HATUPIMI BANDO

28 May 2015

BABA MDOGO ANA VICHWA VIWILIKuzaliwa kijijini ni raha ya aina yake. Mimi nilizaliwa kijijini, nikakuwa mpaka nafikia miaka minne nilikuwa sijawahi kuona wala kusikia gari likipita kijijini kwetu. Kijijini kwetu ilikuwa raha tu inayoanza alfajiri. Saa  tisa usiku jogoo la kwanza likiwika, bibi alikuwa anaamka na kuwasha moto na kuanza kutayarisha chakula cha asubuhi, hapo atachemsha viazi vitamu, atapasha moto maharage ya jana, kama kapata sukari atapika na uji, ukiwa tayari anakuamsha ukanawe uso, na maji baridii, kisha unakuta chakula cha kueleweka, sio kimjini mjini eti kikombe cha chai ya rangi ndio mtu unatoka kuanza siku, hapana hapo unaanza siku na i viazi vitamu vilivyochemshwa au kuokwa kwenye majivu, maharage, uji wa sukari umetiwa ndimu, siku nyingine ugali kwa mboga ya majani au maziwa ya mgando ukimaliza hapo kitumbo ndii, mnasindikizana na bibi shambani, jua halijachomoza hapo bado giza la alfajiri. Ndege aina mbalimbali wanaimba, mnapita njia  nyembamba yenye umande kuelekea shambani. Ukifika shambani wewe kazi yako kupiga kelele kufukuza ndege wasile mazao wakati bibi analima au anapalilia. Hapo ndipo utakapojifunza kutumia manati kuwinda ndege. Ilieleweka kuwa ukiweza kumpiga mbayuwayu, unajichanja halafu unapaka damu yake basi unakuwa na shabaha sana maana kumpiga mbayuwayu si kazi rahisi, ndege huyu ni hodari sana kwa kukwepa.
Siku ambayo sitaisahau ni siku ya kwanza kuisikia na kuiona pikipiki. Tulikuwa tunatoka na bibi shambani, ghafla kwa mbali nikasikia sauti mpyaa, kama kitu kinachanika praaaaaaaaaaaa, nikamuangalia bibi kwa wasiwasi, sauti ikazidi kutukaribia, nikajishikilia kwa bibi. Hatimae kupitia kanjia kembamba kikatokea kitu chenye sauti ya kutisha na mtu mwenye kichwa kikubwa cha mviringo, kikasimama jirani yetu sauti ya ile niliyoisikia ilikuwa inatoka kwenye kitu hiki, kilikuwa kinatisha kweli, bila kujijua nilikwisha jikojolea kwa woga, mbaya zaidi si nikaona yule mtu anajinyofoa kichwa, nikajificha nyuma ya bibi. Bibi nikamsikia kwa furaha anataja jina la yule mtu, ambaye sasa alikuwa kazimisha ile kelele akaja akamkumbatia bibi wakaongea kwa furaha, cha kutisha ni kuwa alikuwa na vichwa viwili kimoja kikubwa cha mviringo kakishika mkononi. Bibi akanambia, “Msalimie baba yako mdogo”. Nilikuwa naogopa hata kumuangalia usoni, japo nilipojaribu kumuangalia nikaona ana sura ya upole, lakini kichwa alichokuwa kashika mkononi ndio kilikuwa kinanitisha. Bibi akasema twende nyumbani, baba mdogo akanambia twende wote nipande kile kitu cha kutisha, nilichomoka mbio na kuingia porini nikawahi nyumbani, tena nikaenda kujificha kwenye ghala la mahindi.
Muda si mrefu nikawasikia bibi na baba mdogo wamefika, nikachungulia kwenye katundu kadogo nikamwona baba mdogo kaegesha lile likitu lake lenye kelele, akaweka na kile kichwa chake juu ya lile likitu akapewa kiti akakaa. Bibi akaanza kuniita, nikalazimika kujitokeza, maana bibi alikuwa kikuita unaenda, kwani ukimkorofisha kipigo chake si kawaida. Bibi na baba mdogo wakawa wanajaribu kunitoa woga, baba mdogo akanipa pipi aliyoitoa kwenye koti lake, kidogo moyo ukatulia, lakini macho yangu kwenye lile lidude lenye kelele. Baba mdogo akanambia kwa upole, “Hiyo inaitwa pikipiki usiogope, inasidia kusafiri, unapanda kama punda”. Baba mdogo  alishinda siku nzima, ndio nikajua kumbe yeye anakaa mjini, akanambia iko siku atanipeleka mjini nikapaone kuna pikipiki nyingi sana. Miaka mingi sana imepita toka siku ile, nilikuja mjini nimekuwa dreva wa bodaboda maarufu, huwa nikikumbuka kuwa  siku ya kwanza kuiona pikipiki niliiogopa mpaka nikajikojolea huwa nacheka peke yangu, nacheka zaidi kila ninapovaa au kuvua helmet, nikikumbuka kuwa nilikuwa naona kama vile baba mdogo eti alikuwa na vichwa viwili.

