PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

Teh teh teh kwaheri 2015 karibu 2016


Kwanza nawatakieni wote heri kwa mwaka mpya 2016, hata wale waliomaliza mwaka kwa ‘kutumbuliwa majipu’. Unajua ni ngumu kidogo kuwaonea huruma kwa kuwa nimegundua kumbe ile barabara ya mtaani kwetu mliotusumbua kwa kuifunga miezi kadhaa kwa kisingizio cha kuitengeneza kumbe ilikuwa kanyaboya, yaani mtaa mzima mlitufanya  mafala, tukawa tunajisifu tuna barabara ya lami miezi mitatu tu baadae lami imefutika.
Nawatakia heri wanasiasa waliowini na wale ambao  hawakuwini, na wale wanaodhani waliwini lakini eti hawakuwini na wale waliowini lakini kikweli hawakuwini.
 Kila unapoanza mwaka lazima upime yaliyopita na ujipange kwa yajayo. Mimi pia nimeamua nijiwekee mikakati ya 2016 kwa kuangalia mpango kazi wa 2015.
1.     Mwaka 2015 nilipanga nipunguze kitambi. Hili nimeweza kutokana na mshkaji aliyekuwa akininunulia bia katumbuliwa jipu, bia za bure na mshkaki vimepotea ghafla. Na ujue huyu jamaa alikuwa kama benki yangu inayotembea, sasa ni full ukame. Kitambi kimepotea chenyewe.
2.     Nilipanga kuwa lazima 2015 nihakikishe kila mwezi naweka benki alfu 50. Hili limeshindikana, yaani nchi hii kwa mizinga dahh, ukipata hela utadhani wananusa, haipiti dakika kumi mesej zinaanza utasikia huyu anaomba vocha yule anaomba mchango wa luku, mwingine anakukumbusha ulisema utamnunulia simu. Wengine wanakumbusha michango ya harusi dahh. 2016 sitaki mchezo. Tunaomba kampuni za simu zizuie mesej za kuombana hela.
3.     Nilipanga lazima 2015 nioe demu wa Bongomuvi. We we we we, mwanzoni mwa mwaka ilikuwa kazi ngumu, toka majipu yametumbuliwa, inalazimika niwakimbie, kama sita hivi wanataka niwaoe. Hamnipatiiii, doli doliii
4.     Usafiri 2015 lazima. Imeshindikana na ni wazi 2016 ntaendelea kusota na daladala, hii ishu ya levo siti, ina maana japo ntakuwa siibiwi mara nyingi mwaka 2016.
5.     Nilipanga 2015 cheo lazima. Nilikosa mwaka huo, ni wazi kwa miaka mitano ijayo hakuna cheo cha kirahisirahisi, Kwanza hii spidi ya Hapakazi tu mi siwezi. Cheo nini bwana.
6.     2015 lazima nitoe singo. Kwani mimi nina nini na Diamond ana nini? Watu wenye roho mbaya walinilogwa 2015, lakini 2016 lazima nitoe singo kali yenye ujumbe mzito


Comments