu alikuwa anakuja kwangu kila siku na gari jingine, akanambia kazi yake ni dalali wa magari, na akaniahidi kuwa na mimi ataninunulia gari ili nisiwe na tatizo la usafiri. Niliongeza mapenzi kwake ili asijekusahau kunipa gari. Uchumba wetu ulichukua miezi mitatu kisha tukaoana katika ndoa ambayo mpenzi wangu alisema tufanye kakitu kadogo tu kakisiri tusiharibu pesa. Ndugu zangu walininunia lakini mimi sikujali. Kwa kuwa nilikuwa na chumba kizuri katikati ya mji, ilionekana maisha tuanze kwetu maana mume wangu akisema alikuwa akiishi na mama yake nje ya mji, aliyekuwa akimkataza asipange chumba. Huwezi kuamini Anko, si juzijuzi tu ndio nimegundua kumbe nilikuwa nadanganywa siku zote, kumbe mume wangu kazi yake ni kuosha magari, hana udalali wala nini. Kuna kijiwe chao kando yam to wanaosha magari mchana kutwa sasa akiachiwa aoshe gari basi ndio huzunguka nalo na ndipo alipoweza kunidanganya nikaingia kingi. Kwanini alinidanganya vile? Si angenieleza tu ukweli nijue? Ntaendeleaje kumuamini sasa?  Mbaya zaidi mi nimemaliza chuo kikuu na  nimegundua kuwa jamaa hakumaliza hata fom tu,  Anko what do I do? Wenzangu walikuwa wananicheka nilikuwa siwaelewi. Nilikuwa kila siku napiga picha niko kwenye gari tofauti nazituma instagram, jamani watu wakigundua si ndio watanichamba mwaka mzima? Ndugu zangu walinionya  kuwa wanamuona jamaa tapeli nikagombana nao sana, narudije kwetu? Anko nipe ushauri.
 Hata mimi sijui nimwambieje huyu mdada, hivi alikuwa fala kiasi gani hakuona kuwa anatapeliwa?