26 May 2015

CHEKIBOB KACHANIKA MAKALIO


Chekibob kaget krash kwenye mnuso akalewa njwiii, akaondoka huko na chupa nyingine za Nyagi kaweka mifuko ya nyuma ya KATA K yake. Sababu ya ulevi alipofika karibu na kwake akateleza akaangukia makalio chupa zikavunjika na kumchanachana makalio. Akajikongoja mpaka ndani kwakwe, alipovua suruali akaamua kujitibu kwa kubadika plasta kwenye vidonda, basi kwa msaada wa kioo cha kabati lake akawa anajiaangalia palipo na kidonda na anabandika plasta. Hatimae akaona amefanya kazi nzuri akajitosa akalala...... Asubuhi alipoamka, akashangaa kioo chote kimebadikwa plasta na makalio yanauma

14 May 2015

HIVI WEWE NI RAFIKI WA AINA GANI?


Ukipenda usipende rafiki zako wamekuweka katika kundi fulani, unaweza kuwa na mtu ambaye rafiki zako wanakukumbuka kila mara kwa kukutakia mema, au unaweza kuwa aina ya rafiki ambaye rafiki zako wakikuona tu wanaanza kukutukana na kukulaani. Sasa wewe unajijua rafiki zako wamekuweka kundi gani? Inawezekana wewe ni aina ya rafiki ambaye unakumbukwa tu kama kukiwa na mnuso au watu wanataka kutoka out,  hasa kama una pesa au gari, lakini kama hakuna ishu hakuna anayekutafuta. Au wewe ni aina ya rafiki ambaye watu wakiishiwa ndio wanakukumbuka? Maana unauwezo wa kumkopesha mtu hata akipiga simu saa nane za usiku, bila matatizo unamtumia  hela tu, halafu uzuri wake wew huwa hudai kiviiile. Halafu kizuri  zaidi siku za sikukuu unawakaribisha wote unaowadai kwa bonge ya mnuso, tena kiroho safi. Au wewe ni yule rafiki ambaye akiombwa mchango, hata ile michango ya kiajabu ya kisiku hizi inayosema mchango si chini ya laki we unatuma tu, halafu kwenda shughuli huendi? Au wewe ndio wale marafiki ambao kamwe hawachangii mchango wowote, hata kama unamsaidia? Au wewe ndie aina ya rafiki ambaye ukisikia mwenzio anashida lazima uhangaike kumsaidia, hata kama ukisikia yuko gerezani Uchina utaenda tu kujaribu kumtoa? Yaani aina ya wale tunaowaita marafiki wa ukweli? Tatizo ni kuwa marafiki wa dizaini hii wako wachache sana. Au wewe ndio wale marafiki ambao hawana doa, wana kazi nzuri, nyumba nzuri, wanavaa vizuri, wana stori nzuri, wana roho nzuri, yaani mpaka wenzio wanataka kuwa karibu na wewe kila mara? Au wewe ndiye yule rafiki ambae wenzako wanakufanya kichwa cha habari kila wakikutana? Kazi yao kukuongelea wewe tu na vituko vyako, ukitokeza tu wanaanza kukuchekea na kukukaribisha, ukigeuka tu stori ni kuhusu wewe, ulivyofumaniwa huku, ulivyoiba kule, ulivyofukuzwa kazi mwaka juzi, yaani wewe ndie chachu ya mazungumzo? Au wewe ndie yule rafiki anaedai anamjua kila mtu? Ukiulizwa kuhusu Ikulu, kuna mtu unamjua, TRA kuna mtu unajua, msikitini  kuna mtu unamjua, kanisani kuna mtu unamjua, Bongomuvi kuna mtu unamjua, Bongoflava kuna mtu unamjua na wote hao unadai unawajua kiundani, au wajomba zako au unawadai? Au wewe ndie aina ya rafiki ambae unajua mambo yote kuhusu rafiki zako? Majina ya wake zao, waume zao tarehe zao za bethdei, maduka wanayonunua nguo, pafyumu wanazotumia, hata dawa walizokunywa walipougua mara ya mwisho? Au wewe ndie aina ya rafiki watu wenzio wakikuona mapema wanakukwepa maana huna siri kila unalosikia na kuona haraka sana unalisambaza? Na kwa siku hizi za mitandao ya kijamii watu wanakukwepa kama ukoma. Au wewe ni aina ya rafiki ambaye ukimuona rafiki yako yoyote lazima umpige mzinga, hata kama umeshinda mamilioni ya Zembwela jana yake tu? Maana kuna wengine hawaombi kwa kuwa wanashida laa wanaomba kwa kuwa wamezoea kuomba, hata kama mfukoni ana alfu kumi akikuona mkononi una shilingi mia mbili, ataomba mgawane. Haya wewe ni rafiki aina gani?
Tukutane www.johnkitime.co.tz