PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NIMELOGWAAA?????????


Niko chumbani kwangu nafanya mazoezi ya kucheza NGOLOLO , jasho linanitoka mwanawane, unajua tena umri umesogea lakini imekuwa muhimu hapa mjini kujua kucheza ngololo. Kila mtu anajua kucheza ngololo kasoro mimi why?  Ila kuna kitu huwa kinaniudhi sana, mnakumbuaka wakati ule Marlaw alipokuwa anatupa raha kwa Kiduku, ikawa kila mtu anacheza Kiduku na mi nikaona lazima nijifunze, nikajifungia ndani wiki mbili nilpotoka hapo nilikuwa naweza kushuka nikawa mfupi kama mtoto mchanga, natembelea vidole tu, mbona walipata tabu mtaani, kwenye maharusi, kwenye bar, au popote pale   nikimsikia tu Marlaw akiimba Pii Pii nawasha moto, kwani umaarufu ulidumu basi, si wanamuziki wakaja na kitu kipya kinaitwa Kwaito, kila mtu akawa anacheza Kwaito kasoro mimi, maana ilikuwa aibu, unakuta ukumbi mzima hata vitoto vidogo wote wanaenda stepu moja, nikijitahidi kujiunga niwafwate inakuwa tabu wakigeuka kushoto mie kulia, wakija kulia mi naenda mbele, kumbe wao sasa wanaima na kuinuka. nikaona isiwe tabu, nikajifungia chumbani kwangu na kupiga tizi kali la kucheza Kwaito. Mwanawane nilipozipatia kitu cha kwanza nikapanda basi nikaenda kijijini kwetu kule Iringa ndanindani na kuanza kufanya mambo yangu kwenye vilabu kila jioni, nikageuka supasta, hata jina la ukoo wetu likapaa, ingawa  hii ishu ikaniletea  bifu na supasta niliyemkuta kule kijijini aliyekuwa akitamba kwa staili yake ya kwasakwasa, ile ya kucheka kama unakata miwa huku kiuno kinazunguka kama feni. Niliposikia anataka kuniloga nikaona nirudi Dar. Kufika Dar hasara tupu, huku nimekuta mambo yamebadilika ndio nimekuta hii kitu Ngololo, ndio niko bizi sasa naifanyia kazi.
Lakini mi nadhani nimelogwa, maana maisha yangu yote nimekuwa nyuma kwenye mambo mengi, na  nikijitahidi niwakute wenzangu mchezo unabadilika. Nakumbuka enzi hizooooo wakati wadada wote wakali wa mjini ilikuwa lazima wawe na kalikiti, mimi demu wangu alikuwa kang’ang’ania kusuka mabutu. Nikaona nisiendeleze aibu, heri nimuache nitafute na mie demu wa kisasa mwenye kalikiti, ile nampata tu sijaanza hata kutamba mjini , wadada wakabadili staili wakawa wajanja wanasuka rasta, ikala kwangu.  Hata enzi hizoo wakati kila mjanja alikuwa anavaa viatu vya raizoni, mimi nilikuwa bado na viatu vyangu maarufu kama Safari buti, nikajitahidi nikajinyima nikapata pesa ya kununua raizoni, nikanunua nikaamimi ntakuwa kwenye kundi la wajanja, wiki chache tu baadae staili ya mjini ikawa kuvaa viatu vinaitwa moka, ikala kwangu. Hata karibuni tu imenitokea  kwenye ishu ya simu, wajanja wote wakawa na Blackberry mi nikawa nasota na  Nokia tochi yangu, nikastrago nikaweza kununua Blackberry, nikaanza mbwembwe za kuwatangazia watu  kuwa nina PIN namba, sasa wananicheka wananambia siku hizi mambo Samsung watu wanakutana kwenye Whatsapp sijui Insta, imekula kwangu tena……..Nauliza au nimelogwa?.........HII ILITOKA KWA MARA YA KWANZA  KATIKA GAZETI LA UWAZI....KILA JUMANNE SOMA VITUKO VYA  CHEKA NA KITIME KATIKA GAZETI LA UWAZI

Comments

Iddy Nassoro said…
That nice i like it