22 March 2016

WAMENIUZIA MCHICHAAAA

Baada ya kuhangaika muda mreeefu kutafuta njia ya kuingia studio kurekodi nyimbo zake , hatimae jamaa yangu jina nalihifadhi, akakutana na  jamaa wakamwambia kuwa wao wanamfahamu mtu mwenye studio. Ndugu yangu akasindikizana na rafiki zake wapya mpaka jengo moja akaambiwa hapo ni studio, akakuta vijana wenzie nje ya lile jingo, wengine akawafahamu, wasanii maarufu ambao aliwahi kuwaona tu kwenye TV na magazeti , hapo akajua lazima nae sasa atakuwa mmoja wa wasanii maarufu Bongo hii.  Baada ya hapo kila siku akawa anafika pale studio akibembeleza nae kuingia kurekodi wimbo wake, kitu alichokigundua mapema ni kuwa wengi wa wasanii walikuwa wakivuta sigara, lakini kichwani akajua hii si sigara halali maana harufu ya sigara hiyo ulikuwa tofauti, na uvutaji wake uikuwa wa kisirisiri. Baada ya hapo ilionekana  waliovuta walikuwa wakichangamka  na kuchekacheka bila mpango huku mistari ikianza kuwatoka mfululizo. Ikaonekana kila mtu anajisifia alivyovuta sigara hiyo mara ya mwisho mara ya mwisho kwa stori za kufurahisha, jamaa yangu peke yake akawa hana stori ya kueleza, polepole akaanza kuwaza namna ya kuaanza kuvuta  sigara wanayovuta wale masupasta. Hilo lilikuwa kosa la kwanza. Swali likawa atapata wapi, na hakutaka aulize maana wenzie wangejua kuwa yeye mshamba na  kuwa hajawahi kuvuta ile sigara wala hajui inapatikana wapi. Hatimae akagundua kuwa kuna jamaa alikuwa akija pale studio ndio aliyekuwa akileta zile sigara zenye harufu tofauti. Siku hiyo akamfwatilia na kumsimamisha. Kwa wasiwasi akaanza, ‘Mambo bro”. Jamaa akajibu, “Poa nikusaidie nini?” ‘ Nilikuwa nataka ile kitu”. “Kitu gani kuwa muwazi” Hapo akasita maana hakujua sigara zile zinanunuliwa kwa pakiti au moja moja. “Naomba zile sigara” Muuzaji akamuangalia machoni,”We mgeni ehh? Haya unataka kiasi gani, aina gani?”, “Nichagulie wewe ile unayoona nzuri“,  Muuzaji akachekaa sana  “Haya leta alfu mbili nikupe kitu cha Makambako chenye mix” ,pamoja na kuwa alikuwa haelewi maana ya maelezo hayo akajikakamua na kujibu, “Yah hiyo sio mbaya”. Jamaa yangu akatoa pesa akapewa kitu kimefungwa kwenye karatasi, kwa spidi akaondoka na kurudi studio.  Kufika studio akazunguka nyuma ya jingo ambako ndiko wavutaji walikuwa wakijificha na kuvuta. Akafungua na kukuta majani haraka kwa kuangalia wengine akasokota sigara yake  na kuomba kibiriti na kuanza kuvuta. Kosa la pili alivuta moshi mwingi mno, akaanza kukohoa bila kupumzika, huku wenzie jirani wakimcheka bila kumsaidia. Akajikaza na kuendelea kuvuta hadi sigara ikaisha, kilichomsikitisha ni kutokusikia mabadiliko yoyote, na hivyo kujua kuwa katapeliwa kauziwa mchicha. Haraka akaanza kulalamika kwa wote waliokuwepo pale, “Unajua jamaa kaniuzia mchicha? Unajua nimeuziwa mchicha?” Kila mtu akaanza kumuangalia kwa makini na kumshangaa kuhusu mada hiyo mpaya ambayio aliianza ghafla. Jamaa yangu akaingia studio na kukuta kazi ya kurekodi inaendelea, bila wasi wasi akamtaarifu producer tatizo lake. “Producer subiri kwanza unajua jamaa kaniuzia mchicha shilingi alfu mbili” Producer akabaki anashangaa na kumshauri jamaa atoke nje ya studio. Jamaa yangu huku akishangaa kwanini watu hawamuelewi kuwa alitegemea kauziwa kitu cha kumpa stimu badala yake kauziwa mchicha.  Rafiki zake waliomkaribisha studio wakamfuata na kujaribu kuelewa nini kinaendelea. Ndipo akawapa mkasa mzima na kuwaeleza jinsi alivyotapeliwa kwa kuuziwa mchicha kidogo kwa shilingi alfu mbili. Hapo ndipo wenzie wote wakajua kuwa mwenzao akili si yake. Wakamshauri apumzike kwenye kochi aondoe uchovu..  Jamaa yangu akawa anasikia sauti kichwani mwake ikimwambia vua nguo  kabla hujalala kwenye kochi maana kuna joto. Hapo akaomba ushauri kwa wenzie avue au asivue. Zogo kubwa likaanza studio, jamaa yangu akisisitiza kuwa lazima avue nguo ili aweze kulala kwa amani kwenye kochi. Hapo kazi ikawa kuwaza namna ya kumsaidia jamaa akili imrudie, wengine wakasema apewe maziwa wengine amwagiwe maji, wengine wakidai awekwe chini ya feni, mwenye aking’ang’ania kuvua nguo.  Ghafla akaanza kudai moyo unataka kutoka, akawa ajiziba mdomo akidai moyo unataka kutokea mdomoni, na akaatimua mbio masupastaa kadhaa wakimfukuza. Jamaa akaaingia hoteli ya jirani na kuomba maji maana moyo unataka kumtoka. Hatimae alikamatwa na wenzie kumrudisha kwao ambako alikimbilia kwa baba yake na kushtaki kuwa kauziwa machicha  wa shilingi alfu mbili na tapeli.

19 March 2016

BOSI UNAJISIKIAJE SASA

Kajamaa ambako hakajawahi kusafiri kwa boti kalilazimika kwenda na boti Zanzibar. Kakaa kwenye kiti karibu na dirisha, kabla safari haijaanza, bonge mmoja akaja kukaa pembeni ya kale kajamaa. Safari ikaanza, haukuchukua mda mrefu Bonge akawa anakoroma. Kamjamaa si kakaanza kusikia kichefuchefu, kakawa kanaogopa kumwamsha Bonge ili kapite kakatapike chooni, na kumruka Bonge pia kakawa hakawezi. Kakajitahidi kujikaza lakini bahati mbaya boti ikarushwa na wimbi kakashindwa kujizuia kakaachia tena kakamtapikia Bonge kifuani. Bonge akstuka akaamka akakuta matapishi kwenye shati na suruali yake, wakati Bonge bado anashangaa, Kamjaa kakawahi;
KAMJAMAA: Pole, vipi unajisikiaje sasa?

