PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

MATAYARISHO YA SUPASTA KUHUDHURIA MISIBA Wiki hii ningependa kutoa ushauri kwa masupastaa wetu. Kubwa hapa ni kuhusu taratibu za supasta kujitayarisha na hatimae kuhudhuria msiba, na hasa kama ni msiba wa supasta.
Kuna hatua kadhaa zinahusika, kwanza ni matayarisho , pili utekelezaji hatimae tathmini ya zoezi zima la kuhudhuria msiba.
Mheshimiwa supasta, mara upatapo taarifa kuwa kuna msiba, lazima uaanze kujipanga. Magazeti, redio, TV zote lazima zikusanyike, hivyo basi ni muhimu kuangalia fyucha itakuwaje. Hizi ni nafasi adimu kufufua jina lililoanza kupotea, hivyo muhimu sana kujwa tayari. Kwanza ni kuenda saluni. Kama mwanaume hakikisha unatengeneza wev, unapata skab ya nguvu ukitoka hapo mtu unamvuto wa kueleweka. Kisha ni swala la nguo, hapa ni muhimu kununua au kuazima suruali na koti jeusi, viatu vyeusi shati jeupe na mawazi meusi kama yale waliovaa akinaWill Smith kwenye ile picha Men in Black. Kama unavyo vitu hivyo peleka haraka dry cleaners. Jambo muhiu linalofuata ni kupeleleza kama kamati husika  zimeanza kuteuliwa na kupeleleza nani muhusika, ni muhimu kuwa katika kamati hasa kamati ya fedha.
Kwa wadada kimsingi matayarisho nayo yatalazimika kuanzia saluni. kuhakikisha uso unatengenezwa vizuri, mapoda, wanja, lipstik vinahusika. Nywele si muhimu sana kwa kuwa utalazimika kuvaa kilemba kichwani. Ila sura, kucha za mikono na miguu ni muhimu kzifanyia ukarabati wa hali ya juu. Baada ya hapo kutafuta dira la nguvu kama huna kaazime, ukikosea na kuja na kimini msibani shauri zako, waandishi watakuandama kuliko dengue. Muhimu kununua perfume ya kueleweka maana kila mtu atakuja ananukia perfume za bei mbaya, hata kama kaomba chumba cha jirani yake, sasa ukija unanukia vipafyum vya alfu tano utaumbuka. Simu ni ishu,chondechonde usije na Nokia tochi, kila mtu anakuwa kwenye Whatsapp na Instragram we utakuwa unafanya nini saa hizo? Wakati wanajipiga selfie we utakuwa unafanya nini? Kitu kingine muhimu ni kufanya mazoezi staili ya kulia. Unajua ukipaka wanja sio unalia hovyo machozi yatafuta wanja hivyo unafanya mazoezi ya staili ya kulia bila kuharibu ‘makeup’. Na jingine muhimu ni kufanya mazoezi ya kuzimia, na ikiwezekana uwe na mpambe wa kukudaka wakati unajitupa chini, mshirikishe kwenye zoezi kabla hamjafika eneo la tukio. Kumbuka kuna watu wengi wanakuja sasa usipofanya kitu kipya hutaweza kutokea kwenye magazeti na TV, kuzimia  ni bonge ya dili, hivyo muhimu kufanya mazoezi ya kuzimia.
 Baada ya hapo sasa ni kuhudhuria msiba, ni vizuri kuulizia kabisa kama kuna watu wa magazeti na TV. Ukijua ndipo utakapojua namna ya kuingia msibani. Kama unaingia kwa kilio kikubwa na kuzimia getini, au unaingia kimyakimya na kungoja midia ili kuanza kilio na kuzimia au kuzimia kabisa wenzio wakubebe ukaingia msibani umekwisha zimia. Onyo kabla ya kuzimia kabidhi simu yako kwa mpambe  wa jirani.
Msiba ukisha malizika ni wakati wa kutathmini shughuli nzima. Kwa wadada ni muhimu kuweka pembeni hela ya kununua magazeti yote kucheki umetokelezea mara ngapi, maana uwingi wa picha yako utaongeza kiki kwenye fani. Kwa wale jamaa zangu waliokuwa wanawania kuweko katika kamati hapa ndipo wakati wa kuhesabu mapato.

Comments