HATUPIMI BANDO

6 January 2013

BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA...naomba uniteue


Mheshimiwa, salamu,
Mheshimiwa mimi ni mwananchi mtanashati, mrefu mnene mwenye mwanya wa wastani, mwenye mwendo wa maringo hatua za hesabu, tabia ya pekee na shingo ya upanga, umeonaee.
 Kwa kweli nimekuwa nasikiliza ushauri wako kuwa wananchi tutengeneze ajira sisi wenyewe, Mheshimiwa mimi nimegundua ajira ambayo itaniletea manufaa na pia kuliletea Taifa letu changa mapato mengi umeonaee. Mheshimiwa naomba uniteuwe wadhifa wa Katibu KATAKATA Mkuu Tanzania. Hadidu rejea za wadhifa huu  ni kuwa mratibu wa Kata kata zote nchini. Labda nitoe maelezo mkuu, hapa nchini kuna watu wanakatakata mambo bila mpangilio, kwa kunipa cheo hicho nitaanza kuratibu katakata zote na hivyo kutoruhusu  mtu kukata kitu bila kupewa stika ya ushuru, na hivyo kila kukata kutalipiwa umeonaee.
 Kimsingi chochote chenye neno KATA ni lazima kipewe kibali na mimi Katibu Kata Mkuu. Ni wazi nitaanza na hawa wanaokatakata umeme, ni lazima wapate kibali ambacho watalipia kodi na ndipo kuruhusiwa kukata. Kuna wengi tu wanaotumia bure huku kukata, kwa mfano hawa wanamuziki wa Njenje wanawimbo wao wanasema, ‘Kata kata , kata chako mwenyewe, kata mwenyewe hayuko’ na hivyo kuhamasisha watu wakate kiuno bure, hii iwe mwisho sasa, watalazimika kupata stika ya kodi kabla ya kuimba wimbo wao huu, na wote wanaokata kiuno walipie ushuru kwa kufanya hivyo.
 Kuna watu wengi tu wana Kata tamaa, bila taarifa yoyote, wengine wana kata kiu bure kabisa bila kulipia kodi, kuna wale wanao kata roho hawamuelezi mtu kwa hiyo kulinyima Taifa letu changa mapato, hii si sawa umeonaee. Mheshimiwa nadhani utaweza kuona ukubwa wa kodi ambayo tutaweza kukusanya ni zaidi hata ya mapato kutokana na madini, hata hawa jamaa wakitaka kukata gesi isije huku, watalazimika kuniomba kibali ili walipie kodi. Hata tukichukulia wale wanao kata kodi, kata tiketi, kata shingo, au hata wale wanao wakata wenzao kilimilimi, au kuwakata ngebe, ni lazima walipie. Hawa wanaotaka kukata kauli ni vyema tukawatengenezea mazingira wawahi kulipa kabla hawachukua uamuzi huo mgumu umeonaee. Nami nitateua makatibu wa katibu katakata, kutoka kata mbalimbali kuratibu katakata zozote ili kusikatike mtiririko wa makato ya wakataji nchini umeonaee
MKUU NOMBA UNITEUE NIWE KATIBU KATAKATA MKUU WA TAIFA nawasilisha hoja.

1 comment:

Anonymous said...

Pia mwambie muheshimiwa asisahau kwamba tunapoteza kodi pia tutoka kwa vijana wanaoshusha trauza zao na kuacha nguo ya ndani ikawa nj. wenyewe wanaita kata K..hawa ni wengi sana na ukusanyaji kodi utakuwa rahisi kutokana na mazingira wanayopatikana..kwenye mabar,kwenye kumbi za starehe, mavyuoni na nasikia hata maofisi pia wapo..