PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

NAANZISHA BODABODA DRIVING ACADEMY

HII ishu ya kukamata fursa imenifanya nikeshe siku tatu mfululizo nikiwaza, niikamatie wapi hiyo fursa?  Hatimae usiku wa kuamkia leo kitu kama saa tisa na nusu hivi,  picha ya wazi ikaja ya nini nifanye.
Hapa nipo namalizia kuandika mambo ambayo nitayafanya ili niishi vizuri hapa mjini. Hii ni siri nawaambia nyinyi tu ndugu zangu, nimeamua kuanzisha chuo kitakachoitwa  International Bodaboda Driving Academy, kifupi IBODA.
Mtakubaliana nami kuwa fursa hii iko wazi kabisa na haina ugomvi na mtu, wateja na mateja wako kibao wanataka kuingia katika biashara ya kuendesha bodaboda. Yaani fursa hapa iko nje nje  waziwazi. Kimsingi hatua ya kwanza nimepanga kuanza kusaili wanafunzi wa kujiunga na chuo. Sio kila anaekuja kuomba kusoma atakubaliwa. 
Kitu cha kwanza kutakuwa na mtihani wa maswali machache ambayo ili ujiunge na chuo lazima ufeli, chuo kinachukua wale tu watakaopata divisheni 5 ya usaili huu. Hapa pia ni kutoa fursa kwa divisheni 5 nao waweze kupata maendeleo, utaona kuwa hapa tunafanya kazi ambayo wengi huikwepa nayo ni kuwawezesha divishen 5 waishi mjini.
Pia soko la waendesha bodaboda linahitaji watu wenye vipaji vya kipekee ambavyo vinaweza kupatikana kwa njia hii ya  kuchuja wenye divisheni 5 tu. Maswali ya usaili yatakuwa machache tu nayo ni  kama ifuatavyo; JIBU NDIO AU HAPANA, Je, ukigongwa na gari utaumia? NDIO/HAPANA.
Je, ukikatika mguu utaota tena? NDIO/HAPANA. Je, kusubiri taa za barabarani zibadilike ni ushamba? NDIO/HAPANA. Je, kuvaa helmet ni ushamba? NDIO/HAPANA. Je, mshikaki wa abiria watano unawezekana? NDIO/HAPANA. Atakaefeli maswali yote ni wazi uwezekano wake wa kujiunga na academy upo wazi, maana ukipasi ni wazi akili yako haifai kuwa dereva wa bodaboda.
Kati ya somo muhimu katika chuo litakuwa ni staili mbalimbali  za upigaji wa honi.  Somo hili litachukua muda mwingi sana hapa, kwani honi ndio chombo muhimu kuliko vyote katika uendeshaji wa bodaboda.
Ukiwa unaendesha bodaboda huna haja ya kupunguza spidi, we kazi yako kupiga honi, kila kitu kinakuachia njia, watu, magari, malori ya mchanga, hata kama kuna treni inakuja we piga honi, lazima itakupisha.
Somo jingine muhimu ni namna ya kuendesha bodaboda huku umefunga macho, utaalamu huu hutumika na waendeshaji pale wanapotaka kuvuka wakati taa zinaonyesha rangi nyekundu.
Pamoja na mengine mengi Academy itafundisha somo muhimu la namna ya kuvunja ‘saiti mira’ za magari wakati dereva wa bodaboda anapo ‘ovateki’ au kupita katikati ya foleni ya magari. Silabasi ya namna ya kupanga abiria ili kuwa na mshikaki mrefu inaandaliwa. Karibuni.......MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA UWAZI...SOMA UWAZI KILA WIKI UKUTANE NA CHEKA NA KITIME

Comments