HATUPIMI BANDO

10 July 2014

NDOTO NYINGINE BALAA


Ndoto bwana, mara nyingine ziko poa mara nyingine unajilaumu kwa nini ulilala. We fikiria unaweza kuota unafukuzwa na mbwa mtaani huna hata nguo moja,  kila ukikata kona huyu hapa, unaamka jasho chapachapa, au unaota uko vitani tena zile vita za kizamani za mapanga, ile unataka kukatwa kichwa unashtuka, ukitaka kulala inarudia palepale utadhani unaangalia muvi. Halafu kuna zile ndoto za maudhi, we fikiria unaota umekaribishwa msosi wa nguvu Ikulu, hapa wewe hapa JK, na sio Jk huyu John Kitime, hapana JK mwenyewe laiv, mnatia stori za kuhusu maendeleo ya nchi, maendeleo ya Diamond, basi mambo fresh kabisa, msosi unaletwa Mzee anakwambia kula  usiogope, unatafuta paja la kuku lililonona unatakakuling’ata tu, unaamshwa na hodi za baba mwenye nyumba anataka kodi yake ya mwaka. Yote tisa yaliyonikuta wiki iliyopita ndio kiboko. Nilienda kutembea kijijini kwetu Iringa ndani ndani , kijiji kinaitwa Mgama, pana kijito fulani kinapita katikati ya mashamba ya mboga,nilikuwa nimekaa pembeni najipumzisha njaa inaniuma baada ya kutembea mwendo mrefu, unajua kijijini kwetu bado hakuna bodaboda,  ghafla akatokea binti mmoja mzuri sana , nikashangaa huyu naye katokea wapi? Akanisalimu kikwetu, si unajua Kamwene, unogage na kadhalika, kaniuliza mbona umekaa peke yako? Nikamjibu nimechoka na njaa imenizidi, akanikaribisha kwao nikapumzike. Bwana huwezi amini nikaingia nyumbani kwao kuko vizuri sana, nikakaa kwenye kiti yaani sikuwa kijijini tena kila kitu cha kisasa, nikapewa juice nikanywa, msosi ukatengenezwa nikala vizuri, akanambia nimfwate , kumfwata akaniingiza chumbani kwake. Bonge la kitanda saba kwa saba, nikaonyeshwa bafu nikaoga akanambia sasa pumzika. Sikuwa naamini nakwambia. Ile kausingizi kanataka kuja nae akapanda kitandani. Akanambia, “Sogea na mimi nilale”, Sikuamini bahati yangu, nikasogea, akanambia, “Mbona mwoga sogea vizuri baby” Nikajisogeza vizuri ili Baby apate nafasi ya kulala. “Baby jamani sogea tena” Nikasogea…Dah huwezi amini kilichofuata si nilitaka kufa, maana nilijikuta nimetumbukia mtoni laiv na minguo yangu. Kumbe saa zote nilikuwa naota....HABARI HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA RISASI JUMATANO. KILA WIKI CHEKANAKITIME HUKUJIA NA MKASA MPYA KUPITIA GAZETI HILI

No comments: