MAKENIKA WA GEREJI ZA BONGO

Ukiwa fundi magari hapa Bongo kuna mambo ambayo ni muhimu uyafuate ili uweze kupata fedha za kueleweka na maisha ya raha. Jambo la kwanza ni muhimu uwe unaonekana mchafumchafu. Fundi gani msafi? Ni muhimu pia ukiletewa gari kutengeneza hakikisha linatoka na alama kibao za grisi kila mahala, kwenye viti kwenye steringi, kwenye vioo, hiyo ndio itakuwa alama muhimu kwa mwenye gari kuwa kweli ulikuwa unashughulikia gari lake. Kitu kikubwa na muhimu kama makanika uwe unapendelea zaidi wateja wanawake, ila sio wale ambao ukiwa unatengeneza gari nae anashinda hapohapo gereji, anakufwata mpaka duka unalonunua spea hapana hao ni sumu katika kazi, na muhimu kuwakwepa kama mtu anae kudai. Wateja safi ni wale akina mama wanaokupigia simu na kukwambia “Njoo nyumbani uchukue gari linasumbua kweli sijui ni  nini’  na ukienda kuchukua gari swali lao moja tu, ‘Sasa itakuwa shilingi ngapi?” Hapo inakuwa wewe tu na akili yako, unatunga spea za uongo na magonjwa ya uwongo na bei za uwongo, usijisikie vibaya sana, maana unampa sevis ya kuchukua gari toka kwake, hahangaiki chochote na likiwa tayari unamrudishia, sawa tu na tofauti ya bei ya soda kati ya dukani ambako unalazimika kufwata mwenyewe utanunua shilingi mia 800/- bila glasi na ukienda hoteli za kitalii unaletewa soda kwenye glasi iliyochemshwa na mhudumu aliyevaa yunifom ya kitenge, huku ukiwa unapulizwa na kiyoyozi kikisindikizana na muziki wa kizungu kwa mbali, pembeni yako unakaa na wazungu laiv, na soda inakuwa shilingi 3000/-. Watu wakikusema vibaya Mungu atawahukumu. Achana na wajuaji, wale wanaokuja gereji eti uwafanyie sevis gari wakiwa wamekuja na kila kitu wameshanunua, mtu anakuja na oil, filta yaani kwa kweli wanakupotezea muda tu hao. Kuna wale watu ambao huwa wanajali sana magari yao, hawa mara nyingi bahili sana, hivyo akija siku ya kwanza ukaona anafuatilia kila unapogusa, tena anakushauri kabisa utasikia,'Hapo inafaa spana namba kumi', mtu kama huyu we mvumilie tengeneza tu gari kisha ingia uvunguni mwa gari na umwambie kama rafiki, ‘Mzee nadhani huku chini dampa imekaribia kwisha , ila usipate tabu inaweza ikafanya kazi miezi miwili mitatu haina haraka’, lakini wakati uko huko chini legeza nati moja au mbili, hili litasaidia kumfanya arudi mara akisikia kuna kitu kinagonga na atakuona wewe bonge ya makanika , kama gari litamharibikia  njiani bora zaidi maana atakuita na wewe utamkumbusha kuwa ulishamtaarifu kuhusu ugonjwa huo, hapo utakula hela yake kiulainiii. Ukimaliza kutengenza gari, lakini jioni na wewe unakideti na demu mpya, ambaye anahitaji usafiri wa kwenda kupeleka vitu kwa mama yake Kisarawe, hakikisha unafanya chini juu gari moja lisirudi kwa mwenyewe. Ni kweli atalalamika lakini  we mwambie kuwa we hupendi kazi za haraka haraka na kwa manufaa yake, lazima utaeleweka. Hasa ukimwambia umeona ni muhimu kucheki kama kwenye injin maunting kuna oil ya kutosha, tena utafanya bure. Ila hakikisha gari haipati mikwaruzo na usisahau kinga chini ya kiti cha gari….tutaendelea


No comments:

Post Top Ad

Powered by Blogger.