HATUPIMI BANDO

WADHAMINI

11 September 2017

HOTUBA YA BABA MKWE ILIKUWA YA MWAKA


Yaani baba mkwe katoa mpya juzi, mpaka sasa bado sijajua nicheke au nisikitike, maana nasema tena baba mkwe katoa mpya. Juzi Jumamosi tulifanikisha sherehe ya harusi ya mtoto wa kiume wa rafiki yetu. Sisi ndio tulikuwa wanakamati hivyo kwanza nijisifu tuliwezesha bonge ya harusi, japo huwa nawaza tu ule mkwanja tuliokusanya wangepewa hawa maharusi hakika wangemaliza umasikini na kuanza maisha ya kifahari, lakini ndio hivyo tena tulipanga kutumia mamilioni yote yale kwa ajili ya kula na kunywa kwa masaa machache tu.

Turudi kwa baba mkwe, sherehe ilianza vizuri kabisa, MC alikuwa mmoja wa wale ma MC ambao wanapenda kusikia sauti zao wenyewe basi anaongea huyo, kila jambo analirefusha mpaka inachosha. Hatimae ikafika wakati MC akatutangazia kuwa baba mkwe anataka kuja kutoa wosia. Binafsi kipengele hiki huwa kinanichekesha sana, kama mtoto hakupewa malezi mazuri, haka kahotuba ka dakika za mwisho ndio kweli katarekibisha tabia zao kweli? Tuache hayo, baba mkwe akakamata maik, akasalimu ‘Mambo?’. Hapohapo nikashtuka, nikaona baba mkwe huyu wa kileo sana, baada ya kumcheki vizuri nikagundua kuwa kinywaji alichokuwa amekunywa vimemchangamsha kidogo. Baba mkwe baada ya kujibiwa salamu zake akaanza hotuba ambayo sitaisahau mapema. ‘Kijana upo? Naona umeamua kumuoa binti yangu, mimi kama baba yake nasema wazi inaonekana humfahamu binti yangu vizuri, mtu anaemfahamu binti yangu hawezi kufanya uwenda wazimu wa kutaka kumuoa huyu mtoto’. Dahh ukumbi mzima ugeuka kimyaa, bibi harusi alikuwa kajiinamia. ‘Huyu binti yangu ni mkorofi katusumbua sana mimi na mama yake, toka alipofikisha umri wa miaka kumi na sita. Kafukuzwa shule tatu, kila shule ikilalamika kuwa anawaharibu wanafunzi wenzie. Hatimae shule ikamshinda, kifupi sijui haswa baada ya hapo alikuwa anaishi wapi. Japo mara chache alikuwa analala nyumbani. Huyu binti yangu hebu fikiria hata instagram walifungia ukurasa wake kutokana na picha alizokuwa akiziweka humo. Nadhani kijana ulimuona picha zake kwenye magazeti ukaona umepata malaika, hafai kabisa huyo hafai. Nimeona nikueleze ukweli usije baadae kunilalamikia mashetani yake yakimpanda. Mimi na mama yake sasa tunaondoka, tulikuja kuwaonya tu ili msije kutusumbua baadae, pole kijana wangu’ Baba mkwe, mama mkwe, mashangazi, wajomba, makaka haooo wakasepa.

9 September 2017

ASANTE SANA BWANA HARUSI


Unajua kila zama zina mambo yake , teknolojia nayo inasababaisha kuweko mambo ambayo wazee kama mimi tunabaki kushangaa tu nini kinaendelea. Katika jambo ambalo limefanya mabadiliko makubwa ni eneo la sherehe za harusi. Enzi zetu watu walikuwa wanatafutiwa wachumba, mwanaume unaambiwa kuna binti umetafutiwa lazima ukubali, na mabinti vile vile wanatafutiwa mume na hakuna kubisha, taratibu zote zinafaywa na wazee wewe unakabidhiwa mzigo tu.

