HATUPIMI BANDO

25 June 2014

MADUKA YA DAWA SIO VIJIWE VYA KUSOGOA MNATUKWAZA


Rafiki yangu Richii, sio huyu Richi unaemjua wewe, Richii ninae mwongelea anaishi maeneo ya Kwa Manyanya Kinondoni. Basi rafiki yangu Richii kanambia siku hizi akiwa anataka kwenda Famasi kununua dawa lazima awe anatembea na kiboko. Anasema kiboko hicho ni kwa ajili ya watu waliobadili matumizi ya maduka ya Famasi. Aliponihadithia mkasa uliompata, kwa kweli na mimi nimeamua ntafuata ushauri wake, na nikiwa naenda Famasi lazima nitembee na mkwaju, hata mkiniita Mzee Kifimbocheza potelea mbali. Richii kanambia mtaa wa pili toka kwao alihamia binti mzuri sana, roho yake yote ikamtoka akawa anajitahidi kila njia apate nafasi ya kuongea na huyu malaika. Zali likamuanguakia akapata namba ya Whatsap ya binti, mawasiliano mazuri yakaanza. Siku hiyo wakawa wamekubaliana kukutana sehemu kupata mishkaki. Wakachagua kagrosari kanaangaliana na Sipapune Guest House.  Baada ya vinywaji kadhaa Richii akaaga kidogo na akavuka na kwenda kuulizia chumba pale gesti, chumba akaambiwa kipo, alipoulizia kinga akaambiwa hakuna ila kuna kafamasi kako kona ya jirani.  Richii akakimbilia kwenye famasi ili amuwahi binti kabla hajamaliza kinywaji, kuingia tu ndani ya Famasi kashikwa na kigugumizi, si kakuta wadada wanasukana, kabaki kuangalia tu madawa kama vile anafanya windoshoping, akatoka kimyakimya bila kusema neno. Unajua kununua  kinga inataka faragha kidogo, akazunguka kona mbili akakuta famasi nyingine, hapa kakuta watu kama sita hivi wanaangalia mechi ya Kameruni na nani sijui, akatoka kakimbilia Famasi ya tatu anakuta wadada wanahadithiana kuhusu mkutano ulioitishwa na mchungaji wa kanisa lao. Richii si akaona heri arudi grosari akamueleze mdada kilichomsibu, si kakuta binti kishasepa, na mbaya zaidi keshalipa  na bili yote na kutoa kashfa kuwa mwanaume kanywa kasepa………..SOMA KIU KILA JUMATANO UPATE MAKALA YA CHEKA NA KITIME

No comments: