PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

MJINI CHA BURE SALAMU TU


Yamenikuta, yamenikuta, nani anaukumbuka wimbo wenye maneno hayo? Basi yamenikuta. Nimeingia salun kutengeneza nywele zangu, si unajua kuweka bleki, mvi zimezidi mno naonekana si mkazi wa hapa mjini. Basi nimeingia saluni, kwanza mambo sio kama enzi zilee, nimepokelewa na wadada wawili wamevaa suruali zimebana hao, sijui walizivaaje, masikioni wanahedfon  mdoni chingam, ‘Karibu mzee, karibu kiti’ Haya mapya, enzi zile vinyozi wote walikuwa wababa tu hukuti mdada kwa kinyozi, kwanza tulikuwa hatusemi tunaenda saluni, tulikuwa tunaenda kwa kinyozi; bei zimeandikwa, kwenye kibao wazii, kunyoa kipara  500/-. Amigo 700/-, Madilu 800/-  Sasa mambo tofauti kabisa, saluni ina TV, muziki toka kwenye sabufa, wadada kibao, viti vya makochi dah. Haya nikakaa kwenye kochi la kifahari, mdada mwenye suruali imebana akaja, ‘Unanyoa nywele?” Nikasema hapana napaka rangi tu.  Kanishikashika kichwa na masikio akanambia , ingekuwa vizuri upunguze kidogo ndio rangi itapendeza, mtu ukishikwa masikio akili inasimama, bila kufikiri nikajibu ndio. Akaitwa mkaka mmoja akachukua mashine na kuanza kupunguza nywele zangu, nae akauliza, ‘Vipi mustach? Itafaa upunguzwe kidogo’ Nikajibu sawa na kwa kweli niliwasifu hawa vijana wanajali mteja. Baada ya
mkaka kupunguza nywele na mustachi, akaja mdada mwingine nae kavaa kisuruali cha kubana, mkononi kashika kibakuli cha rangi ya nywele, akaanza taratibu kunipaka kwa uangalifu sana, huku ananiongelesha kwa sauti yenye mvuto, vipi skrab? Nikamuuliza ndo nini? Akanambia ni kusafisha uso, na itakuwa vizuri kama nifanye na skrab maana ntapendeza, tena akausifu uso wangu kuwa hauna vichunusi, nikakubali skrab , ilikuwa pia nataka kujua ndio nini. Nikaambiwa nihamie kwenye chumba kingine kuoshwa nywele, kule nikakuta mdada mwingine kanambia nivue shati, nywele zikaoshwa vizuri, wakawa wadada wawili mwingine kaanza kunipaka mafuta ya nywele kisha nikaanza kusafishwa uso na maji ya moto, ikaanza hiyo skrabu. Nikaanza kufikiria kuwa nilitoka kwangu kuja hapa kupaka rangi nywele tu, hawa watoto wamenipenda wamenipunguza nywele na mustach, wamenifanyia skrab, hapa ndio pa kuja kila wikiendi. Hatimae nikaambiwa tayari, nilipojiangalia kwenye kioo nimekuwa mpyaaa, nikauliza bei, naambia alfu ishirini na tano, akili ika simama kwa sekunde, kidogo nizimie. Nikaja juu, ‘Kupaka rangi nywele shilingi alfu ishirini na tano toka lini?” Mzee si umenyoa nywele, mustach, umefanya scrab, umesema tukupake mafuta yale expensive jumla ndio hiyo mzee. Mfukoni nilikuwa na hizo hizo ambazo zilikuwa bajeti ya usafiri wa kwenda kazini wiki nzima. Nikazitoa na kukumbuka neno nililiona limeandikwa kwenye gari fulani….Mjini cha bure salamu tu

Comments