BARA SIRUDI TENA YAKHEEEE

Rafiki yangu Mwinchumu, mkazi wa Dole, hukooo Zanzibar alinikaribisha nikamtembelee Zanzibar, mwenyewe alinipa sifa hizi za Zanzibar, 'Njoo yakhe ubabadili upepo, ule urojo, usikilize taarab asili'.  Nami hili nililipokea kwa furaha kubwa, we fikiria mtu kutoka Iringa kuvuka bahari mpaka Zanzibar, mbona ningerudi Iringa wangenikoma. Nikingia kilabuni watu wangekuwa wananong’onezana, ‘Aise huyo jamaa aliwahi kwenda Zanzibar, hebu mpeni kisado cha ulanzi atuhadithie kukoje huko’, nina uhakika ile ningerudi tu ningepata hata mke. Si mchezo waif angekuwa anajisifu kisimani.’Mume wangu aliwahi kwendaga Zanzibar”. Kijijini kwetu hawana dogo wangetunga hata wimbo. Maana kuna jamaa kijiji cha jirani aliwahi kuwa na ndugu yake aliyepanda ndege basi akatungungiwa wimbo, 'Wagendye mwindege salama', yaani ulisafiri na ndege ukarudi salama,
Hatimae siku ilifika nikawa nimeshafika bandarini tiketi mkononi nikaingia kwenye meli, sijui kwanini rafiki yangu Mwinchumu alikuwa anaiita hii meli ‘chombo’, kwetu chombo ni bakuli na sahani. Basi nikaingia kwenye chombo. Kulikuwa na viti vingi, maTV kila upande yanaonyesha masinema, nikatafuta kiti nikakaa, pembeni nikaona kagrosari nikaenda na kununua juis ya mapera na sambusa kumi. Unajua kwetu mapera ni kitu unaanza kula toka una umri wa miaka miwili, hivyo juis yake inanikumbusha mbali sana, halafu nilikuwa na hamu sana na sambusa. Nikarudi kwenye kiti changu na kuanza kula na kunywa kwa furaha. Chombo kikaanza safari, nikaanza kuiona Darisalama hiyooo inapotea taratibu. Mara akapita mhudumu akatugawia mifuko ya rambo, sikutaka kuonekana mshamba na mimi nikapokea na kuuhifadhi nikajua lazima hawa jamaa wakati wa safari watagawa korosho au karanga au pengine hata sambusa, hivyo wanagawa mifuko kwanza.
Kausingizi lazima kalinichukua, maana ghafla nikashtuka, yaani fujo, tulikuwa tunarushwa mara tunashushwa, kuagalia nje, mawimbi makubwa yalikuwa yanakiyumbisha chombo. Nikajua ndio tunazama, macho yakanitoka, nikajizuia kupiga kelele. Nikaanza kujisikia hovyovyo, yaani tumbo likawa kama linapigwa ngumi. Nikawa naona kizunguzungu cha ajabu, nikawa naanza kusikia kichefuchefu, boti inarukaruka huko na kule, nikawa nimejishikilia kwenye kiti kwa nguvu. Nilifunga macho tabu, nilifungua macho shida, cha ajabu niliona mama mmoja anamnywesha juis mwanae, nao hawana wasiwasi kabisaaa, nini kilikuwa kikinitokea mimi? Pembeni kule nikaona mtu mmoja anatapikia kwenye mfuko ya Rambo, hapo ndipo nikagundua kazi ya ile mifuko niliogawiwa. Kwa kweli nilikuwa najua sasa nafia baharini, yaani Mnyalu nafia kwenye maji? Halafu hata kuoa sijaoa.  Chombo kilivyokuwa kinarushwa kama karatasi, na nilivyokuwa najisikia nilianza kukumbuka sala zote na matambiko yote ya kikwetu. Nilichukua mfuko wangu wa Rambo, nikatapika juis ya mapera na sambusa zote kumi na chai niliyokunywa asubuhi hata ugali wa jana nao ulitoka, ukawa utumbo nao unataka kutoka. Sikumbuki mengi ila nakumbuka kwa mbali nasikia watu wanasema tumefika Zanzibar, muhudumu mmoja akaninyanua na kuanza kunitoa nje, miguu ilikuwa inakataa kusimama, wakanitoa nje, nikakutana na Mwinchumu, nae kuniona eti kaanza kucheka,’ Yakhe vipi tena hahahaha? Mbona umelegea karibu Unguja yakhe’ Kwa kweli sikumjibu nilikuwa tayari naanza kufikiria kwa woga safari ya kurudi Iringa. Na kama mambo yenyewe yanakuwa kurudia yaliyonikuta leo, nikajikuta narudia tena na tena, ’Mwinchumu, Mwinchumuee mi Bara sirudi tena”

18 March 2016

ACHA MASWALI YA KIJINGA HAYO


MKE: Mbona unanukia pafyumu ya kike?
MUME: Yaa kuna mwanamke tulikuwa tumeminyana ndani ya daladala
MKE: Na lipstiki kwenye shati?
MUME: Tulikumbatiana na wageni toka Zambia walitembelea ofisi yetu
MKE: Na ile kondom iliyotumika kwenye mfuko wa suruali?
MUME: Bwana ee acha maswali ya kijinga mi nalala nina usingizi
MKE: Lazima niulize mie huwa nahakikisha nimeacha kila kitu hukohuko ndio narudi nyumbani
MUME: Umesema nini wewe?
MKE: Bwana ee acha maswali ya kijinga mi nalala nina usingizi

JINA LA PEDESHE SIRI SISEMI

Baada ya tetesi kufikia blog hii kuwa wadada wasanii wamekuwa na tabu kweli kuwataja  wapenzi wao kwa kuogopa kuibiwa , blog hii ilimtuma mwandishi wake mahiri akajaribu kupata ukweli kuhusu hili.
MWANDISHI: mambo sister
MDADA: Poa tu jamani nani mwenzangu?
MWANDISHI: (Akitoa kitambulisho chake ambacho sijui kapata wapi) Dada mimi ni muandishi wa lile gazeti mashuhuri la mtandaoni ambalo limeapa kusema ukweli daima kama inalipa. Niliomba nikuhoji, kwa kuwa gazeti letu linasomwa mpaka Ulaya , hii itakuwa promo sana kwako
MDADA: Ai weweeeee, ehe unataka kujua nini? Maana mie sijatoa muvi wala singo muda sasa
MWANDISHI: Kiukweli mimi nilikuja kujua kuhusu maisha yako, unajua nyie masupastaa, watu hutaka kujua maisha yenu, sasa tumeambiwa una jumba la kifahari kama la Rihanna tulipenda wafuasi wako wajue
MDADA: Is true. Nina nyumba ya kifahari hapo Tandale kwa Mtogole, ina choo cha kifahari, bafu la kifahari, sebule  na korido ya kifahari na jiko la kifahari. Kila chumba kina TV mbili na redio moja
MWANDISHI: Safi sana, sasa hii nyumba umepanga shilingi ngapi?
MDADA: Nyoooooooooo unaona shepu ya kupanga hii? Nimenunuliwa na bwanangu mpya. Tunaoana karibuni, harusi yetu itakuwa Palestina, tutasindikizwa na Mashauzi Classic Taarab
MWANDISHI: Ohh hongera sana. Umempa nini mpaka akakununulia nyumba hii?
MDADA: Unauliza makofi polisi hahahahaha
MWANDISHI: Okay. Nadhani wafuasi wako wangefurahi kumjua huyo anayemtunza supasta wao , unaweza kunambia jina lake?
MDADA: Hilo hapana haliwezekani
MWANDISHI: Kwanini? Mganga kakukataza?
MDADA: Oh no, mambo ya waganga baadae kidogo,  ila bwana huyu  nikimtaja tu wenzangu wataniibia
MWANDISHI: Hayo matusi sasa, ina maana kuwa wadada wa hapa mjini wezi namna hiyo?
MDADA: Habari ndio hiyo
MWANDISHI: Labda niulize kitu dada, huyo bwana wako zuzu kiasi gani hata akununulie nyumba halafu kesho aibiwe kama mzigo wa kuni?
MDADA: Wanawake hasa wasanii wabaya watamshawishi tu.
MWANDISHI: Kwa hiyo, usiri huu utaisha lini, maana akijulikana tu watu watachukua mzigo, hata kama mmeshaoana
MDADA: Bwana ee ngoja nikwambie ukweli, hii nyumba wanachangia pango wanaume wengi, sasa nikimtaja mmoja hao wengine itakuwaje si watakimbia? Kwa hiyo sisemi kitu ili kila mmoja kwa kuwa hawajijui anaona ye ndio mjanja
MWANDISHI: Okay sasa ninaanza kuelewa, Kumbe ndio staili yenyewe?
MDADA: Mjini hapa kaka ukiwa na bwana mmoja si atachoka kulipa bili
MWANDISHI: Okay mdada siri yenu simwambii mtu bye

