PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

CHEKANAKITIME KUKIMBILIA MAHAKAMANI


Kwa kipindi sasa  kwa niaba ya  blog ya www.chekanakitime.blogspot.com nimekuwa napokea tuhuma nzito kwa njia ya ujumbe kwenye facebook, text message kupitia namba yangu 0758474500, na baruapepe kupitia jokitime@gmail.com unaonaee. Tuhuma hizi nzito kutoka kwa watu mbalimbali eti NINA WAVUNJA MBAVU haziwezi kuachiwa zipite hivi hivi na kuenea kitaifa na kimataifa bila kupingwa kwa nguvu zote na mimi kama mtuhumiwa mkuu wa kuvunja watu unaonaee.
Mimi ni mzee mmoja mtanashati, si mrefu wala mfupi, nina tabasamu la wastani, mwendo wa kudunda japo si sana unaonaee. Nina sura ambayo imepambwa na mustachi uliyosheni ndevu nyeusi ambazo kwa mbali zimepambwa na mvi chache zilizopangwa kisayansi na hivyo kuleta mvuto ambao wenye busara huuona toka mbali na kutoa sifa kitaifa na kimataifa, unaonaee. Wanaonifahamu wananisifia kitaifa na kimataifa kuwa mimi ni mpole, mtaratibu ambaye hupata majonzi makuu kama nikimkanyaga hata sisimizi kwa bahati mbaya, wengi wanajua hata kwangu mbu hupendelea kuishi kwa wingi kwa kujua mimi si mmoja wa wale watu makatili ambao hudiriki kununua sumu ya mbu na kufukizia  ili kufanya kitendo cha ukatili wa kuuwa kiumbe hiki chenye sauti nyororo kiitwacho MBU unaonaee. Sasa turudi kwenye tuhuma hizi nzito za mimi kuvunja watu mbavu, tuhuma hizi ninaweza kuziweka katika makundi makubwa mawili, wababa na wamama.
 Kuna wababa wanalalamika kuwa nawavunja mbavu, na kuna wamama, ambao wengine singo wengine mered wengine hata hawajulikani wako kundi gani, maana status za Facebook zao zinabadilika kama taa za disco, singo, mered, not singo, double he wajameni, ene wei wote hao wamo katika kunituhumu kuwa nina WAVUNJA MBAVU. Hebu tuangalie kitendo cha kumvunja mtu mbavu, kwanza ni kitendo kinachohitaji  ukatili na nguvu za ziada, maana baada ya kumkumbatia mhusika na kumkamua kwa nguvu mpaka usikie taaaa, ndio unajua hapo mbavu imevunjika. Sasa ukirudi kwa wababa,kwanza  nakataa tena nakataa sijawahi kumkumbatia mbaba yoyote, hata kama ni kwa salamu zile za kiuwana siasa unaonaee, na pili sijawahi kumukumbatia mbaba nikamminya mpaka nikamvunja mbavu, hebu pata picha mi na mustachi wangu huu wa ukweli, nimembana mbavu mbaba mwenzangu, jamani, this is scandalous, si vizuri kunituhumu mambo kama hayo jamani.  Kuhusu wamama nao hebu imajin napita maofisini, kamata sekretari bana mbavu mpaka zivunjike, kamata sijui programe ofisa bana, marketing bana (lakini hawa wa maketing kweli kuna haja ya kuwavunja mbavu, nawaomba matangazo wanani promise kwa kizungu,’ Yua blog is so fanii, wi wil kol you tumoro’ ndio jiiii au ndio ile ya tumoro neva kams?) unaonaee Haya naingia maintanet kef, shika wadada minya mbavu mpaka zivunjike, jamani walimwengu hamuoni kuwa tuhuma hizi ni wazi si za kweli? DHEAFO KWA HIYO…NATANGAZA KUANZIA LEO NTWABURUZA MAHAKAMANI WOTE WATAKAO NITUHUMU KUWA NIMEWAVUNJA MBAVU.
           

Comments