Siku hizi ndugu yangu kila harusi inatengeneza vipengele vipya. Zamani bibi harusi na bwana harusi walikuwa ni watazamaji tu wa sherehe yao wenyewe, siku hizi wanashiriki kila kitu ikiwemo kutoa hotuba. Wiki iliyopita niliingia kwenye harusi ambayo bwana harusi alitoa hotuba kali sana. Baada ya MC kututanganzia kuwa bwana harusi ana machache ya kusema  tukaanza kumsikiliza. Akiwa na suti yake maridadi akakohoa kidogo kasha akaanza, ’Asante MC, kwanza naomba nimshukuru Mungu kwa kumuumba mke wangu, kwa hilo Mungu uko juu. Pili nimshukuru baba mwenye nyumba wangu kwa kukubali niwe na deni la kodi ili kufanikisha harusi hii. Naomba nitoe shukrani kwa bosi wangu kwa kunipa likizo fupi ili nikamilishe shughuli hii. Naishukuru kamati yangu ya harusi kwa kuwezesha kukusanya fedha zilizofanikisha kulipa mahari, nimshukuru mke wa kaka yangu kwa kutuazima gauni la harusi, na kaka yangu kwa kuniazima suti hii niliyovaa. Natoa shukrani kwa mtengeneza keki, leo hakuna kukata keki, nitairudisha keki kwako kesho kama tulivyokubaliana. Nawashukuru wazazi wangu kwa kuja na kikundi cha ngoma toka kijijini, kweli kimeziba pengo la burudani katika harusi hii. Naishukuru kamati ya wazee wa kanisa kwa kufanikisha kumshawishi mke wangu aolewe na mimi, niwape aksante kwa akina mama jirani kwa kuja na vyakula toka makwao ili kufanikisha harusi hii, na vijana kwa kuja na pombe za halali na haramu mradi harusi hii ni furaha tupu. MC wewe ni rafiki yangu nashukuru kwa kukubali tulipane kidogokidogo aksante sana’ Kisha bwana harusi akakaa chini watu wote tukabaki kimyaaaaa


26 August 2017

MJINI KUMEJAA MACHIZI

YAANI hapa mjini ukipaangalia kwa makini unaweza ukajikuta unacheka peke yako barabarani watu wakadhani we chizi kumbe unakumbuka uchizi wa wakazi wa mjini. Yaani kuna vitu watu wanafanya havieleweki, wanajitengenezea mazingira ya kupata matatizo makubwa. Hebu we fikiria, jamaa anakuwa na mabinti 15 kila mmoja anamwambia anampenda kuliko kitu chochote duniani. Wote hao wanamuangalia yeye kwa matumizi yao ya kila siku ili waonekane wa maana mjini, na wote wamemuomba awanunulie simu, wengine Samsung model mpya, wengine iPhone6 na wote amekubali maombi yao, baada ya hapo anaanza kuhangaika kuuza hata mali zake na za kazini kwake ili afurahishe timu yake ya wapenzi. Sasa kwanini nisicheke peke yangu? Wakati huo fala huyu anatakiwa kulipa kodi ya nyumba yake ale vizuri apeleke matumizi kwa wazazi wake, yaani kama sio uchizi huo ni nini? Halafu kuna hawa jamaa ambao wako kibao hapa mjini, utawakuta kila siku baa. Hawa wanaanza siku na kilo mbili za mishkaki na ndizi tatu, kachumbari pembeni, baada ya hapo chupa zinaanza kuteremeshwa na ofa kutolewa kwa marafiki na mashabiki. Na wakati huo zoeezi la kuagiza nyama na supu ya pweza linaendelea tena na tena, kimsingi mpaka jamaa anaamua kuelekea nyumbani kwa mke na watoto wake wane amekwisha tumia kitu kama laki mbili kwa masaa manne. Sasa kwake sasa, watoto wamekula ugali kwa mchicha, tena unga wenyewe ulikuwa hautoshi wamelala na njaa, watoto wamelalia kigodoro cha nchi moja wakishindana kuvutana shuka moja, yeye mwenyewe anapokuja kulala ni juu ya godoro limechoka kabisa anajifunika kanga ya mkewe. Mke alimuachia shilingi alfu tatu asubuhi. Sasa kama sio uchizi huu ni nini sasa? Asubuhi anaamka ana shilingi alfu tano anajifanya mtu mzuri anamwambia mkewe, ‘Tugawane hii we chukua alfu tatu mi nipe alfu mbili hali ngumu mke wangu’. Pambafu.
Halafu machizi wengine ni hawa wazazi ambao mzee mfanya kazi mshahara wake laki nne kwa mwezi, mkewe mama ntilie anauza maandazi, kila saa kumi alfajiri anakuwa tayari yuko mtaani anajaribu kukusanya shilingi alfu mbili tatu, wazazi hawa wakikusanya kipato chao kwa mwezi hakifiki laki saba. Wana binti yao yuko kidato cha pili, ana simu kali mbili, kila moja bei yake si chini ya laki nane. Wazazi wanaona poa tu, hawajui wapi kapata simu, wapi anapata vocha. Tena mara nyingine wanamuomba awapigie simu ndugu na jamaa, kama sio uchizi ni nini? Wacha nicheke barabarani peke yangu mie.

24 August 2017

USHAURI KWA WAPENZI WA ARSENAL

KIKUKWELI kwanza lazima niwape sifa wapenzi na mashabiki wa Arsenal. Hawa ndio wapenzi wa ukweli, sitaki kueleza kwanini lakini wenyewe wanajua.
Hawajali jua wala mvua roho yao kwa klabu yao. Lakini kuna kitu nimeona niongelee nacho ni hii jezi yao mpya (angalia pichani). Kiukweli hii jezi ina matatizo kidogo katika mchezo wa soka tunaoufahamu wengi, hivyo nashauri msitumie jezi hii kwenye mechi zenu kwa kuwa mtavuna magoli yasiyo idadi. Najua kufungwa hakutawafanya muhame timu lakini tukubaliane sio vizuri wakuu kama nyinyi tukisikia mmefungwa magori ishirini. Nadhani jezi hii inaweza kufanya vizuri kwenye timu yenu ya mchezo wa marede, lakini ni ushauri tu asante sana

23 August 2017

19 August 2017

NAKULA CHOCHOTE

Baada ya kubembelezwa sana unamtoa mdada ‘out’, mnaenda sehemu mmekaa.
Wewe: Ehe utakula nini switii?
Mdada: Chochote
Wewe: Nikuagizie ice cream
Mdada: Hapana meno yanauma
Wewe: Haya wacha walete chips kuku
Mdada: Jamani kila siku chips kuku leo tubadilishe
Wewe: Toa wazo basi unataka kula nini
Mdada: Chochote

18 August 2017

MADEREVA KAMA MNATAKA KUJIUA MSITUSHIRIKISHE

Nimewaza sana kuhusu madereva wa bongo, yaani kila nikiwaza najikuta jibu ni moja tu, madereva wa siku hizi ni tofauti sana na enzi zetu. Enzi zetu barabara zilikuwa nyembamba, magari machache tena sio mazuri kama siku hizi, ilikuwa kawaida sana kusikia ajali imetokea kwa kuwa steringi imekatika, au tairi limechomoka, mara nyingine utasikia breki zimefeli. Lakini siku hizi magari yameboreshwa, si rahisi kusikia eti steringi ilichomoka au breki zimefeli lakini ajali ndio zimeongezeka sana. Enzi zetu pikipiki pia zilikuwa za kizamani hazina indiketa, pikipiki zilikuwa na breki za waya ambazo uliweza kusikia zimekatika wakati wowote. Pamoja na hali hiyo ajali za kizembe zilikuwa chache sana.
Sasa siku hizi kama nilivyosema gari zimeboreshwa, pikipiki zimeboreshwa, barabara zimeboreshwa sasa eti madereva nao wameboresha ajali. Madereva wa bodaboda wakiona ajali haziwatokei huamua kuvuka taa nyekundu bila kuangalia kushoto wala kulia. Madereva wa magari nao wakiona siku nyingi hawajapata ajali wanaanza kutuma meseji wakati wanaendesha gari. Sio ajabu ukasikia dreva wa basi aliovateki kwenye kona akiwa spidi kali. Sasa naomba nitoe ushauri kwa serikali. Nimefanya utafiti wa siri nyumbani kwangu, nimegundua kuwa kuna madreva wanakuwa wana ajenda ya siri wawapo barabani. Yaani jama unamuona freshi kabisa anaongea na wewe anacheka kumbe ndani anampango wa kujiua. Au siku hiyo ana hamu ya kuuwa mtu. Dreva akitaka kujiua utaona anachukua simu na kuanza kuchati kwenye simu huku anaendeesha, hapo ujue  anatafuta taimingi abamizwe afe. Kama ni dreva wa bodaboda au bajaji,  utamuona anajipitisha katikati ya magari kwa spidi moyoni anaomba abamizwe afe. Sasa kuna ule wakati dereva anakuwa na hamu ya kuuwa mtu, hapo ndipo ataanza vituko hivyohivyo huku akiwa na abiria, hapo anajua akikosa kumuua abiria basi atampata mtembeea kwa miguu. Sasa baada ya utafiti huu, nashauri trafiki mkimkamata dreva anavunja sheria barabarani sio mnamtwanga faini, haisaidii, mchukueni kwanza mkampime mkojo kama kavuta bangi, kisha mpelekeni kitengo cha kupima akili, ndipo ijulikane adhabu stahiki. Mi nina akili sana mjue.

HAYA KACHUKUE SIMU YAKO SUPAMAKETI

BINTI  mmoja alisahau simu yake supamaket. Meneja wa supa maketi aliangalia kwenye phone book na kukuta namba imeandikwa 'Mama'. Akapiaga na mama akapokea;
MENEJA: Shkamoo mama mwanao kwa bahati mbaya amesahau simu yake hapa supamaket, unaweza kumtaarifu aje aichukue?
MAMA: Marahaba mwanangu, hakuna tabu na asante sana, nitamtaarifu sasa hivi.
Baada ya sekunde chache simu ikaanza kuita, jina lililotokea ni 'Mama', meneja akapokea na kabla hajajibu mama akaanza kuonea
MAMA: We Fulo, angalia ujinga wako sasa, simu umeenda kuiacha supamaketi, haya nenda ukaichukue sasa hivi usirudi bila simu. 

15 August 2017

YANAYOENDELEA KWENYE SUPAMAKETI NI VITUKO PLUS

Juzi niliamua kuzunguka mjini kuangalia vituko vya maendeleo. Yaani we acha tu, ushishangae kuona fenesi zimefungwa kwenye glasi za juis, wala usishangae kuona chandarua kimegeuzwa neti ya kuvulia samaki, mambo yako shaghala baghala.
Lakini shaghala baghala kubwa niliikuta nilipoingia supa maketi. Baada ya kuchunguza kwa makini nikagundua kuna kitu cha ajabu sana kinaendelea ndani ya supamaketi zetu, kumbe sio kila anaeingia supamaketi anaingia kununua bidhaa, watu wana sababu mbalimbali. Aina ya kwanza ya wateja ni wale wanaoingia kujipiga picha, wenyewe wanaziita selfie, yaani hawa wako kibao kila kona unakuta mtu anajipiga picha aonekane alikuwa supamaketi na haraka kuposti whatsap na insta. Katika hili wadada ndio wengi zaidi ingawaje na kwa upande wa wakaka wale wanaovalia suruali nusu mlingoti ndio idadi kubwa zaidi. Sasa hawa wakimaliza kujiselfisha mara nyingi hawanunui chochote ila wakijitahidi sana hununua bigi ji au maji madogo.

Halafu hapohapo wako madenti ambao wanapendana, basi hupanga kukutana supamaketi, hawa utawaona wanazunguka tu humo ndani hawatoki, wanajipiga selfi kibao ingawaje hawazipost insta, halafu mwisho hawanunui kitu. Mapenzi ya shule ni sheeeda.
Kuna kundi la wateja ambao huingia supamaketi na kununua vitu ambavyo hata kwenye genge mtaani kwao vipo, lakini kwa kuwa supamaketi unapewa  mfuko una jina la supamaketi, hii ni swaga kubwa  mtaani, kila mtu anajua uliingia supamaket. Hawa huishia kununua mkate, au chumvi, wakijitahidi wataongeza na blubendi. Halafu kuna kundi la wamama washua, hawa huingia supamaketi na kikaratasi kimeandikwa kila kitu wanachotaka kununua, bahili hao, utakuta wanatembea na kalkuleta, wanaenda hesabu sambamba na mhudumu, mara nyingi hawa huja na watoto wao wakorofi, wanakimbia kimbia hovyo supamaketi, na ni wazi wanasoma intanesho, maana utasikia wamama hao kila dakika wakiita ‘ Junia, junia kam hia, Juni no stop that’ Wazungu weusi flani hivi. Halafu kuna wale wachunguza bei. Hawa huwa hawanunui chochote kazi yao kuzunguka tu supamaketi wanaangalia bei ya vitu, wanashika shika tu. Mara yuko kwenye sabuni, kahamia kwenye chakula mara aangalie sahani arudi kwenye sabwufa, akitoka hapo anaenda kwenye friza hawachoki hawa anaweza kuzunguka
 supamaketi kwa saa tatu kwa siku halafu hanunui kitu.

