HATUPIMI BANDO

14 March 2015

ENGLISH MEDIUM MPAKA NGOMA ZA KIASILI ZINACHEZWA KIZUNGU


Yamenikuta  makubwa tena ya kujitakia, hilo lazima nikubali. Unajua nilikuwa naona wivu sana nikiwatembelea rafiki zangu na kukuta wana watoto tena wadogo hawajaanza hata darasa la kwanza, wanaongea kingleza utadhani ndio wametoka Uingereza jana. Halafu kilichokuwa kinanipa wivu zaidi ni kuwa hawa rafiki zangu wengi tumetoka kijiji kimoja nawajua mpaka wazazi wao, na najua kwenye ukoo wao hakuna anaejua kingleza kabisaaa. Kimoyomoyo nikawa najisemea nikipata mtoto lazima na mimi nihakikishe anajua kingleza bado mdogo, kuwaringishia ndugu zangu. Hasa kuna kakangu flani anaringia sana hela zake, ningekuwa Jumapili asubuhi najidai namtembelea halafu nakaachia katoto kangu kawe kanaongea kizungu mbele yake, hiyo lazima itamchanganya maana hajui hata neno moja la kizungu hahaha, we ngoja tu. Mungu si Masanja, mke wangu akazaa katoto ka kike, kila siku nikawa nakangoja kakuwe kaanze nasari.
Nikaulizia kwa jamaa nasari gani inafundisha vizuri Kingleza, nikaambiwa Fudenge Intaneshno Nasari Skul ni kiboko, mwenyewe nikaenda kuiona kwa kweli nilifurahi, mabembea, walimu wanaongea kingleza tu, vyoo visafi vina malumalu, vitabu vyenye picha za watoto wa kizungu, yaani kila kitu kama Ulaya. Hatimae mwanangu akaanza shule. Ada ya mwezi ilikuwa kubwa kuliko kipato changu cha mwezi, lakini ilikuwa lazima nistrago ili na mtoto wangu ajue Kingleza. Wala haikupita wiki mtoto akaanza kuongea Kingleza na kuanza kutuchanganya mimi na mama yake maana tukawa mara nyingi hatumuelewi, tunaishia kusema ‘Yes’  kila akisema neno la Kingleza. Yaani hata kulia mtoto akawa analia kizungu, ‘No mother no, giv ais krim’                         hata sijui alikuwa anataka nini , basi atalia hapo mpaka labda tumpe biskuti au soda ndio ana nyamaza.
Walimu walituletea barua inayoelekeza vyakula muhimu kwa mtoto, vyote vya kizungu, milk, juice, hamburger, sausages, na eggs hivyo lazima mtoto ale kwa makuzi mazuri ya kizungu, na mtoto alikuwa anaalia sana akiamka na kukuta chai kwa maandazi asubuhi. Pamoja na joto la jiji letu hili la Dar es Salaam niliambiwa nimnunulie sweta ambazo zinauzwa shuleni kwa laki mbili na tai mbili za kubadili kila wiki, pia atafutiwe begi la mgongoni la kubebea vitabu, tena sio mtumba linatakiwa litoke dukani, kuna duka la watoto wa wenye hela na  mabegi yanauzwa hapo, na sisi tukaelekezwa huko. Kiukweli hela yote niliyokuwa napata huku na kule iliishia kwenye matumizi ya shule ya mtoto. Kiingeleza kilikuwa kinaongezeaka kila siku, hata akicheza na watoto wenzie yeye ni kiingleza tu, kimoyomoyo nilikuwa najisifu sana kwa kweli.
Hatimae tukaambiwa tunakaribishwa kwenye siku ya wazazi, nikaazima suti na mke wangu akavaa bonge la kitenge na kofia kubwa kama ya mama mchungaji, tukaenda shule, kwenye siku ya wazazi.
Tukonyeshwa pa kukaa shamra shamra zikaanza, kama kawaida ya kwetu hotuba ndefu zikatolewa na na Mkurugenzi wa nasari, mwalimu mkuu wa nasari, mwalimu wa darasa la nasari, muwakilishi wa wazazi wa nasari, hatimae mgeni wa heshima ambaye najua watoto walikuwa hawana hata habari nae akaongea nao na kuwaasa wasome waje kuwa viongozi wa kesho. Yakaanza maonyesho ya watoto, watoto wakawa wanatoka mmoja mmoja na kuonyesha jinsi wanavyojua Kingleza. Hatimae tukaambiwa watoto sasa watakuja kucheza ngoma ya kiasili. Si ndio vitoto vyote vikaja mbele yetu kiunoni vimejifunga kanga, Dj akaanzisha wimbo wa Kinaijeria ‘Chop my mani, chop my mani’ vitoto vikaanza kukatika kiuno, mzazi mmoja akainuka kumtuza mwanae na mimi nikaenda kumtuza   wangu. Kwa kweli hii shule kiboko inafundisha kiingereza kila kitu mpaka ngoma za kiasili wanacheza nyimbo za kiingereza.                                                                             

No comments: