PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAUFUNGA MDOMOWANGU

NAUFUNGA MDOMOWANGU
NAUFUNGA MDOMO WANGU

Kwako Mzee wa Cheka na Kitime


Kwako Mzee wa Cheka na Kitime,
Dar es Salaam.
Salaam nyingi zikufikie popote ulipo, sisi huku ni wazima kabisa. Nimekuwa nikisoma makala zako na kugundua kuwa wewe ni mtu mwenye busara sana. Namuomba Mungu akuzidishie uhai.
Nia na madhumuni ya barua hii ni kukuomba ushauri kwa tatizo langu. Kiukweli ndani ya moyo wangu nina wasiwasi mke wangu si muaminifu ndani ya ndoa. Yeye kaajiriwa Sinza Mori kwenye kibanda cha simu, sisi tunaishi Gongo la Mboto.
Kila siku huwa anachelewa kurudi nyumbani,  na kila siku anarudi na taxi, mi najua mshahara wake hautoshi kugharamia hilo ndiyo maana nakwambia nimeanza kuwa na wasiwasi. Hebu fikiria wiki iliyopita nilijaribu kugusa simu yake alikuwa mkali kwelikweli kidogo aniue, nikashangaa sana ukali wote huo wa nini?
Ila niwe mkweli, sijawahi kumuonyesha dalili zozote  kuhusu wasiwasi wangu, sitaki kumuudhi bila kuwa na ushahidi. Lakini mzee, jana niliamua kumfuatilia mke wangu hukohuko kazini kwake, nijue nini kinaendelea. Nikajificha mahali ambapo ilikuwa rahisi kumuona anapotoka kazini bila yeye kuniona.
Muda wa kufunga kazi ulipofika nikamuona anatoka kazini kwake akisindikizana na mwanaume mmoja mrefu hivi akiwa kamshika mkono wanacheka. Moyo ukaanza kunikimbia, nikaona niliyokuwa nahisi inawezekana ni kweli. Ili niwe na ushahidi mzuri nikaona niangalie saa ili nijue ni saa ngapi walitoka, wakati wa kesi kila kitu kiwe na ushahidi.
Mzee wangu nilipoangalia saa si ndiyo nikagundua saa yangu imesimama. Mzee saa yangu ni aina ya Rolex, na saa za aina hii ni bei ghali sana. Hii saa nilirithi kutoka kwa baba yangu, yeye aliniambia alinunua Uswisi wakati alienda kule kwa ajili ya kusindikiza mgonjwa aliyeenda kutibiwa huko na aliniambia kuwa ilikuwa na gerentii haitasimama kamwe, sasa ile kuona imesimama ilinichanganya sana.
Je, unanishauri vipi?  Niitengeneze kwa mafundi wa hapa Dar au nigharamie ikatengenezwe Uswisi? Au unanishauri ninunue nyingine?

Comments

Anonymous said…
bomba