PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

JE UNAPENDA BIA ZA BURE?

Leo nichukue nafasi ndugu wananchi kutoa darasa ambalo litawasaidia wengi tu. Lakini haswa darasa hili ni kwa wanaume wanywaji wa pombe na hasa wale wanaopenda pombe lakini pesa hawana. Kuna wale jamaa zangu ambao wamejiwekea utaratibu wa kupata japo chupa mbili za bia kila siku japokuwa mbongo te, au kwa Kiswahili cha mjini mkwanja umekataa. Kitu cha kwanza kabisa lazima uhakikishe kuwa unakuwa smat unapoelekea bar au grosary kwenda kudandia pombe, unaoga na kuvaa vizuri kama vile unahela. Ukifika tu uwe mchangamfu, na kusalimia vizuri hasa mtu ambae umeshamtageti kuwa atakununulia pombe kwa siku hiyo, na kama unamfahamu jina, basi weka bonge ya sifa mbele ya jina la mfadhili.  Unaweza kuanza, “ Ahh mzee wa wazee, Mkuu wa majeshi Kitime, mlezi wa wana upo mzee?” Yaani muhimu utoe sifa sana, kama yuko na mamaa, wahi kutoa sifa nyingi kwa mamaa, japo ikitokea kuwa unaemsifu ni dadake na sio bibi yake unaweza kukosa bia ukaambulia matusi na kufukuzwa, hapa lazima uwe makini kidogo. Kama mfadhili umemkuta kakaa na kundi la watu, lisifu kundi zima, “ Ahhh mzee naona umezungukwa na jopo la watu wenye akili tupu, wazee wa mipango, wazee wakali wa mji” na sifa kama zile. Kisha vuta kiti wakati bado wanacheka na haraka uanze kuwapa vichekesho vikali mfululizo. Ni muhimu kabla hujaingia bar kuwa umefanya mazoezi na kupanga vichekesho utakavyo hadithia, usije ukaanza kichekesho ukaishia katikati, kisipochekesha utawaboa utakosa bia. Kwa kawaida ukiweza kuwachekesha wote waliopo,  unaweza kuanza  kuagiza bia, lakini usiingie mkenge wa kutamka agizo hilo wewe, hakikisha unamuingiza mkenge mfadhili kwa kumuuliza ‘ Mzee wa wakuu, ninywe nini mwanao?” Atakachokuchagulia ndicho hicho unywe, ujue mtu anaeomba hana mamlaka, jitayarishe hata kunywa bia za aina tatu kwa siku kutegemea na anaekuagizia anakunywa nini.
Kinywaji kikifika usinywe kwa pupa angalia upepo je, kuna uwezekano wa kuagiziwa kinywaji kingine? Ukiona hali ni nzuri ongeza spidi ya kunywa. Usiache kuongea sana maana kete yako ni hadithi, usijali ni za aina gani, ziwe za kweli au uwongo wewe mwaga tu.  Kitu kingine muhimu hauruhusiwi kuwa na msimamo, wewe msimamo wako wa siasa, dini, bendi bora msanii bora, muvi bora utategemea anae nunua kinywaji anasema nini, akisema serikali tatu, wewe haraka unga mkono na kushabikia serikali tatu, akisema serikali moja, fwata hukohuko, hata akisema nchi isiwe na serikali, wewe upesi unga mkono.  Mwisho hakikisha unaondoka bila kuharibu mambo, ili kesho mkikutana uendelee kukamua ng’ombe wako kwa raha zako…nasubiri ripoti ya utekelezaji
ILITOKA KATIKA CHEKA NA KITIME.GAZETI LA KIU.........

Comments