PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

SIINGII DISCO TENA


Yaliyonikuta Jumamosi iliyopita sitasahau, ila niseme tu siingii tena disco. Unajua enzi zetu disco lilikuwa raha sana, wakati huo wanamuziki waliokuwa wanatamba walikuwa Bonney M, ABBA, najua hamuwajui hao walikuwa wana vibao moto kama Chikitita na Bonononos vikipigwa hivyo tulikuwa tunajimwaga ukumbini kwa shangwe na hoyehoye, suruali zetu zilizokuwa zinabana kiunoni na huku chini zilikuwa pana, shati zimebana kifuani yaani tulikuwa wa kisasa kweli si mchezo. Tena nyie hamna jipya sisi tulikuwa tunabana shati ila suruali pana nyie mnabana suruali ila mashati mnavaa mapana. Haya nisiende huko, nirudi mambo yaliyonikuta Jumamosi. Huyu mjukuu wangu anaevaa suruali ikiwa inakaribia kuanguka muda wowote kanikaribisha kwenda nae Disco, nilimcheka na kumwambia mimi nimewahi kuwa mpiga disco enzi zangu sioni kuna jipya huko kwenye midisko toto. Akang’ang’ania “Babu njoo uone swaga za washaji”. Basi nikamkubalia ili nimtoe ushamba. Kwanza kitu cha ajabu akanambia tutaondoka nyumbani saa saba usiku, nikamwambia si ndio itakuwa karibu wanafunga disco, akajibu hapo ndio taim ya kuanza. Hatimae tukafika ukumbi wa disco, hapo nje nikakuta vibinti vimevaa nguo za kiajabu ajabu nikabaki kutoa macho tu. Mjukuu wangu akanishika mkono tukaelekea ndani. Kilichonishtua karibu nipate ugonjwa wa moyo, ni sauti, muziki ulikuwa juu, lile bezi nilikuwa nalisikia kama likitaka kunitoa roho, nikaanza kujivuta ili nikimbie nje, mjukuu wangu akanishika kwa nguvu na kunivutia ndani, huko ndani taa za rangi rangi zilinichanganya hata nikawa sioni nilikotoka wala ninakokwenda, baadae zikaja taa zikiwafanya watu kuonekana kama mashetani yanacheza, kama vile watu wanagandaganda, mapigo ya moyo yakaanza kupanda, moshi wa masigara yao waliyoyaweka kwenye chupa yakawa yananiziba pumzi, muziki unagonga kwenye tumbo, jasho likaanza kunitoka. Nikakuta mjukuu kanifikisha kwenye kochi, ‘ Babu unakunywa nini nikuletee?’ Sikuwa na hamu ya chochote nilikuwa nataka kurudi nyumbani tu, nilijua nikikaa hapa nusu saa nyingine nakufa. Nikalazimika kumwambia mjukuu wangu, “Nirudishe nyumbani nakufa sasa hivi”
“Lakini babu mi napafom sasa hivi subiri nikipafom ntakurudisha hom”. Kifupi sikumbuki mengi zaidi ya taa za marangirangi, na kelele nyingi na presha kupanda. Hatimae mjukuu akaja kunambia haya babu twende home leo hapa ilikuwa mzuka sana vipi uliufeel?” Asubuhi niliamka moyo bado unaenda mbio, nimeapa sitaenda tena disco

Comments