PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

LALA PEMA MADIBA.....ISHU HII INGEKUWA BONGOLAND


Ile ishu ingekuwa kuleeee Bongoland……Kwanza kungeundwa Kamati ya mazishi ambayo ingepewa uwezo wa kutoa mikataba ya shughuli mbalimbali ambazo zingetakiwa kufanyika. Kwanza ingetolewa tenda ya kukarabati uwanja wa ndege wa kijiji kwenye mazishi, tenda ya kukarabati mabarabara ya kuelekea kijijini huko, pia kungetakiwa kuagiza ambulensi bullet proof kwa ajili ya kusafirisa mwili toka hospitali mpaka eapot, pia ingetolewa tenda ya kuagiza magari 20 ya kifahari  ya kusindikiza mwili. Jamaa zetu wangepewa tenda ya kujenga jukwaa na kuratibu shughuli zote za kuaga mwili pale Leaders Club.
Burudani zingesimama kwa miezi mitatu, kiukweli hapa wanamuziki wangekatazwa kupiga muziki miezi mitatu lakini redio na TV zingepiga tu kama kawaida, na sanaa nyingine zingeendelea tu. Yunifom za wahudumu wa shughuli zingeagizwa toka Uholanzi japo kuwa zimetengenezwa Uchina. Wananchi wangehamasishwa kuvaa yunifom hizi kuonyesha uzalendo, zingeuzwa kwa bei rahisi, Tshirt 20,000/- tu. Mashirika yangeshindana kutoa rambirambi kwenye magazeti, TV na radio, matangazo haya yangefanyiwa tathmini ya undani gharama zingefikia mabilioni kadhaa. Wanamuziki wangepishana studio na kutoa singo ambazo zingeuzwa na wasio wanamuziki na kuingizia watu mkwanja wa ukweli na kuwaacha wanamuziki wanadaiwa malipo ya studio. Mablog yetu yangejaa vichwa vya habari..Ona picha za mwisho za marehemu akiwa mochwari, Ingia hapa uone chumba alicholala marehemu alipotembelea Iringa, Pata picha ya nyumba ndogo wa marehemu akilia, ingia hapa uone picha za nyumba ndogo ya rafiki yake mdogo wake marehemu akiwa kavaa kanga moja akielekea bafuni na kadhalika. Baada ya hapo Wabunge wangekuja juu kuhusu matumizi makubwa ya shughuli hiyo na kuomba tume iundwe kuchunguza matumizi ya  Kamati ya Mazishi, kwa kuwa uchaguzi uko mbali ishu ingekufa baada ya siku chache kama ile ishu ya matumizi ya miaka 50 ya nanihii.

Comments