PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

JANUARI MBONA NDEFU HIVI?Hivi hii Januari inaisha lini? Kila kila mtu analalamika, kila mtu kanuna. Chakuchekesha kila mtu alikuwa anashangilia siku mwaka mpya ulipoingia,  ilikuwa kelele za furaha kila mtaa, watu walikula na kunywa  kila kona ulisikia watu wakisema, ‘ Mwaka mpyaa huoooo, asante Mungu nimeuona’. Ilikuwa chereko chereko, hata mama mwenye nyumba wangu alinikumbatia, Mangi nae alinitumia meseji ya kunitakia mwaka mpya, kwa kawaida mesej zake ananikumbusha anachonidai. Wengine tukawa tunatuma  ujumbe wa pongezi kwenye simu kwa wake zetu, wake zetu watarajiwa, wake maboresho, wake academia, michepuko, michepuko maboresho, michepuko academia, basi raha tupu. Tarehe moja januari ilikuwa kula kunywa kufurahia mwaka mpya. Furaha yote ilianza kuisha tarehe tano, mama mwenye nyumba kaanza kukumbushia kodi, meseji za Mangi zikaanza tena kukumbushia deni, mfukoni kweupeeeee. Kila unaemwendea analalamika, ‘Januari hii mwanangu sijui pesa imeenda wapi’. Hata yule ambae hujawahi kusikia ana mtoto Januari hii utasikia anaaza, ‘Nimebanwa watoto wanahitaji ada, madaftari, na yunifom sina kitu kabisaa’. Najua ilikuwa fiksi ada si imeondolewa, au jamaa anamsomesha mwanae praivet?
Jioni ikifika unajishauri jinsi ya kuingia kwenye chumba chako mwenyewe, ukifika mtaani unacheki kwanza mwenye nyumba yuko wapi. Unajua ikifika Januari wenye nyumba wanapenda sana kukaa karibu na mlango wa mbele na kusababisha ugumu wa mtu kuingia kwenye chumba chako.  Inalazimika kucheza mchezo wa paka na panya, akikosea akapotea kidogo unanyata na kuingia chumbani kwako, unaminya kimyaa. Hakuna kuwasha TV wala taa, unaingia kwenye shuka saa moja usiku ndo unalala hivyo hadi kesho yake. Huko nje unamsikia mama mwenye nyumba anauliza, ‘Huyu mshenzi hajarudi bado? Ngoja arudi leo atanijua mi nani? Hapo ukilala hujigeuzi zisije zikasikika chaga za kitanda ukashtukiwa. Simu unaweka kwenye ‘silent’, maana katika kipindi hiki kuna simu nyingi toka kwa wale uliowatakia heri ya mwaka mpya, mke maboresho ,mchepuko maboresho, mke academia na mchepuko academia, hapo ujue wanabip na kutuma mesej kila moja akikutaarifu kuwa ‘kaishiwa hatari’.
Panya wana tabia mbaya sana ya kuanza kusumbua kipindi hiki, utakuta panya kakupitia usoni na kwa kuwa ni kiza unaweza ukajikuta umepiga ukelele wa nguvu bila kujua.  Chezea Januari wewe…
John Kitime
0763722557

Comments