PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

JE UNATAKA KUJA DAR ES SALAAM? ZIJUE STAILI ZA KUVUKA BARABARA KWANZA

Kwa kweli blog hii asubuhi hii imeona itoe ushauri kwa ndugu wananchi ambao wanaopanga kuja katika jiji la Dar es Salaam aidha kutembea au kuhamia au hata kuja kufanya kazi ya uhauzgelo. (Siku hizi blog hii imegundua kuna mahauzgelo kadhaa wanaoisoma ili kuongeza akili.)
Ndugu mwananchi, ukifika Dar katika moja ya mambo ambayo yatakuchanganya ni namna ya kuvuka barabara. Kwanza kuna  barabara za aina nyingi sana, kwa mfano kuna nyembamba za njia moja, ziko nyingine ni njia mbili, kuna hata moja inatoka Moroko hadi Mwenge ambayo hata wanasayansi wa kimataifa wameshindwa kujua kama ni ya njia 3,4,5 au 6. Ni hatari sana kuvuka barabara hii ya Mwenge Moroko.
Ukifika Dar kabla hujavuka barabara kwanza angalia kushoto, kisha kulia, kisha kushoto, kisha kulia chonde chonde usianze kuvuka hata kama hujaona kitu pia tumia masikio kusikiliza kama kuna kitu kina kuja, kuna hawa jamaa wa bodaboda na bajaj, huwa wanazuka kama majini ghafla unawakuta wako mguuni kwako ni muhimu sana kuhakikisha hawako jirani, bado usinyanyue mguu kuvuka angalia juu kwanza, hapa Dar kumekuwa na mchezo wa kujenga ghorofa kwa kutumia mchanga wa baharini ili kupunguza matumizi, ghorofa kadhaa zimekwisha dondokea vichwani mwa watu hapa mjini, hivyo angalia juu pia kucheki kama ghorofa la jirani liko poa? Wakati huohuo angalia nyuma, mji una vibaka huu balaa. Kama una mtindo wa kizamani wa kuweka pochi mfuko wa nyuma ni muhimu uwe na jicho huko usije ukavuka barabara kumbe wenzio wamchukua pochi. Kama uko mitaa ya Tandika, Manzese, Kinondoni Mkwajuni wakati unataka kuvuka ukisikiaa  ghafla mtu anakwambia "mdudu huyo, mdudu huyo", we endelea kuvuka usiogope hao ni matapeli wanataka kukuchanganya wakuibie simu. Baada ya hapo kama kila kitu kiko poa, Mungu akusaidie anza kuvuka huku ukikwepa magari kwa staili ya Rambo anavyokwepa risasi. Hii staili ya kukwepa risasi inaweza kukusaidia sana maana pia unaweza kuwa unavuka barabara ukakuta kuna jamaa wameamua kutembeza risasi kwenye shughuli zao za ujambazi. Hata hivyo wanyalukolo wenzangu  karibuni Dar

Comments