PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

BABA MDOGO ANA VICHWA VIWILIKuzaliwa kijijini ni raha ya aina yake. Mimi nilizaliwa kijijini, nikakuwa mpaka nafikia miaka minne nilikuwa sijawahi kuona wala kusikia gari likipita kijijini kwetu. Kijijini kwetu ilikuwa raha tu inayoanza alfajiri. Saa  tisa usiku jogoo la kwanza likiwika, bibi alikuwa anaamka na kuwasha moto na kuanza kutayarisha chakula cha asubuhi, hapo atachemsha viazi vitamu, atapasha moto maharage ya jana, kama kapata sukari atapika na uji, ukiwa tayari anakuamsha ukanawe uso, na maji baridii, kisha unakuta chakula cha kueleweka, sio kimjini mjini eti kikombe cha chai ya rangi ndio mtu unatoka kuanza siku, hapana hapo unaanza siku na i viazi vitamu vilivyochemshwa au kuokwa kwenye majivu, maharage, uji wa sukari umetiwa ndimu, siku nyingine ugali kwa mboga ya majani au maziwa ya mgando ukimaliza hapo kitumbo ndii, mnasindikizana na bibi shambani, jua halijachomoza hapo bado giza la alfajiri. Ndege aina mbalimbali wanaimba, mnapita njia  nyembamba yenye umande kuelekea shambani. Ukifika shambani wewe kazi yako kupiga kelele kufukuza ndege wasile mazao wakati bibi analima au anapalilia. Hapo ndipo utakapojifunza kutumia manati kuwinda ndege. Ilieleweka kuwa ukiweza kumpiga mbayuwayu, unajichanja halafu unapaka damu yake basi unakuwa na shabaha sana maana kumpiga mbayuwayu si kazi rahisi, ndege huyu ni hodari sana kwa kukwepa.
Siku ambayo sitaisahau ni siku ya kwanza kuisikia na kuiona pikipiki. Tulikuwa tunatoka na bibi shambani, ghafla kwa mbali nikasikia sauti mpyaa, kama kitu kinachanika praaaaaaaaaaaa, nikamuangalia bibi kwa wasiwasi, sauti ikazidi kutukaribia, nikajishikilia kwa bibi. Hatimae kupitia kanjia kembamba kikatokea kitu chenye sauti ya kutisha na mtu mwenye kichwa kikubwa cha mviringo, kikasimama jirani yetu sauti ya ile niliyoisikia ilikuwa inatoka kwenye kitu hiki, kilikuwa kinatisha kweli, bila kujijua nilikwisha jikojolea kwa woga, mbaya zaidi si nikaona yule mtu anajinyofoa kichwa, nikajificha nyuma ya bibi. Bibi nikamsikia kwa furaha anataja jina la yule mtu, ambaye sasa alikuwa kazimisha ile kelele akaja akamkumbatia bibi wakaongea kwa furaha, cha kutisha ni kuwa alikuwa na vichwa viwili kimoja kikubwa cha mviringo kakishika mkononi. Bibi akanambia, “Msalimie baba yako mdogo”. Nilikuwa naogopa hata kumuangalia usoni, japo nilipojaribu kumuangalia nikaona ana sura ya upole, lakini kichwa alichokuwa kashika mkononi ndio kilikuwa kinanitisha. Bibi akasema twende nyumbani, baba mdogo akanambia twende wote nipande kile kitu cha kutisha, nilichomoka mbio na kuingia porini nikawahi nyumbani, tena nikaenda kujificha kwenye ghala la mahindi.
Muda si mrefu nikawasikia bibi na baba mdogo wamefika, nikachungulia kwenye katundu kadogo nikamwona baba mdogo kaegesha lile likitu lake lenye kelele, akaweka na kile kichwa chake juu ya lile likitu akapewa kiti akakaa. Bibi akaanza kuniita, nikalazimika kujitokeza, maana bibi alikuwa kikuita unaenda, kwani ukimkorofisha kipigo chake si kawaida. Bibi na baba mdogo wakawa wanajaribu kunitoa woga, baba mdogo akanipa pipi aliyoitoa kwenye koti lake, kidogo moyo ukatulia, lakini macho yangu kwenye lile lidude lenye kelele. Baba mdogo akanambia kwa upole, “Hiyo inaitwa pikipiki usiogope, inasidia kusafiri, unapanda kama punda”. Baba mdogo  alishinda siku nzima, ndio nikajua kumbe yeye anakaa mjini, akanambia iko siku atanipeleka mjini nikapaone kuna pikipiki nyingi sana. Miaka mingi sana imepita toka siku ile, nilikuja mjini nimekuwa dreva wa bodaboda maarufu, huwa nikikumbuka kuwa  siku ya kwanza kuiona pikipiki niliiogopa mpaka nikajikojolea huwa nacheka peke yangu, nacheka zaidi kila ninapovaa au kuvua helmet, nikikumbuka kuwa nilikuwa naona kama vile baba mdogo eti alikuwa na vichwa viwili.

Comments

Anonymous said…
Asanti Sana,nimekumbuka kwetu Kalenga