SORRY NILIKUWA NAKUTANIA

MKAKA: Sweety mambo?
MDADA: Poa asante
MKAKA: Samahani dada, mimi ni kijana ambaye nimekuwa nikikufuatilia kwa muda sasa, na nimegundua wewe ni mtu ambaye ningependa uwe mke wangu niishi nawe milele, naomba nikuoe
MDADA: Haleluya, hatimae sala zangu zimejibu, nimepata taabu sana mimi kaka, nimedanganywa na wanaume wengi nikajitahidi kutumia waganga wengi ili nipate mume haikuwezekana, nikaamua kuokoka , nikafunga sana na kukesha sana na kutoa sadaka sana hakikutokea kitu, nikaamua kujiingiza hata katika klabu za mpira, mwaka mmoja nikawa Yanga mwingine nikawa simba, wapi sikupata mume wa kunioa, nikajikondesha niwe na shepu ya kimiss lakini bure, nikahama toka Moshi nikaenda Tanga na hatimae kuja kuja Dar haikusaidia, nikajiunga na facebook, twitter, instagram, whatsapp nikaanzisha mpaka blog ya kujieleza natafuta mume, sikupata mume  wa kunitamikia atanioa, nikajitahidi kuhudhuria maharusi mbalimbali bure, hatimae leo maombi yangu yamejibu, asante sana kaka niko tayari hata leo kufunga ndoa
MKAKA: Nakutaniaaaaaaaaa

ACHA KUNUNA, PESA ZITAANZA KUPATIKANA SOON


Devi kashtuka usingizini kauta gheto kwake wameingia wezi;
DEVI: Mnatafuta nini?
JAMBAZI: Tunatafuta pesa
DEVI: Aise ngoja niamke niwasaidie tukipata tugawane
********************************
GULO: Bebi simu yako nzuri umepata wapi?
DEVI: Nilishinda kwenye mashindano
GULO: Mashindano ya nini Bebi?
DEVI: Mashindano ya mbio, kati yangu, mwenye simu, polisi na wananchi wenye hasira kali.
***********************************
DOGO: Eti mama malaika huwa wanapaa?
MAMA: Ndio malaika wanapaa, kwanini unauliza?
DOGO:Baba alimuita dada Malaika, dada atapaa?
MAMA: Ndio atapaa leoleo kurudi kijijini kwao
********************************************
Mdada kasimamisha gari mataa ya Moroko, kijana mmoja akaja kumuomba msaada,
KIJANA: Nisaidie mama sijala toka jana
MDADA: Samahani sina kitu
KIJANA: Samahani unanikumbuka
MDADA: Hapana sijawahi kukuona kabla ya leo
KIJANA: Sema umenishahau, mi rafiki yako facebook

Imani zetu;
1. Mvua ikinyesha wakati jua linawaka……….simba anazaa
2. Ukinywa maji ya nazi……utapata busha
3. Mtu akikuruka…..utakuwa mfupi
4. Usiokote chakula kilichodondoka…..shetani amekila
5. Mtu akikuuma, pka mavi ya kuku alipokuuma…meno yake yataoza
6. Ukifagia usiku…unafagia bahati
7. Uking’oa jino tupia juu ya bati…kunguru wakichukua watakuletea jingine
8. Ukimpiga mbayuwayu na manati chanjia damu yake unakuwa na shabaha
9. Ukivaa kiatu kimoja…titi la mamako litavimba
10. Mtu akisimama nyuma yako wakati umekaa anakunyonya damu

10 March 2016

HII PANTONI YA KWENDA KIGAMBONI


Jamaa kamkuta mwanamke mmoja pale Ferry analia, 
JAMAA: Nini shida mama angu?
MDADA:Heri nife,maisha yamenishinda
MJAMAA: Huna haja ya kufa, sikiliza mimi ni baharia na meli yetu inaenda Ulaya leo, kama unataka ingia kwenye boksi nikakufiche stoo, meli ikitia nanga Ugiriki, nakutoa ukatafute maisha huko. Bibie akaona heri hilo akaingia kwenye boksi, jamaa akambeba na mdada akajikuta yuko kwenye stoo moja wapo katika meli, jamaa akawa anamletea chakula kila siku na mara nyingine yeye mwenyewe analala huko kwenye hako kastoo,kila mara akimhakikishia mdada kuwa wameshapita visiwa vya Komoro, siku nyingine akimwambia wako India. Zilipita wiki mbili ndipo yule mdada akagundulika na nahodha wa chombo hicho.
NAHODHA:We unafanya nini humu?
MDADA:Chonde naomba msinitupe baharini, nilindeni mkifika Ugiriki mnishushe
NAHODHA: Unajua mbona sikuelewi? Mdada akalazimika kumueleza nahodha ishu nzima.
NAHODHA:Dah wala usipate taabu sikutupi popote, ila jamaa yako kakudanganya hii si meli ya kwenda Ulaya ni pantoni ya kwenda Kigamboni, tukifika huko shuka