HATUPIMI BANDO

8 December 2013

NIMEAMUA KURUDIA KAZI YANGU YA UTABIRI KWA MUDA TU..TUMIA NAFASI VIZURI

Huwa sipendi sana kutumia utaalamu wangu wa nyota, ambao nilifundishwa huko Uajemi kusini wakati nikiwa katika safari zangu za kutafuta vichekesho vya Kiajemi. Lakini kwa maombi ya wengi nimelazimu kuchukua nafasi hii kutabili mambo muhimu katika kipindi cha mwaka kilichobakia. Kutokana na nyota zilivyokaa nitazungumzia zaidi hali ya mapenzi na wapendanao kwa kipindi cha mwaka kilichosalia.

UTABIRI....Kuanzia leo tarehe 8 hadi 25 Disemba ni kipindi kibaya kwa wapendanao. Kuna wadada wengi watajikuta wanaachika bila sababu maalumu, kitendo cha kumtania tu umpendae, au kuchelewa kujibu simu, text, whatsapp kitaishia kufukuzwa na kutengwa  kwa hasira kuu, hii ni kutokana na nyota kuingiliana njia, hizi nyota zimejichanganya za kusini zikapita njia ya zile za magharibi. Bahati nzuri ni rahisi sana kukwepa balaa hili la kuachika. Wadada ni muhimu nasema ni muhimu, kuanzia leo, usitamke neno ZAWADI. Kwa kuwa kinyota neno hilo limezingirwa na nyota nyeusi isiyotabirika na hivyo kuweza kumfanya mpenzi wako asitabirike na kukufukuza bila sababu. Epuka narudia tena epuka kutamka neno ZAWADI na hasa ukIwa umeunganisha katika sentensi moja neno KRISMAS au NEW YEAR. Balaa hili litapita tarehe 31 Disemba asubuhi, hapo unaweza kutamka maneno hayo bila balaa yoyote kukumba. Ila kwa wale wataakaoachika wasipaniki maana nyota zinaonyesha mapenzi yatarudi katika hali yake kuanzia hiyo tarehe 31.

No comments: