PAKUA HAPA ANKO KITIME APP

Utajuaje kama umelewa?


Mlevi wa ukweli hupitia hatua kadhaa za ulevi, hatua ya kwanza ni BUSARA, katika hatua hii pombe zinakupa BUSARA kuliko mtu yoyote duniani, hapa unakuwa na uwezo wa kuongelea chochote na majibu unakuwa nayo, iwe ni matibabu ya ukimwi au ni namna rahisi ya kuleta maendeleo hapa Tanzania kwa kipindi cha mwezi mmoja tu, yote hayo unaweza kuyaelezea, yakiwa na takwimu na mifano kutka nchi kama Kenya , Uholanzi na hata Iceland. Ukiendelea kulewa kidogo unaanza kuwa MTANASHATI, kwa kweli hapa unakuwa ni mtu mwenye sura ya mvuto, kama ni mwanaume, wadada wote wakikuona tu wanakutaka wao, na ukiwa mdada katika hatua hii hakuna mwanaume duniani anaeweza kukukataa, katika hatua hii, wanaume kwa wanawake huanza kurembua macho, ikiwa ni kama ishara ya uhandsome au ubeauty (wanaume nao hurembua macho sana tu). Hatua inayofuata ya ulevi ni kuwa PEDESHE, katika hatua hii unakuwa na uwezo wa kuagizia mtu yoyote kinywaji hasa wale ambao hawajatambua kuwa unavutia, pesa zinakuwa hazina kazi mfukoni zaidi ya kununulia watu kinywaji, soda hununui wewe ni pombe tu, tena ikiwa na bei kubwa zaidi kwako ni bora zaidi. Ukiongeza ulevi unaingia hatua ya kuwa BAUNSA na kuwa na nguvu kuliko mtu yoyote duniani, katika hatua hii unajikuta unaweza kuruka Kungfu kwa ufanisi zaidi kuliko Jackie Chan, ni hatari sana kwa mtu yoyote kupinga kuwa wewe si MZURI au wewe si PEDESHE wa kutisha au kupinga BUSARA zako ukifikia hatua hii. Mara nyingi ukiendelea na ulevi baada ya hapa unaingia katika hatua ya kuwa na uwezo wa UCHAWI wa kuweza kutokuoneka. Hapa unaweza kuwa na uwezo wa kukojoa chini ya meza katikati ya baa na hakuna mtu anakuona, yaani hapa unaweza kuanza kuvua nguo moja moja na watu hawakuoni kabisa. Nawasilisha hoja.

Comments