14 August 2017

WAKUBWA WAZIMA MNAAMINI MAZIMWI?
Mheshimiwa mmoja baada ya kupata cheo si akapewa nyumba mitaa ya watu wenye pesa, akahamia huko akiwa na mke na mwanae. Siku moja mwanae aliyekuwa kazoea maisha ya Uswazi akawa anawinda ndege na manati kwenye uwanja wa jumba lao, bahati mbaya jiwe likapitiliza na kwenda kuvunja kioo cha nyumba ya jirani. Mheshimiwa na mkewe wakaamua kumfuata mwenye nyumba wakamuombe msamaha. Walipogonga mlango akafukua mbaba mmoja akawakaribisha kwa heshima, wakaingia na kuanza kujieleza. ‘Samahani sie tumehamia karibuni hapo nyumba ya pili, mwanetu kavunja kioo chako kwa bahati mbaya, tumekuja kuomba msamaha na kuona kama tunaweza kutengeneza’. Mwenyeji wao akawaomba wakae kisha akawaambia, ‘Naomba niwahadithie kitu. Kwanza mimi nawashukuru nyinyi na mtoto wenu. Mwenye nyumba hii ni mchawi mkubwa sana, mimi ni ZIMWI alikuwa amenifungiwa kwa zaidi ya miaka 200 kwenye kichupa ambacho kilikuwa kwenye dirisha lililovunjwa na chupa nayo ikavunjika nami nimekuwa huru, kwa hiyo kwa shukurani ombeni chochote mtakacho nitawapa, nina uwezo huo’ Hapo hapo muheshimiwa akauliza tena,’Yaani kitu chochote?’ Akajibiwa ‘Ndio’. Basi pale pale akasema, ’ Mimi naomba niwe bilionea mpaka nife’ Akajibiwa ,’ Hilo jambo dogo sana kwangu, umepata na kesho utaamka tajiri’ Mama nae akaomba vyake, ‘Mi nataka niwe na nyumba kila nchi duniani na niwe na biashara Dubai na China na HongKong’ Akajibiwa, ‘Umepata mama, kuanzia kesho hayo ni yako. Mimi nawashukuru kwa uhuru wangu lakini nina kaombi kadogo’. Mheshimiwa haraka akajibu, ’Sema tu wewe ni kama ndugu yetu sasa’ Basi ZIMWI likasema, ‘Naomba mkeo abaki hapa kama masaa mawili tu, unajua kifungo nilichofungwa kilinizuia kila kitu, hata mke sijapata kipindi chote hicho. Nikimaliza tu hilo ntaondoka kurudi kwetu Uzimwini hamtaniona tena, itakuwa siri yetu’. Mme na mke wakajadiliana wakaona utajiri waliopata ni mkubwa sana, na hilo jambo ni dogo sana la mara moja tu tena kwa siri, wakakubali sharti. Mke akabaki pale kwa masaa kadhaa. Shughuli ilipokwisha, mama wa watu akiwa anajitayarisha kurudi kwa mumewe kichwani akiwaza utajiri, ZIMWI likakohoa kidogo na kumuuliza yule mama, ‘Samahani una miaka mingapi na mumeo ana miaka mingapi?” Mama wa watu akajibu, ‘Mie nina miaka 40 mume wangu ana miaka 46’ Yule Mbaba akacheka sanaa, ‘Sasa nyinyi wakubwa wazima mpaka leo mnaamini stori za MAZIMWI?