HATUPIMI BANDO

14 August 2014

WAKUBWA WAZIMA MNAAMINI MAZIMWI


Mheshimiwa mmoja baada ya kupata cheo si akapewa nyumba mitaa ya watu wenye pesa, akahamia huko akiwa na mke na mwanae. Siku moja mwanae aliyekuwa kazoea maisha ya Uswazi akawa anawinda ndege na manati kwenye uwanja wa jumba lao, bahati mbaya jiwe likapitiliza na kwenda kuvunja kioo cha nyumba ya jirani. Mheshimiwa na mkewe wakaamua kumfuata mwenye nyumba wakamuombe msamaha. Walipogonga mlango akafukua mbaba mmoja akawakaribisha kwa heshima, wakaingia na kuanza kujieleza. ‘Samahani sie tumehamia karibuni hapo nyumba ya pili, mwanetu kavunja kioo chako kwa bahati mbaya, tumekuja kuomba msamaha na kuona kama tunaweza kutengeneza’. Mwenyeji wao akawaomba wakae  kisha akawaambia, ‘Naomba niwahadithie kitu. Kwanza mimi nawashukuru nyinyi na mtoto wenu. Mwenye nyumba hii ni mchawi mkubwa sana, mimi ni ZIMWI alikuwa amenifungiwa kwa zaidi ya miaka 200 kwenye kichupa ambacho kilikuwa kwenye  dirisha lililovunjwa na chupa nayo ikavunjika nami nimekuwa huru, kwa hiyo kwa shukurani ombeni chochote mtakacho nitawapa, nina uwezo huo’ Hapo hapo muheshimiwa akauliza tena,’Yaani kitu chochote?’ Akajibiwa ‘Ndio’. Basi pale pale akasema, ’ Mimi naomba niwe bilionea mpaka nife’ Akajibiwa ,’ Hilo jambo dogo sana kwangu, umepata na kesho utaamka tajiri’ Mama nae akaomba vyake, ‘Mi nataka niwe na nyumba kila nchi duniani na niwe na biashara Dubai na China na HongKong’ Akajibiwa, ‘Umepata mama, kuanzia kesho hayo ni yako. Mimi nawashukuru kwa uhuru wangu lakini nina kaombi kadogo’. Mheshimiwa haraka akajibu, ’Sema tu wewe ni kama ndugu yetu sasa’ Basi ZIMWI likasema, ‘Naomba mkeo abaki hapa kama masaa mawili tu, unajua kifungo nilichofungwa kilinizuia kila kitu, hata mke sijapata kipindi chote hicho. Nikimaliza tu hilo ntaondoka kurudi kwetu Uzimwini hamtaniona tena, itakuwa siri yetu’. Mme na mke wakajadiliana wakaona utajiri waliopata ni mkubwa sana, na hilo jambo ni dogo sana la mara moja tu tena kwa siri, wakakubali sharti. Mke akabaki pale kwa masaa kadhaa.  Shughuli ilipokwisha, mama wa watu akiwa anajitayarisha kurudi kwa mumewe kichwani akiwaza utajiri, ZIMWI likakohoa kidogo na kumuuliza yule mama, ‘Samahani una miaka mingapi na mumeo ana miaka mingapi?” Mama wa watu akajibu, ‘Mie nina miaka 40 mume wangu ana miaka 46’ Yule Mbaba akacheka sanaa, ‘Sasa nyinyi wakubwa wazima mpaka leo mnaamini stori za MAZIMWI?

No comments: