HATUPIMI BANDO

14 January 2013

SERIKALI ICHUNGUZE SPONJI ILIYOWEKWA KWENYE VITI VYA BODABODA

-->
Honda 90
Pikipiki ya kwanza
Pikipiki zilianza kutumika Ujerumani katika karne ya 19. Ulikuwa usafiri uliokuwa mpya lakini ulirahisisha usafiri hasa ukukimbuka watu wa huko wakati huo wengi walitumia wanyama kwa usafiri. Huku kwetu enzi ya Muingereza ndio pikipiki zilianza kusambaa sana na kati ya pikipiki zilizopendwa zilikuwa za aina ya BSA kutoka Uingereza, pikipiki hizi zilipata jina kutoka kampuni iliyokuwa inazitengeneza iliyoitwa Birmingham Small Arms company. Baada ya Uhuru pikipiki za Honda na Suzuki kutoka Japan,  zilikuwa maarufu sana hapa nchini, kwani kuna wakati serikali iliwapatia Makatibu Tarafa , Mabwana Shamba na watumishi wengi wa serikali pikipiki aina ya Honda 90 na baadae Honda 125. Miaka yote hiyo waendesha pikipiki walikuwa watu wastaarabu walioheshimika na kuheshimu sheria za barabarani. Miaka hii michache zimeingia pikipiki za Kichina, ambazo zimezagaa kwenye biashara inayoitwa Bodaboda. Waendesha bodaboda wamekuwa watu wa ajabu ambao hudhani kuwa wao wana haki ya barabara na hata pembeni ya barabara kuliko mtu mwingine yoyote, na kuwa wao sheria za barabara haziwahusu. Pia ni watu wanaoamini kuwa ukipiga honi tu inatosha hata miti inahama wakati wao wakitaka kupita, mamia wanajeruhiwa na wengine kufa kwa ajaili za kila siku za usafiri huu. Naomba serikali ifanye uchunguzi kwanini watu wakiendesha hizi pikipiki za Kichina akili inahama? Mimi na mashaka na sponji inayotumiwa kwenye viti vya Bodaboda, inawezekana ina madini ambayo yakimuingia anaeiendesha akili inahama. Serikali ifanye uchunguzi wa wasiwasi wangu huu. Kwa kuwa sioni sababu kwanini waendeshaji wa zamani walikuwa hawapotezi akili. NAWASILISHA HOJA

No comments: