MAAZIMIO YA MUZEE WA CHEKA NA KITIME 2015


Kwanza nawatakieni tena wote heri kwa mwaka mpya 2015, hata wale walioanza mwaka kwa ‘kuwekwa kiporo’, waliofukuzwa kazi na bosi, waliogawana ule mkwanja, waliokosa ule mkwanja, wanaolalamika kwa kuwa walikosa ule mkwanja, wanaolalamika kwa kuwa wanaona wananchi waliukosa ule mkwanja, wanaolalamika kuhusu ule mkwanja kusudi wapate mkwanja, wanaolalamika kwanini watu wanalalamika kuhusu ule mkwanja, wanaolalamika kuwa watu wasilalamike kuhusu ule mkwanja, na Taifa lote kwa ujumla, bila kuniacha mimi mwenyewe au vipi??
 Kila unapoanza mwaka lazima upime yaliyopita na ujipange kwa yajayo. Mimi pia nimeamua nijiwekee mikakati ya 2015.
1.     Lazima 2015 nipunguze kitambi. Wiki hii nimeshachelewa lakini kuanzia wiki ijayo ntakuwa naamka kila siku saa kumi na moja naanza jogging na mazoezi ya kuruka kichurachura kuzunguka uwanja wa mpira hapo mtaa wa pili, mwaka huu sitanii lazima kitambia kiende.
2.     Lazima 2015 nihakikishe kila mwezi naweka benki alfu 50. Yaani sitaki mchezo hii habari ya kufikia Januari nahaha kutafuta ada ya shule ya watoto, huku mama mwenye nyumba kanikalia kooni kama mie sio mtoto wa mwanamke mwenzie lazima iishe, yaani hata kama nikipata mchepuko mpya nakomaa nauambia laiv ‘Mi sina pesa’. Au ukiomba vocha najibu’ Mi sio wakala’  Kikubwa ni kula jiwe
3.     Lazima 2015 nioe demu wa Bongomuvi. Kwani wengine wana nini? Ujue watu huwa wanakosea sana, wanadhani eti hela ndio itasaidia, hapana hawa wadada ni binadamu kama sisi, hivyo ukimlilia hali na kumwambia huna hela lakini unampenda atakuelewa tu. Maisha ya ndoa muhimu mapenzi. Na wengi wamesha sema wanatafuta watu wa kuwazalisha, mimi ni dume la mbegu, ulizia kijijini kwetu usikie sifa za ukoo wetu. Kila mtu ana watoto nane au tisa. Kwa hiyo mwaka huu ndugu zangu tegemeeni ndoa yangu na supasta, nipeni wiki mbili nijue yupi nimuibukie. Nitatumia staili ya ana ana ana doo, kachanika pasto, isplingi matingoo, kumchagua anaefaa
4.     Usafiri 2015 lazima. Sina makuu hata kagari hata kadogo tu kama hutu tuvitz katanitosha, unajua ukoo wetu hakuna aliyewahi kuwa na gari lake, unajua jinsi Waafrika tulivyo na roho mbaya unaweza kukuta kuna kazee pale kijijini kaliloga ukoo wetu tusipate gari, ntajitahidi kuhudhuria kwa yule Mzee anae onekanaga kwenye TV anahubiri halafu watu wanamtuza kama muimba taarab, nasikia ukienda kule mara mbili tatu mikosi yote inayeyuka unapata Kivitz chako kiulaini.
5.     2015 cheo lazima. Nilichelewa kugombea uenyekiti serikali za mtaa maana, nilipotaka kujiunga na chama hiki wapambe wakaniambia huko utashindwa, nikataka kwenda chama kile wakaniambia huko ndiko kabisa hakuna mvuto utashindwa, nikachelewa kujiandikisha, sasa najipa muda mpaka mwezi wanne ntakuwa nimepima maji chama gani kitashinda basi najitosa huko kugombea Ubunge. Ndugu zangu niombeeni, nikipata Ubunge matatizo yetu yote yameisha, na mimi si mnajua ni matirio kabisa ya kuweza kuwa Waziri, tukifika Uwaziri hapo ni funga kazi
6.     2015 lazima nitoe singo. Kwani mimi nina nini na Diamond ana nini? Nikitoa Singo moja tu hayo yote hapo juu nimesov. Kasoro lile la kitambi lakini ukiwa na singo unatengeneza kundi la madansa unafanya nao mazoezi mpaka kitambi chote kinayeyuka si ndio. Singo iki hiti, Ubunge unakuwa rahisi kabisa, wananchi wanapenda sana wasanii.
7.      Mwaka huu pombe basi. Nitajitahidi ingawaje kimsingi bado sijaona sababu kwanini niache pombe, kwa mwaka huu mara mbili tu ndio nimeangusha gari baa. Sasa  mtu nakunywa kila siku mwaka mzima halafu bahati mbaya mara mbili tu nimeangusha gari sio mbaya maana kuna watu wanaangusha deile. Kwa hiyo tuseme ntapunguza pombe.


No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.