PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

MTIZAMO WA BLOG HII KUHUSU IDADI YA SERIKALI

Baada ya kutafiti kwa makini sana mazungumzo yanayoendelea nchini, hasa kuhusu hili ambalo linawatesa wanasiasa, swala la idadi ya serikali, blog yenu makini imefanya utafiti wa makini kwa kufuata ule usemi wa wahenga wa Ulaya unaosema 'No research, no right to speak'. Blog hii makini kwanza ilitafuta mamilioni ya fedha toka kwa wafadhili wa ndani na wa nje, ili kuwezeshwa kufanya utafiti huu ambao matokeo yake yataushtua ulimwengu wa huu wa Bongo. Watafiti wa blog walizunguka nchi nzima na kuhoji mamilioni ya watu wakiwemo wanaume, wanawake, na hawa jamaa ambao hawajulikani kama wako upande gani, pia ilihoji hata watoto wachanga. Matokeo ni kuwa asilimia 99 ya watoto wachanga waligoma kabisa kujibu, wakaonyesha dharau kwa watafiti wetu, na asilimia moja wakiamua kulia au kucheka kwa kila swali la watafiti. Tunaishauri serikali iwachukulie hatua kali watoto hawa kwani wameharibu kabisa utafiti na hivyo kuleta majibu yasiyokubalika katika utafiti. Kwa kweli blog ilipita hospitali kadhaa na kuhoji hata wale wenye matatizo ya uchizi. Hawa walisaidia sana blog hii kuwaletea majibu yetu kuhusu tafiti hii. Kimsingi tunapingana na tafiti zote za kisomi kuhusu idadi ya serikali katika nchi hii. Kwanza kuna makosa makubwa kuhusu idadi ya serikali zilizopo, bila kupepesa macho imekuwa ikisisitizwa kuwa kuna serikali mbili, utafiti rahisi uliofanyika pale Mirembe uligundua hakuna ukweli wowote wa jambo hili. Watoto kadhaa pia waliweza kututaarifu kuwa hata mtaani kwao kuna serikali. Hivyo basi ukikusanya serikali za mitaa zote, ukijumlisha na mbili zinazotajwa sana tayari una maelfu ya serikali nchi hii. Kwa msingi huu blog hii inaomba kutengeneza upya rasimu ya katiba ya Bongo. Asante. Utafiti huu utawekwa wazi karibuni

Comments