PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

HISTORIA YA BOSI WETU

Mimi mwenyewe 'live'

Naitwa John Kitime, nilianza kufurahia vichekesho mara baada ya kuzaliwa na kukuta watu wazima kila wakinichukua walijitahidi kunichekesha kwa kuanza kuonea lugha ambayo sijaijua mpaka leo, maana mara alikuja mmoja na kuanza ‘bujibujibujibujibuji,jigijigjigjigjijij, grugrugrugru’ na maneno mengine ya ajabu nilijitahidi kuwavumilia nisiwacheulie maziwa lakini baadae nikagundua heri niwe nacheka wakianza vituko hivyo, maana baada ya hapo walikuwa wanajiona wanajua kuchekesha watoto wachanga.Niliendelea kukua nikaanza shule nakukuta vituko vingi sana vya kuchekesha, kama vile  watu kujikojolea darasani, hili bahati mbaya nililikuta linajirudia pia kuwakuta wakubwa wakijikojolea kwenye baa, na kilabuni, ene way, nilimaliza shule na kujiunga na vyuo mbalimbali nchini na huko nilijifunza utalaamu wa kunywa pombe na huko nilikutana na watu wengi wenye kujua kuchekesha, kucheka na hata wasiojua kuchekesha wakijitahidi kuchekesha , cha kushangaza si nikakuta wengine hawajui kucheka kabisa, au wanaweza kucheka mahala pasipo na kichekesho cha kuchekesha wachekaji.
Katika kiota hiki ntaweeleza mengi yaliyonikuta katika maisha yangu haya yaliyojaa furaha sana NAMSHUKURU MUNGU.
Pia mimi ni mwanamuziki napiga gitaa naimba kwenye bendi, lakini huwa sichezi, sijui kucheza, chacha inanichanganya kabisaaa, hii mitindo ya kisasa ndio kabisa siiwezi. Kuna hii inaitwa kiduku, wakati najitahidi kujifunza imeanza kwaito, sijaishika sawasawa imekuja Kibajaji, mara ngololo , sijui skeleu heee jamani si mngoje japo nijuwe staili moja ndio mbadili? Halafu kwa kweli huwa inanishangaza, mtu analipa kuingia muziki halafu anacheza kuliko sisi wanamuziki jamani, mnajua mngepewa majembe mlime badala ya kucheza mngesha maliza tatizo la njaa hapa nchini?

J F K

Comments