PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

MBWA WETU ANAJUA KUSOMA NA KUANDIKA


Tajiri wa kijiji aliyekuwa anapenda sana sifa,alifanya kila jitihada mwanae ajiunge na chuo kikuu kimoja ili awe mtu wa kwanza kijijini kuwa na digrii. Yanki alijiunga na chuo lakini baada ya miezi michache akaishiwa pesa, akawaza atapataje pesa toka kwa mzee wake? Akapata wazo, akamuandikia baba yake barua.
 'Baba mpenzi huku chuoni mambo mazuri sana, naendelea vizuri sana na masomo mpaka wanataka kunipeleka Ulaya, nia na madhumuni ya barua hii ni kukwambia baba kuwa kuna maajabu makubwa sana. Hapa chuoni kuna profesa amegundua njia ya kufundisha mbwa kuongea, baba mlete mbwa wetu BINGO na ada ya shilingi laki 5, baada ya mhula mmoja atakuwa anaweza kuongea kama binadamu. Wasalam mwanao.’
Mzee wa watu haraka akatuma mkwanja na mbwa.  haikuchukua muda mkwanja ukaisha. Denti akamtumia baba yake barua nyingine kuwa wameboresha elimu sasa wanaweza kumfundisha BINGO kusoma, mzee aongeze kamilioni tu. Mzee wa watu aliyekuwa tayari anajisifu kijiji kizima kuhusu mbwa wake atakaerudi anaongea,  haraka akauza ng'ombe akatuma mkwanja. Likizo ikafika Denti akabaki anawaza anaenda kumwambia nini baba yake kijijini, maana uwongo wake ulishafika ukingoni. Alipofika tu kwao  baba yake akamuulizia BINGO. Denti akamuita baba yake pembeni,' Baba hili nitakalokwambia sitaki mama asikie'. Baba akauliza,'Vipi tena?'. Denti akaanza,' Jumatano iliyopita tumeamka vizuri na BINGO, yeye kama kawaida yake akaenda kununua gazeti la Risasi kama kawaida yake maana alikuwa tayari ameshajua kusoma. Akarudi na gazeti akakaa kwenye kiti na kuanza kusoma, wakati huo mimi nilikuwa najitayarisha kuingia darasani, ghafla BINGO akaniita akanambia hivi, 'Baba yako huyu vipi?’, nikamuuliza ,’Kwani vipi?’ Akaniambia,’Naona babako bado anaendelea na kale kachangudoa ka kijiji pale mtaa wa pili, naona hapa wameandika stori yake yote humu, nikirudi kijijini namwambia mke wake', Baba kwa kweli  nilishtuka. Mzee akaingilia kati,'Ungemuua hapo hapo mbwa mshenzi huyu nampeleka shule yeye anataka kuniharibia mambo yangu?', Denti akajibu,'Baba na mimi lilinijia wazo hilohilo sikumchelewesha nikamtwanga nyundo ya kichwa'. Baba akamsifu mwanae'Safi sana, safi sana mwanangu, una akili sana huyu mbwa angetuharibia familia mwanangu'............IMETOKA CHEKA NA KITIME GAZETI LA RISASI JUMATANO 30/7/2014.

Comments