PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

LEO NIMEKUMBUKA ENZI ZILEEEEEE

Nimekumbuka enzi ziiile ambazo Pikipiki ilikuwa haijaitwa Bodaboda, na Vigogo walikuwa wanaitwa Manaizi, hii ilikuwa kabla hawajaitwa Mabwanyenye. Kwanza niseme, waliitwa Manaizi kutokana na sera iliyojulikana kama Africanization, yaani mara tu baada ya Uhuru kulikuweko na kazi ya kuwaweka Waafrika katika vyeo vilivyokuwa vinashikiliwa na wazungu. Hawa Manaizi ndio walikuwa wenzetu ambao tulisota wote kudai Uhuru wao walipopata nafasi zilizokuwa za wazungu wakawa wengine kabisa wakaitwa Manaizi, kama leo jamaa mnasaidiana kudai haki, mnamchagua awe kiongozi wenu anageuka mtawala wenu halafu anakuwa Kigogo. Turudi kwenye mada, nakumbuka enzi zileee kabla warembo hawajaitwa, kichuna, kisura, kipusa, baadae kuitwa Kishtobe (kutokana na meli yenye jina hilo) , siku hizi dah, demu, gashi, changu, haya tena. Nakumbuka enzi zileee wakati kabla ya RTC, wakati kulikuweko na COSATA, hii ilikuwa kabla ya kuweko kwa BADEKO, MODECO, IDECO,MBEDEKO,BUDEKO, na kiukweli nakumbuka kabla ya kuweko maduka ya kaya, ambapo mwenye duka alikuwa na daftari inayoonyesha umenunua sukari kilo ngapi wiki hiyo, nakumbuka sana ule mwezi wa Februari 77, ambapo bia ya Safari ilianza kusambazwa , tukaanza kusikia watu wanapoteza fahamu kwa kunywa safari 3 tu, hiyo ilikuwa kabla wamama hawajawa na ujasiri wa kunywa Konyagi hadharani, hii ilikuja baada ya Konyagi chupa ndogo kuwa na bei ya shilingi 6 na nusu, ndio shilingi sita na senti hamsini, wakati Konyagi kubwa ilikuwa shilingi kumi na tatu. Guiness for power ilikuwa kinywaji cha kawaida, kule Iringa ilikuwa unanunua ulanzi lita tano  unachanganya na chupa moja ya guiness. Nakumbuka enzi zile za Pwagu na Pwaguzi hiyo ilikuwa baada ya kipindi maarufu cha Mahokaaaaaaaa eeee mama mbavu zanguuu. Nakumbuka enzi zileee wakati kulikuwa na gazeti la Ngurumo, Nyota, kiongozi, Mwenge, Reporter, na hiyo ilikuwa kabla gazeti la Baraza halijapigwa marufuku kutokana na kuandika vituko vya Manaizi kufumaniwa katika ukurasa wake wa pili uliojulikana kama Panapofuka Moshi, mwandishi wake akiwa FJ Khamis. Hiyo haikupishana sana na kufungiwa kwa gazeti la Reporter baada ya kutoa kibonzo kilichoonyesha Mwalimu kapakatwa na Mao Tse Tung wakati Mzee Kenyatta akikimbia mbio. Nakumbuka enzi zileee wakati Wamarekani walikuwa wanadondosha chakula kwa ndege kwenye sehemu zilizokuwa na njaa nchini, na nchi nzima kukaenea mafuta ya kupikia ya msaada, unga wa ugali wa njano, na buluga. Wakati huo Mzee makongoro akiimba Kuleni kuku mayai mboga samaki maziwa. Nakumbuka wakati ambapo RTD walikuwa wakitangaza 'live' dhifa za kitaifa na hapo wakati una njaa hujui utakula wapi unasikia mtangazaji akisema,' Na sasa namuona Waziri Mkuu amepakuwa wali uliopikwa kwa taaluma ya Kichina akiongeza na vipande vya miguu ya kuku iliyokaangwa vizuri na kujazia na sosi ya matunda  ambayo yameagizwa toka Uingereza anaenda pale kukaa na kula chakula kile' Nakumbuka  oh Nakumbuka 

Comments

Anonymous said…
Uwiiiiiiiii mbafu syangu mie, weee kitime zihurumie mbafu syang.
John Kitime said…
Kucheka sana ni dalili ya afya njema. Na hasa wakati wa kucheka kama utaona pumzi zinatoka kwa nguvu kila mahala ni vyema tu. Tatizo wakisikia wambeya